MSAMAHA WA KWELI?

JINA LA HADITHI FUPI: MSAMAHA WA KWELI ?

MWANDISHI: SAID KAITA

FACEBOOK PAGE: Saidikaitastories.com

BLOG: Saidikaitastories

MAWASILIANO: 0783372139

E-MAIL: Saidikaita7@gmail.com

       Usilolijua ni sawa na usiku wa giza nene. Ni msemo ambao mara chache hutumika katika ndimi za watu ila huwatokea tu muda ambao jambo husika limeshatendeka pia kuwa na uhakika nalo.
       Usiku ulioambatana na sauti za mbu zililizunguka eneo alilokuwa amelala Ahata. Sauti zilizojawa hasira kila mmoja wao akiwa anatafuta kitoweo. Kwa ukali wa sauti zile ulisikika kama mtu akiwa anapiga kinanda kwa utaalamu na hakuna ambaye angeweza kulala kwa sauti zile. Sauti ya makofi ilikuwa ikisikika kila mahali “Paaa... Paaa” kila mtu alikuwa akijihami asing'atwe. Ahata alikuwa amelala chini ya kalavati akiwa amejifunika na mfuko wa kubebea uchafu. Mbalamwezi iliyokuwa iking'aa angani kwa namna yake iliweza kutoa nuru na kufanya watu wengi waliokuwa wamelala pale kushukuru. Muda huo hakuna aliyekuwa akifanya mazungumzo na mwenzake bali kila mtu alifikiria ni nini alichofanya mchana. Upande wa pili wa kalavati nako palionekana vijana wakiwa wamelala kwa kupanga msitari. Aliyepata box la kulalia alishukuru Mungu na aliyekosa basi ilimbidi avumilie. Sauti ya Ahata ilisikika ikwia imejawa na malalamiko juu ya mbu wanavyowasumbua. “Laaaa laaa laaa... hawa mbu ndiyo wameniamlia hivi?... kama nina ugomvi nao? Eee Mungu embu saidia hawa viumbe wako unaowaona hapa. Tunapata tabu sana katika maisha yetu, nini kabisa tumekukosea? Mchana tunafanya kazi ngumu na hela ndogo, usiku tunalala sehemu ambayo si rafiki kiafya Kabisa. Lini utatutoa huku? Kila siku maombi yangu nimekuwa nikikuomba niondokane na hali hii mimi na rafiki zangu. Ni mwaka wa nne huu umepita tangu nimeanza kuhangaika na haya maisha. Mbona mimi bado tu kiumri lakini maisha yangu yameshaanza kuonekana magumu kama vile mwamba? Wazazi wangu kufariki ikawa ndiyo chanzo cha mimi kuwa hapa? Ama kweli mwanadamu hata awe ndugu yako vipi muangalie usoni tu sababu moyoni humjui. Kuwa nao makini sana... Leo mimi ni wa kuhangaika hivi kweli? Kwangu mvua ikija sawa naipokea, ikija baridi kali kwangu naipokea na hata ukija upepo mkali vyote vyangu tu. Vyote vinanipiga mimi na wenzangu huku ambao hatuna hata pakukimbilia. Ukikimbilia kibarazani kwa mtu ndiyo hivyo utaitwa mwizi, wanadamu walivyo na roho za kinyama utaona watakavyokufanyia. Eeee Mungu waweke wazazi wangu mahala pema, wambie wameniacha katika hali mbaya sana, ila sina namna ntahesabu nyota weee hadi usingizi unijie”. Mahali hapo palikuwa pamejaa harufu za sigara na bangi. Mipishano ya kukohoa haikuepukika kutokana tu na kazi ngumu za mchana walizokuwa wakifanya nyingine zikiwa ni za vumbi zaidi. Hata kama ni za vumbi hakuna aliyekuwa na ratiba ya kununua maziwa ili kujiweka vizuri. Ilifikia kipindi Ahata usiku anakula mkate na maji tu.
Alfajiri na mapema ilipowadia sauti za kuwaamsha waislamu kwenda kufanya ibada zilisikika. “swalaaa swalaaa... Swala ni bora kuliko usingizi...” Japokuwa sauti zile zilikuwa ni za kuwajulisha watu kwenda kusali lakini kwa Ahata na rafiki zake ilikuwa ndiyo muda wao kujiandaa na kwenda stendi kubeba mizigo ya abiria. Aliyekuwa na mkokoteni aliufuata na kuuchukua kuanza nao kazi, aliyekuwa na guta naye alifanya hivyo hivyo. Ila kuna baadhi ambao hawakuwa navyo hivyo wao walikuwa ni kubeba mzigo begani tu. Ahata alijiandaa kwa kujifuta matongotongo bila hata kupiga mswaki safari ikaanza.
Palipozidi kupambazuka kila mtu alizidi kuumiza kichwa ni wapi pakupatia kibarua. Hata jua lilipowaka Ahata wala hakujali sababu hata aseme apumzike alijua kabisa mjini hakuna hela ya bure. Ukisema ukaibe dakika utajikuta kwenye tairi. Ahata alionekana akiwa amekaa pekee yake huku akiwa ameshikilia kimfuko cha maji akipunguza kiu. Akiendelea kunywa alitokea jemba lenye miraba minne na kumwambia. “Leta maji hayo”. Ahata alikataa na kutaka kuondoka sehemu ile lakini pande lile la mtu dakika tu alimpiga teke la makalioni, kwa uzito wa teke lile Ahata alianguka chini na maji yakadondoka yakawa hayana hata sura ya kunywewa. Alichafuka kwa vumbi lililokuwa pale chini. Ahata alikuwa ni mdogo sana kwahiyo hata hakuweza kumfanya lolote bali alibaki kulia tu akiwa pale chini jemba lile nalo likawa limeondoka. “Jamaa hili jinga kweli badala litumie nguvu zake kutafuta pesa halali linabaki kuonea watu tu” Ahata alisema, aliinuka na kujikung'uta nguo zake ambazo zilionekana ni chafu sana zimejaa oil tu. “Daa sema afadhali halijachukua vidala vyangu vilivyokuwa mfukoni”. Wenzake walibaki kumwangilia tu sababu hawakuwa na uwezo hata wa kumpiga mwanaume yule.
          Usiku ulipoingia kila mtu alianza kuangalia ni wapi atakapolaza mbavu zake na kuanza kuota ndoto za kujenga angani angali amelala chini. Ahata akiwa na rafiki yake walikuwa wakilonga za maisha huyu akinena hivi na yule vile. “Sasa Ahata haya maisha tutaenda nayo hadi lini? Sababu naona kila kukicha hela zenyewe ndiyo hivyo shida tu”. Rafiki wa Ahata alikuwa akinena hivyo kisha Ahata akasema. “Yaani rafiki yangu kwa hali hii mafanikio ni vigumu kwetu. Sababu angalia kwanza hela tunayopata ilivyo ndogo, kazi tunazofanya ni ngumu sana ambazo zinazidi kutuletea maumivu kwenye miili yetu tu. Wala hatutumii hata dawa, nini tunajitakia? Yaani leo mimi nina miaka kumi na mbili lakini sura yangu inaonekana kama nina miaka arobaini” “Sasa Ahata unaonaje ili tuondokane na hii hali?” Alikaa kimya kwa sekunde chache huku akiwa amempiga mbu aliyekuwa akimng'ata kisha akasema “Mimi hata sielewi”. “Ahata unajua kuna story naambiwaga kuhusiana na hawa watu waliotajirika sana. Wengi unaambiwa walikuwa hoehae kama sisi tu, mwishowe wakaamua kwenda kujiunga na freemason ndiyo maana wakafanikiwa hivyo. Usiwaone tu wanaendesha magari ya bei ghali hivyo”. Ahata akamuuliza swali. “Freemason ndiyo kitu gani hicho?”. “Ahaa huko unaambiwa ukiingia kuna masharti wanakupa tu ukishatekeleza tu tayari unaanza kufanikiwa” Ahata aliuliza. “Masharti kama yapi?” “Wengi huwa wanasema unatakiwa umuue mama yako kwa vile ndiye unayempenda sana”. Suala la kumuua mama lilimuuma sana Ahata kwa kuwa anajua uchungu wa mzazi, isitoshe mama yake aliuliwa kikatili sana. “Daaa unajua rafiki yangu hadi hapo mimi siwezi kabisa kusikiliza hilo wazo lako. Kwa sababu kumuua mama wakati mama yangu aliuliwa kikatili na ninajua uchungu wa mzazi weee? Embu hiyo mada kwangu usiiweke kabisa. Yaani nikija kukua na nikijua ambaye aliwaua wazazi wangu kikatili vile yaani atakiona cha mtemakuni”. Rafiki yake alimuomba msamaha Ahata kwa kuwa alimkumbusha maumivu makali ambayo yalimtokea miaka minne iliyopita. Kukatika kwa mazungumzo yale yaliwafanya kila mtu aanze kunyemelewa na usingizi na kulala fofofo. Ikiwa ni usiku wa manani ghafla ilikuja mvua kali dakika chache tu mawingu yalitanda. Mvua ilianza kwa kasi sana na kufanya watu waliokuwa wamelala hapo kulowana sana. Ambao walikwa wamelala chini ya makalavati kilichowashtua ilikuwa ni mafuriko yaliyokuwa yakija kwa kasi sana yakiwa na kila aina ya uchafu, walifanya haraka haraka na kila mtu akaanza kujiokoa na kutoka nje.
******************************************
         Ilipopita miaka saba mbeleni Ahata alipata nafasi ya ufadhili kutoka katika shirika la kizungu lililokuwa na makao makuu yake huko Denmark. Shirika lilijukana kama Youth Talent Arise Organization (Y.T.A.O) ambalo liliweka pia tawi katika taifa la Zatan. Lilishughulika na kuinua vipaji kwa vijana. Ahata alipata nafasi huko baada ya kuonekana kuwa alikuwa na vipaji vingi tu kama vile uimbaji, uandishi wa hadithi na uchoraji. Siku ya mashindano Ahata alifanya vizuri na ndipo akawa amesajiliwa Y.T.A.O kwa jina la Ahata Esbern. Ambapo Esbern lilikuwa ni jina la mwanzilishi na mmiliki wa Y.T.A.O. Alimpenda sana Ahata na kumhakikishia kuwa atamhudumia vizuri, mmiliki yule alimjengea kasiri ili kumfanya Ahata aishi kwa raha msitarehe. Esbern aliamua kumtembeza Ahata katika mataifa mbalimbali na watu wakamjua zaidi kupitia kipaji chake. Ahata alizidi kukosha nyoyo za watu hadi ilifika kwa mwaka alitumbuiza katika matamasha makubwa zaidi ya mia. Kwa mwaka mmoja tu alipata tunzo nyingi sana. Hadi wizara ya michezo nchini Zatan ilimpatia tunzo kwa namna alivyokuwa akiipeperusha bendera ya Zatan kupitia kipaji chake, kila mtu alimjua Ahata na kuzidi kumpenda, sura yake ilinawiri sana kama nyota yake ilivyo. Hata na kupata umaarufu vile Ahata hakuwasahau watu wa chini ambao alihangaika nao huko mtaani zaidi ya miaka kama kumi. Aliwapatia fedha na kufanya Ahata azidi kuimarika kwa rafiki zake. Ndugu wa Ahata ambao walimdhulumu mali za baba yake na kumfukuzia mbali walianza kumtafuta na kutaka wapatiwe msaada, kwasababu mali zile wala hawakuzifanyia maendeleo yoyote. Kama ilivyo pesa za dhuluma siku zote hazinawirishi chochote.
        Baba wa Ahata alikuwa ni tajiri mkubwa tu katika eneo alilokuwa amezaliwa. Alikuwa ni tajiri kijana mwenye upendo sana kwa wananchi wenzake. Ahata alipofikia umri wa kujielewa ndipo baba yake akaamua kugombea ubunge. Harata ambaye ni baba wa Ahata alikuwa na wafuasi wengi sana. Lakini mpinzani wake hakuwa na wafuasi wengi japokuwa aligombea kupitia chama tawala cha Zatan kilichojulikana kwa M.K. Mbunge yule kutoka M.K hakupenda hali ile na kuona atashindwa ndipo alipoamua kufanya njama za kumuua Harata, mkewe pamoja na Ahata. Lakini hakufanikisha kumuua Ahata kwasababu siku ya mipangilio yote hiyo Ahata hakuwa nyumbani.  Baba wa Ahata na mama walichinjwa kisha vichwa vikazikwa na miili yao kukutwa imetupwa barabarani. Kiongozi wa M.K alipoulizwa na vyombo vya habari alikana katu katu kuwa hakuhusika na mauaji hayo ya kikatili.
           Mwenyekiti wa Y.T.A.O nchini Zatan alikuwa akiitwa Simba ambaye alifanikiwa kuwa na watoto wawili, mtoto wake wa kwanza ni wa kiume na wa pili ni wa kike. Mwanaye wa kike alijaaliwa uzuri sana hata angeamua kuwania umiss basi angeshinda. Alitumia uzuri wake na kumshawishi Ahata kuwa mpenzi wake. Ahata wala hakusita na kuona kuwa ameamka kitandani na kukuta kifungua kinywa kimeshaandaliwa. Dada huyo alijulikana kwa jina la Aisha. Aisha alijaaliwa uzuri ambao kila aliyemuona mahali fulani basi alisimama na kumuangalia hata dakika moja kabisa. Asubuhi na mapema kwenye vichwa vya magazeti palijaa taarifa iliyokuwa ni habari picha ukisema.  “Ahata apata kigori”. Esbern alimpa Ahata hongera sana kwa kuwa amefikia maamuzi mazuri kwa muda muafaka.
           Dunia nzima ilisikia na kuona uhusiano huo kama walivyotambua vipaji vyake. Maandalizi ya harusi yalianza vizuri sana, kadi za mwaliko zilitumwa katika kila kona za dunia. Maandalizi yote yaliwezakufikia mahala pazuri hadi kufika asilimia tisini na tano. Mungu si Athumani dunia haina siri asubuhi na mapema magazeti yalijawa na taarifa isemayo kuwa Ukweli Wabainika kuhusu mauaji ya Harata UK 04. Kichwa cha habari kile kiliwavutia sana wanunuzi wa magazeti na kufanya wanunue wengi sana. Ahata pia alipenda sana kusoma magazeti asubuhi kabla hajaanza maandalizi ya ratiba za siku. Akiwa kwenye bustani amekaa kwa pembeni palikuwa na chai iliyokuwa imewekwa kwenye meza ndogo hivi. Alishtushwa sana na taarifa ile ndipo akaamua kufunua moja kwa moja ukurasa husika. Alianza kusoma gazeti lile ambapo mwisho wa habari ile palionekana picha ya aliyekuwa mbunge wa M.K na sasa ni Mwenyekiti wa Y.T.A.O bwana Simba. Habari ile ilitoa ukweli wote juu ya mauaji ya Harata. Ahata alichanganyikiwa sana baada ya kuisoma habari ile. Aliwasiliana na Aisha awasili nyumbani kwake haraka sana. Aisha hadi anafika pale nyumbani hakuwa anajua lolote kwa kuwa Aisha hakuwa mfuatiliaji wa magazeti sana. Hali aliyomkuta nayo Ahata ilibidi ashangae sana, kisha akamwambia Aisha. “Soma hilo gazeti ukurasa wa nne alafu utaniambia”. “Alilisoma kwa ufasaha na alipokutana na jina la Baba yake pamoja na picha za Baba yake alichanganyikiwa sana. Alianza kujitetea sana kuwa ile habari si ya kweli huku akimuomba wasije wakaachana”. “Ahata ndiyo unataka kuniacha kwa kuwa umejua ukweli wote huo. Ila mimi sikuwa najua kabisaa. Naona ni uongo huo. Wanataka kumchafua Baba tu”. Muda wote Aisha alikuwa akiongea Ahata alikaa kimya tu. Ghafla simu ya Aisha iliita na alipoangalia ni Baba yake ndiye aliyempigia na Ahata akasema.
 “Pokea simu yako”.
 “uko wapi mwanangu. Nakuomba njoo nyumbani haraka”.
“Baba Niko kwa Ahata hapa”.
Simba kusikia hivyo hapo hapo aliachia simu akaanguka chini na kuzimia. Haraka haraka matabibu waliitwa ili kumshughulikia. Ahata alimjulisha Esbern mkanda mzima na bahati kipindi hicho Esbern alikuwa Zatan ndipo Esbern akamwambia Ahata wakafanye mazungumzo kwa Simba. Ahata na Aisha walielekea moja kwa moja hadi kwa Simba. Muda si mrefu Esbern aliwasili na kumkuta Simba ameshazinduka, Simba alipungua sana mwili kwa taarifa zile. Walimsubiri Simba apate nafuu ndipo wakaanza mazungumzo ya mapatano.
          Ilibidi Esbern aongoze kikao bila hata kuegemea upande wowote ule. Bali aliendesha kikao kile kwa lengo la kuwasuluhisha. Palikuwepo Esbern, Ahata, Simba, Aisha na mke wa Simba. “Aaaaa... Ahata najua ni namna gani una hasira, ni namna gani kichwa kinakuuma, ni namna gani unavyofikiria kuwa katika hili unaweza kumkosa Aisha au laa. Pia, unafikiria ni namna gani utakavyopoteza watu muhimu sana ambao wamekutoa katika umaskini na leo wewe ni nyota wa Zatan na hata nje ya Zatan wanakutambua kuwa wewe ni nyota mkubwa mwenye kipaji kweli. Ulitamani sana leo hii uwe unatumia mali zako na familia yako yaani Baba na mama. Lakini kamwe inashindikana na yote hii ni kutokana na namna mtu fulani alivyokufanyia familia yako. Ila Ahata niseme tu kwamba leo hii umejua ukweli wa kifo cha wazazi wako na unataka kulipiza kisasi. Sawa utalipiza kisasi ila jua kama chuki yenu kamwe haitoisha. Leo ukikubali Simba auliwe tambua hii nayo ni familia hivyo lazima nawo wataanza kupanga namna tu ya kukuua, sababu nawo wanampenda baba yao, wanampenda mama yao na wote wanapendana. Huoni ukifanya hivyo hizi familia zitakuwa ni za kumwaga damu kila kizazi? Kumbuka kama umezaliwa Mungu ndiye aliyepanga uzaliwe, siku zote yeye ndiye hupanga mtu azaliwe kwa namna atakavyo na mtu akishazaliwa kifo kwake ni lazima. Basi kama Mungu ndiye muumba wetu yeye ndiye anayeamua ni namna gani vifo vyetu vinavyotakiwa kuwa. Mimi siyo mwamini sana na mambo ya kidini ila napenda kusoma vitabu vya kidini ambavyo vinanipa maarifa sana. Ahata nakuomba legeza moyo wako, shusha hasira yako juu ya hili, angalia suala hili lisije likakuchafulia jina lako kabisa”. Ahata alikuwa amekaa kwa makini akiwa anamsikiliza Esbern ushauri wake. Maneno yale yalimwingia sana na kuyatafakari kwa kina sana. Mazungumzo yalienda vizuri ndipo Ahata akapatiwa nafasi ya kuzungumza yake kutoka moyoni. “Sina mengi ya kunena bali machache ya kupatanishana, siku zote mtu ukiwa na hasira unaweza ukatoa maamuzi ambayo yanawezakuwa ni mabaya sana kwako. Natambua fika kuanza kwa vita humaanisha kumalizika kwa vita na ndipo mgogoro utaisha. Ila niseme tu hili limeshatokea na lilitokea kwa wazazi wangu tena nikiwa mtoto tu. Mimi kulipa kisasi suala hili kwangu ingekuwa ngumu hata kama Aisha asingekuwa mchumba wangu. Ila yote hii pia ni kwa ushauri mzuri wa Esbern wenye ushawishi na sina hata kukulipa mkuu.  Natambua uchungu wa wazazi wangu na namna walivyouliwa kikatili. Sidhani mimi kulipa kisasi ndiyo itakuwa mwisho wa visa hivi, bali ndipo itakuwa mwendelezo wa visa vingine kwa vizazi vya ukoo wa leo na vizazi vya ukoo wa kesho. Nikilipiza kizazi na kizazi kijacho kitalipa hili kwangu. Niseme tu Baba nimekusamehe. Unawezakujiuliza huu ni Msamaha wa kweli?” Simba alijibu harakaharaka, “Ndi... Ndi... Ndiyo ... Lazima niulize Ahata... Huu Msamaha wa Kweli? Sababu najua ni kosa kubwa nililolifanya. Nilifanya mauaji yale kwasababu tu nilikuwa na tamaa na nafasi ile ya uongozi. Uchu wa madaraka ulinifanya niusahau utu kabisa angali na mimi ni mtu. Nilitanguliza matamanio yangu kwa kuwaaminisha wananchi kuwa mimi ni Kiongozi mwema angali sikuwa hivyo. Wengi tunatamani matamanio yetu yakamilike hata kwa kumuangamiza mtu fulani ambaye anaonekana ni kama kizuizi cha mipango yake”, Ahata alimkatisha Simba maongezi na kusema “Niseme tu kuwa Simba huu ni msamaha wa Kweli”. Simba alishukuru sana na huku Esbern akiwa amemuonesha Ahata kinasa sauti kama ushahidi wa walichokiongea. Kwa ujumla Esbern alijaaliwa sana maongezi ya ushawishi na ndiyo maana hata aliweza kumshawishi Ahata kutupilia mbali chuki hiyo.
          Ahata, Esbern na Aisha baada ya kumaliza yote pale walitoka nje ya geti la Simba kuelekea mahali walipo yaacha magari yao. Hapo nje walikutana na umati wa waandishi wa habari ukiwasubiri kwa hamu sana. Kila mwandishi tayari alikuwa amejikoki maswali ya haraka haraka kwao. Walishangaa sana kukutana na umati wa waandishi wa habari ukiwa wanawasubiri pale nje.
“Ahata vipi ndiyo mipangilio ya arusi imevunjika?” mwandishi aliuliza
“Hatuelewi Ahata asubuhi yote kwa adui yako! Ahata mbona bado uko na Aisha?” wengine wakionekana kudaia. Ni baadhi ya maswali yaliyosikika yakiulizwa na waandishi wa habari. Muda wote Ahata, Esbern na Aisha bado walikuwa wamepigwa bumbuwazi kwa waandishi wa habari waliokuwa wamejaa pale. Ahata alijifikiria kwa sekunde chache alitamani kuondoka lakini alifikiria kuwa kukimbia tatizo siyo kusuhisha tatizo. Alijikaza kiume na Esbern akampa moyo.
        “Habarini ndugu waandishi wa habari. Kumradhi nitazungumza nanyi kwa ujumla juu ya yaliyotokea. Maswali machache niliyoyasikia kutoka kwenu bado yapo kichwani nimeyanasa vizuri. Niseme tu kwamba ndugu waandishi wa habari ninyi nawajua vizuri. Lengo lenu kuu ni kupata habari na habari hizo tena ziwe endelevu. Ni kazi yenu na ni jukumu lenu na hapo nitawapa hongera. Natumai mnatamani sana niwapatie majibu ambayo ninyi mnayategemea na siyo yangu. Nipende kusema tu kuwa yote na yote yaliyotokea hayo ni juu yangu na mimi ndiyo muumivu wa yaliyotokea bali kwa jamii ni mfaidishi kwao. Tayari tumeshafanya mazungumzo na Simba na yote yameshaisha na mwafaka tulofikia si kuendeleza vita bali ni kusimamisha vita. Japokuwa siku zote katika chuki za kivita kuisha kwa vita, hivyo lazima kwanza watu wapigane ndiyo vita itaisha. Lakini kwa mimi nimeona kuwa sina Muda wa kuendeleza vita sababu yote hiyo ilikuwa ni mipangilio ya mungu tu. Kulipiza kisasi itamaanisha kuwa na mimi nitakuwa hatarini daima. Sitaki kufanya kuwa hiki kizazi kiwe kizazi cha kumwaga damu kama Simba alivyokuwa ameanzisha. Maombelezo ya vifo vya wazazi wangu nilishanfanya miaka mingi iliyopita. Wakati huo nilikuwa na mawazo hayo hayo ya kulipiza kisasi. Lakini siku hazifanani kamwe na kila kimbunga kina urefu wake na nguvu yake. Natambua kuwa dunia itashangaa kwa maamuzi yangu ila ndiyo hivyo jukumu huitwa hukumu kwasababu ya maamuzi tu.  Kuhusu uhusiano mimi na Simba bado uko karibu. Bado ninamheshimu akiwa kama mwenyekiti wa Y.T.A.O na baba mkwe wangu mtarajiwa. Kusema hivyo ninamaanisha kuwa maandalizi ya arusi yapo palepale na tarehe iko palepale. Ninashukuru kwa gazeti lililochapisha habari hiyo, kwasababu limeweza kunijulisha mambo makubwa ambayo sikuwa nayajua. Nitajitahidi kufanya nao mazungumzo kwa jambo hili. Hivyo, sina budi kusema kuwa kumradhi kwa mliyokuwa mkiyategemea. Nikushukuruni kwa ujaji wenu hapo”. Ahata na Aisha waliingia kwenye gari moja na Esbern akawa amepanda kwenye gari lake. Madereva walirudishia vioo na Safari kuanza. Aisha na Ahata walielekea kulia na Esbern alielekea kushoto.
         Karibia dunia nzima ilipata habari hiyo na mazungumzo hayo yaliporushwa katika mitandao ya kijamii kila mtu aliliongelea suala hilo kwa namna yake. Wako walitamani Ahata alipize kisasi na wengine wakimuunga mkono. Wengi walitoa maoni yao wakisema kuwa amepumbazwa na uzuri wa Aisha, wengine wanasema kuwa Simba amemloga Ahata akawa ameduwaa tu. Mwaka huo huo Umoja wa Mataifa uliwapatia Ahata na Esbern tunzo ya Amani baada ya masuluhisho yale.
         Siku zote hatua tano unazotaka kuzipiga mbele hujui kama zitakamilika. Usijeukajificha ukasema hakuna aliyekuona bali Mungu anakuona na atatumia namna yoyote siku moja uje uonekane tu. Kulipiza kisasi siyo kwamba ndiyo kumaliza chuki bali ni hatua ya kuendeleza chuki.
                            TAMATI

Comments

  1. Habarini ndugu wasomaji wa hadithi zangu. Napenda kuwakaribisha muweze kujisomea hadithi fupi niliyoiandaa inaitwa MSAMAHA WA KWELI ?. Ni hadithi yenye kuelimisha sana natumai baada ya kusoma hadithi hii mengi utakuwa umejifunza sana.
    Maoni yako ni muhimu sana kwangu.

    Karibu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wooooooow hongeraaa, ni nzuri Sana rafki yng

      Delete
  2. Hongera Sana kijana, well unique crieted

    ReplyDelete
  3. Hongera Sana kijana, well unique crieted

    ReplyDelete
  4. Thanks you to what you doing congrturation and keep it rise sadik

    ReplyDelete
  5. 🤙🤙🤙 big up Broo we a together

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

WIMBO WA AFRIKA MASHARIKI (EAC)

SIRI

PESA ILIVYO