ZUCHU

MUSTAKABALI WA MSANII ZUCHU (ZUHURA OTHUMANI) BAADA YA MIAKA MITANO IJAYO
MWANDISHI NA MCHAMBUZI: SAID H. KAITA MAKALA NAMBA MoJA (2020) +255783372139 1.0 UTANGULIZI Uchambuzi katika makala hii utazungumzia historia fupi ya ZUCHU na hatua hadi kufikia katika muziki, maisha yake ya muziki baada ya kuingia katika lebo kubwa ya muziki barani Afrika iliyopo nchini Tanzania chini ya msanii Diamond Platinumz, Wasafi Classic Baby (WCB Wasafi). Katika uchambuzi huo mfupi ndipo tutakapotoa mustakabali wa ZUCHU baada ya miaka mitano katika muziki atakuwa katika hatua gani? Uchambuzi huu hautajikita katika kutetea upande fulani kwa hisia bali ni kuangalia mambo ya hakika ya msanii ZUCHU na kumpatia mustakabali wake. Mwisho, makala itatoa maoni na ushauri kwa ZUCHU. 2.0 HISTORIA FUPI YA ZUHURA OTHUMANI (ZUCHU) Zuhura Othman (ZUCHU) ni mtoto wa mwisho katika familia yao. Mama yake akiwa ni moja ya wasanii wakubwa wa muziki wa taarabu na mduara ambaye anajulikana kwa jina la Khadija Kopa. Tarehe 17/04/2020 Kupitia mahojiano yaliyofanyika katika channel ya Wasafi FM masafa ya 88.9 Dar-es-salaam na Wasafi TV katika kipindi cha "the switch" kilichokuwa kikirushwa mubashara kupitia YouTube akaunti ya Wasafi Media, muongozaji mkuu wa kipindi alikuwa ni Lil Omy. ZUCHU aliongea haya. Ninanukuu. "Na mimi ni mtoto wa mwisho katika familia. Tangu kuzaliwa nimekuta tayari mama yangu anaimba. Mimi sijamkuta mama yangu anafanya kazi nyingine zaidi ya muziki. Role mode (muigwa) wangu wa kwanza ni mama yangu". ZUCHU Tafsiri hapo juu ni yangu. Zuhura Othuman (ZUCHU) alizaliwa mnamo 22/Novemba/1996 jijini Dar-Es-Salaam. ZUCHU amejaaliwa kipaji cha uimbaji na uandishi wa nyimbo. Tasnia ya muziki anaoimba ni Bongo Fleva, Afro-Pop. Jina ZUCHU limetokana na muunganiko wa majina mawili ambayo ni Zuhura na Othumani. ZUCHU anasema mwanzoni ilibidi iwe ZOCHU kutokana na jina Othuman kwa mkato alikuwa akiitwa OCHU ndipo wakaona ni vyema zaidi kuita ZUCHU. Haya yote aliyaongea kupitia Wasafi FM ambapo mahojiano haya yalioneshwa mubashara kupitia YouTube akaunti ya Wasafi Media na kuoneshwa mubashara pia katika Wasafi TV ikiwa ni 17/04/2020. 2.1 MAISHA YAKE KATIKA MUZIKI ZUCHU ni msanii aliyejaaliwa kuzaliwa katika familia yenye kufanya kazi za muziki mbali na kusikia muziki kwa wasanii wengine. Pia, mama yake ambaye ni Bi Khadija Kopa ni msanii mkubwa sana wa muziki wa taarabu na mduara ambaye ameweza kushika masikio ya mashabiki kwa muda mrefu sana. Jambo hili ndilo hata liliweza kumpa njia kwa yeye kuweza kutambulika kipaji chake. Hii ni tofauti na baadhi ya familia nyingine za kiafrika kuwa mtoto asemapo ana malengo ya kuwa msanii mara nyingi familia yake humchukulia vibaya bila hata kufikiria matunda yake. ZUCHU aliyathibitisha haya kupitia mahojiano yaliyofanyika tarehe 17/04/2020 katika channel ya Wasafi FM masafa ya 88.9 Dar- Es-Salaam kwenye kipindi cha the Swich na mahojiano hayo yalioneshwa mubashara kupitia YouTube katika akaunti ya Wasafi Media. ZUCHU alisema. "Yeah (ndiyo)... Kwa asilimia kubwa mama yangu, familia yangu ndiyo influencer yangu ya kwanza ya mimi kuwa mwanamuziki. Kwa sababu nimekuwa nikisikia muziki nyumbani kwetu ukipigwa, ukifanyiwa mazoezi, You know (unajua) mama yangu kipato chake kikubwa kabisa ni kupitia muziki wake" ZUCHU Tafsiri hapo juu ni yangu. ZUCHU amekuwa katika harakati za muziki kwa muda mrefu kama wasanii wengine ambao ni chipukizi wanavyohangaika ili kupata jina katika tasnia ya muziki. Tangu zamani ZUCHU alikuwa na malengo ya kufanya kazi na msanii Diamond Platinumz katika lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB). Kwa malengo hayo ndipo mama wa ZUCHU alipoamua kumpeleka katika lebo kubwa ya muziki barani Afrika ili kuweza kujiimarisha katika kipaji chake cha muziki. Haikuwa rahisi kwa ZUCHU kutangazwa kuwa amesajiliwa katika lebo ya WCB. Hii ni kutokana na muda ambao amekaa katika lebo hiyo ikiwa ni kwa muda wa miaka minne. Tangu 2016 amekuwa akijionea wasanii mbalimbali wakitangazwa kuwa wamesajiliwa katika lebo ya WCB. Jambo hili kwake lilikuwa likimuumiza sana moyo huku akijiuliza ni lini atatangazwa kuwa naye amesajiliwa katika lebo ya Wasafi? Hata marafiki zake walikuwa wakimuuliza sana swali hili. Swali hili lilikuwa likimuuma sana na hakika yeye akiwa anajionea wasanii mbalimbali wanavyosajiliwa katika lebo kubwa ya muziki barani Afrika ambayo ni Wasafi. Alipiga moyo konde akitambua kuwa siku zote mipango yoyote ya kheri lazima ikumbwe na changamoto na inahitaji kuendewa pole pole. Hivyo, uvumilivu ni jambo la msingi ndipo kuweza kuyafikia malengo kama haya. Uvumilivu ndicho kitu kikubwa kilichomsaidia ZUCHU kuweza kusajiliwa katika lebo ya Wasafi na wala si uhusiano wa karibu kati ya boss wa WCB Diamond Platinumz na Mama wa ZUCHU bi Khadija Kopa kama maneno yalivyokuwa yakisambaa katika mitandao ya kijamii baada ya ZUCHU kusajiliwa Wasafi. Tarehe 17/04/2020 Kupitia kipindi cha the switch kinachorushwa kupitia Wasafi FM masafa ya 88.9 Dar-Es Salaam na Wasafi TV na kuoneshwa mubashara katika akaunti ya YouTube ya Wasafi Media, ZUCHU aliongea haya hadi kusainiwa Wasafi. ZUCHU alisema. "Nilikuwa Wasafi kwa muda wa miaka minne. Lakini watu wengi walikuwa hawajui, watu wanahisi sababu ya mtoto wa Khadija Kopa. Kwangu mimi imekuja labda nimeletewa chakula mdomoni. Nimehustle (pambana). Kwa hiyo miaka minne nilikuwa nafanya harakati za muziki. Lakini hapo nilipoletwa WCB boss hakunichukua palepale sababu ni mtoto wa Khadija. Ilibidi niwaaminishe kwamba nafaa". ZUCHU Tafsiri hapo juu ni yangu. Ilipofika tarehe 09/April/2020 kupitia ukurasa wa ZUCHU wa Instagram ndipo alipowajulisha mashabiki zake kuwa amesajiliwa katika lebo ya Wasafi. Aliandika haya; "It is a huge honor final fulfill my dream () na pia baraka na bahati kubwa sana to be signed under the biggest lable in Africa WCB (kusainiwa chini ya lebo kubwa Afrika WCB) nikiwa kama mwanamke mwenye ndoto yangu kubwa ni kutumia kipaji changu kuthibitisha ule usemi. " Power is not given to you, you have to take it". (Haupewi nguvu, unatakiwa uichukue". Tafsiri hapo juu ni yangu. Kusajiliwa kwa ZUCHU katika lebo hii hakika kulikuwa na mapokezi makubwa sana katika mitandao ya kijamii mbalimbali. Kwa kipindi hicho alikuwa akitamba na wimbo wake mpya uitwao WANA ambao aliuachia katika akaunti yake ya YouTube tarehe 9/April/2020. Hakika ZUCHU tangu kutangazwa kuwa ni moja ya wasanii waliosajiliwa katika lebo kubwa barani Afrika yaani Wasafi alianza kuonekana ni mwenye kipaji cha hali ya juu sana. Hii ni baada ya kusajiliwa na kuweza kuachia wimbo wake ambao ulihusisha audio na picha jongeo (Video) mnamo tarehe 09/April/2020. Ni wimbo wake wa kwanza lakini hapa aliweza kuonesha hakika ana kipaji na ana haki ya kusajiliwa katika lebo ya WCB. Kwa sababu Wasafi ni lebo kubwa barani Afrika ambayo huchukua wasanii wenye kipaji cha kuimba. Wimbo ulienda kwa jina la WANA, kuanzia mashairi, picha jongeo (Video) vyote vilikuwa vizuri katika wimbo huu ambapo picha jongeo ilichukuliwa na director Kenny kutoka katika lebo ya WCB. Kikubwa kabisa kinachozidi kung'arisha na kufurahisha watu ni sauti aliyonayo ya kuimbia. Sauti yake ni nzuri sana, aimbapo na kama ni mpenzi wa muziki lazima tu utatega sikio na utahisi namna sauti yake inavyopenya. Wakati anaachia wimbo huu kwa upande mwingine ingekuwa ni vigumu sana kwa yeye kujulikana na kusikika katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Lakini wapi bado kwa kipindi hiki ndipo alipowika zaidi japokuwa kulikuwa na gonjwa ambalo lilitikisa dunia nzima na kusababisha madhara makubwa katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ugonjwa huo ulijulikana kama Ugonjwa wa homa ya Mapafu ya mwaka 2019 (Corona Virus Disease of 2019 (COVID 19). Kwa hali ilivyokuwa hakika ingekuwa ni vigumu sana kwa ZUCHU kuweza kusikika sana ndani ya nchi na nje ya taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata na nje ya bara la Afrika. Hii ilidhihirisha kabisa kuwa ZUCHU amesainiwa katika moja ya lebo kubwa duniani kimziki. Hii yote ni pamoja na nguvu kubwa kutoka kwa mkurugenzi wa WCB Diamond Platinumz kufanya jitihada mbalimbali katika kutaka msanii wake mpya aweze kujulikana katika dunia. Kusainiwa kwa ZUCHU katika lebo kubwa ya muziki barani Afrika (WCB) hakutaka kulega kamwe bali alizidi kupambania jina lake kwa usiku na mchana azidi kung'ara. Akiamini kuwa kuwepo tu katika lebo kubwa si kwamba ndiyo utajulikana bali zinahitajika na jitihada zako za juu zaidi. Tukio kubwa ambalo alilifanya kabisa na halikuwa limezoeleka kwa wasanii mbalimbali kutoka Tanzania ni uzinduzi wa EP yake ambayo ilikuwa na nyimbo saba. Nyimbo hizo ni; 1. HAKUNA KULALA 2. NISAMEHE 3. KWARU 4. WANA 5. RAHA 6. ASHUA 7. MAUZAUZA Uzinduzi huu ulifanyika mubashara kupitia Wasafi TV na lilikuwa ni tukio ambalo liliangaliwa na watu wengi sana. Pia, tukio hili lilioneshwa katika mtandao wa kijamii wa YouTube katika akaunti ya Wasafi Media. Waliowasili katika uzinduzi huu walikuwa ni watu wachache sana, kwa ujumla ulikuwa ni uongozi wa WCB, mama yake (Khadija Kopa) naye alikuwepo pamoja na wadau wengine. Hii ni kutokana na tangazo ambalo lilitolewa na nchi la kutokufanya shughuli ambazo zitakuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu ya mwaka 2019 (COVID 19) ulioweza kutikisa dunia. Uzinduzi huu ulienda vizuri sana na ZUCHU akiwa ametumbuiza kwa ufasaha kabisa kama msanii aliyezoea jukwaa na kamera. Nyimbo zake hizi zote zinapatika kupitia akaunti yake ya YouTube iitwayo ZUCHU iliyofunguliwa tarehe 19/01/2019. Baada ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) kuisha uongozi wa WCB chini ya Diamond Platinumz uliweza kumuandalia tukio kubwa sana ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City ambapo lilifanyika tarehe 18/July/2020. Tukio hili lilijulikana kwa jina la I AM ZUCHU ambalo lilihusisha uzinduzi wa EP ya ZUCHU likiwa limehudhuriwa na mashabiki mbalimbali akiwemo mkurugenzi wa lebo ya WCB pamoja na watu wengine maarufu, mojawapo ni Bibie Ritha ambaye huwa ni msimamizi wa tamasha la mashindano ya vipaji liitwalo Bongo Star Search (BSS). Katika mahojiano yaliyofanyika kati ya Bibie Ritha na mwandishi wa habari bibie Aaliya katika ukumbi wa Mlimani city wakati wa tukio la I AM ZUCHU katika zulia jekundu (red carpet) kupitia channel ya Wasafi TV ilikuwa mubashara, Ritha alimuongelea haya ZUCHU; "Asivunjike moyo hii safari ni ndefu, lakini kwa kuangalia alivyokuwa mvumilivu, amekaa muda mrefu kutoka, hakuwa na papara. Aendelee kuwa na that kind of strength (nguvu ya namna hii). Inabidi ajue anataka kufanya nini? kuwa nani? malengo yake ni yeye pekee yake anaweza kuyasimamia". Tafsiri hapo juu ni yangu. Tukio hili lilifanyika vizuri sana na hata watu hawakuwa wanaamini kama tukio hili lingejaza watu hivi, lakini kwa siku ile kwa kweli ni siku ambayo ilidhihirisha kuwa ZUCHU ana mashabiki wengi japokuwa ni muda mfupi sana tangu aingie katika muziki. Katika ukumbi huo paliandaliwa sanamu la ZUCHU ambalo kweli lilifanana nae sana. Tukio hili lilikuwa ni la kipekee sana. Kiingilio cha juu sana katika tukio hili kilikuwa ni shilingi milioni mbili na cha chini kilikuwa ni shilingi elfu hamsini. Kuzidi kuona kuwa ZUCHU kila siku anazidi kukua kisanii ni baada ya jina lake kutokea katika kinyang'anyiro cha tuzo za Africa Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020. Aliwekwa katika vinyang'anyiro viwili ambavyo ni; (i) Best Female Artist in East Afrika (Msanii Bora wa kike Afrika Mashariki) (ii) Best Newcomer (msanii chipukizi bora) Tafsiri katika vinyang'anyiro tajwa hapo juu ni yangu. Kategori tajwa hapo juu ni kutoka katika tovuti ya https://afrimma.com/afrimma-2020-nominees/ Septemba, 2020 ZUCHU alizidi kupata mawanda ya juu zaidi, hii ni baada kuwekwa katika tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) katika kinyang'anyiro kimoja cha; (I)Best New Artist (Msanii Chipukizi bora) Hii ni furaha na heshima kubwa sana kwa msanii huyu kwa uwezekano wa jina lake kujitokeza katika vinyang'anyiro hivyo ambavyo ni vikubwa kwa tuzo zitolewazo hapo. Pia, ni heshima kubwa sana kwa lebo ya Wasafi kuwa inalea wasanii mahiri katika muziki. ZUCHU, jina lake likazidi kung'ara, Oktoba, 2020 jina la ZUCHU liliwekwa katika orodha ya tuzo kubwa duniani ambayo ni GRAMMY. Aliwekwa katika kinyang'anyiro kimoja ambacho ni; (i) THE BEST NEW ARTIST (MSANII MPYA BORA) Tafsiri hapo juu ni yangu.
Si jambo la kimzaha kwa msanii mdogo kama huyu tena kutoka Afrika-Tanzania kuwekwa katika orodha hiyo. Hii ilimaanisha kuwa kazi zake zimekubalika. Kwa sababu katika tuzo za GRAMMY kabla jina la msanii halijawekwa katika orodha na kutangazwa kabisa katika mitandao mbalimbali ni lazima msanii atume nyimbo zake na kisha zitapitiwa kwa umakini. Kama imekubalika au zimekubalika ndipo zitawekwa katika vinyang'anyiro husika. Kwa hiyo, ZUCHU amejitahidi sana hadi nyimbo zake kusikilizwa katika idara hizo ndipo jina lake likawekwa katika orodha ya watakaowania. Tarehe ya 15/09/2020 ZUCHU aliachia wimbo ulioitwa CHECHE akiwa amemshirikisha Diamond Platinumz. Mapokezi yalikuwa ni makubwa sana kupitia akaunti yake ya YouTube iliyosajiliwa kwa jina la ZUCHU ambapo ndani ya siku moja watazamaji waliweza kufika milioni moja. Ni mapokezi makubwa sana kwa msanii mdogo kama huyu ambaye hadi muda anaachia wimbo huu bado hajafikisha hata mwaka mmoja katika muziki wa bongo fleva na machoni mwa mashabiki. Ndani ya wiki mbili wimbo huu (CHECHE) tayari ulikuwa umeshafikisha waangaliaji milioni nne kupitia akaunti yake ya YouTube. Hadi muda anatoa wimbo huu ZUCHU ndiyo kwanza ana muda wa miezi sita katika muziki na katika macho ya mashabiki wanaoufuatilia muziki ndipo walikuwa wakizidi. Tarehe ya 28/09/2020 ZUCHU aliachia wimbo wake ulioenda kwa jina la LITAWACHOMA. Wimbo huu ambao ulikuwa ni picha jongeo (Video) alimshirikisha msanii Diamond Platinumz. Kuachiwa kwa video hii hakika kulikuwa na mapokezi makubwa sana katika akaunti yake ya YouTube iliyosajiliwa kwa jina la ZUCHU. Hapa ndipo palipohakikisha kuwa ZUCHU kila anapotoa wimbo ndipo anazidi kuimarika na kuonekana umahiri wake katika muziki. Ndani ya siku moja tayari wimbo huu (LITAWACHOMA) ulikuwa umeshafikisha watazamaji milioni moja kupitia akaunti yake ya YouTube. Jina la ZUCHU lilizidi kuvuma zaidi kimataifa kama ngoma ya usiku isikikavyo, hii ni baada ya kutoa wimbo ambao alimshirikisha msanii kutoka Nigeria aitwaye JoeBoy. Wimbo ulienda kwa jina la NoBody ambao ulihusisha audio na picha jongeo. Wimbo huu aliuweka katika akaunti yake ya YouTube tarehe 16/10/2020. Kwa ujumla, Joeboy alikuwa akikubali sana kazi za ZUCHU. Mbali na kukubalika kwa mashabiki wa kawaida tu, hata rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MH. Dkt John Pombe Magufuli aliweza kumkubali sana kwa ufanisi wake. Hii ni baada ya ZUCHU kurekodi wimbo maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Wimbo huo ulienda kwa jina la "TANZANIA YA SASA" ambao aliutoa tarehe ya 11/Juni/2020 ukiwa ni audio tu. ZUCHU alianza kukaribishwa katika vikao mbalimbali vya CCM akiwa pamoja na uongozi wake wa WCB. Mathalani katika vikao vya upigwaji kura kwa kumpitisha mgombea wa urais 2020-2025 Daktar John Pombe Magufuli pamoja na MH. Hussein Ally Mwinyi kutoka Tanzania bara vilivyofanyika katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma. Tarehe 03/oktoba/2020 ZUCHU alitumbuiza katika viwanja vya Mnazi Mmoja visiwani Zanzibar katika kampeni za mgombea urais kupitia tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli pamoja na MH. Hussein Ally Mwinyi wakiwa ni wagombea katika kiti cha Urais kwa tiketi ya CCM. Dkt John Pombe Magufuli kutoka Tanzania Bara na MH. Hussein Ally Mwinyi kutoka Tanzania Visiwani. Kwa namna alivyotumbuiza vizuri kwa kweli Dkt John Pombe Magufuli hakusita kumpa heshima yake. Ndipo alipoamua kumvalisha kofia ya chama. Ni heshima kubwa sana MH. Dkt. John Pombe Magufuli alimpatia.
Kwa siku hiyo hata aliyekuwa rais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi dkt. Mohamed Shein aliwasili katika kampeni hizo na kushuhudia mambo makubwa yaliyofanywa na ZUCHU katika viwanja vya Mnazi Mmoja huko Zanzibar. Hadi kufikia Oktoba, 2020 ZUCHU ndiyo kwanza alikuwa na miezi sita katika harakati za muziki. Lakini, katika miezi sita hiyo hakika ana mengi makubwa sana aliyoyafanya ambayo yanaweza kupita hata kwa baadhi ya wasanii ambao wapo katika muziki kwa muda mrefu, kutokana na kutokupata njia za kutokea vizuri. Kufanya vizuri kwa ZUCHU katika muziki hakika kuliweza kuibua maneno mengi katika mitandao ya kijamii kutoka kwa watu mbalimbali. Watu wengi hawakuwa wanaamini kuwa kama ZUCHU kutoka kwake kimziki na kufanya mambo makubwa katika muziki si kwa njia ya halali bali kuna namna ambayo anaitumia hadi kufika hatua hii. Wengi walikuwa wakisema kuwa ZUCHU anatumia uganga, yaani amekuwa akienda kwa waganga ili kufanya jina lake lizidi kung'ara zaidi. Ili kujua ni kweli au si kweli juu ya mambo yaliyokuwa yakizungumzwa katika mitandao ya kijamii, tarehe 12/Oktoba/2020 mwandishi wa habari wa Wasafi TV kupitia kipindi cha Refresh kinachorushwa kila siku ya jumatatu hadi ijumaa saa 12:00 jioni aliamua kuvunja ukimya na kwenda kumfanyia mahojiano ZUCHU ili kujua ukweli zaidi juu ya maneno yaliyokuwa yakiendelea. ZUCHU alisema; "Mganga wangu ni Mwenyezi mungu, wallah tena sometimes (muda mwingine) napitiliza hata kusali Mwenyezi Mungu anisamehe. Lakini kiukweli kikubwa mimi nina hofu sana ya Mwenyezi Mungu, nakuwa natia uwoga kwenye kila project (kazi) yangu lazima niwe, lazima nitangulize dua kwanza. Hakuna kikubwa ntadanganya kama nikisema nishawahi kwenda kwa mganga hata hapa ninapokaa sipajui". Mwandishi wa habari yule alipomuuliza kuwa kwa nini walimwengu wanakuchulia hivyo? Hapa ZUCHU alisema hivi; "Labda hawakuwa wanategemea kama ilivyo mimi tu. Mapokezi yamekuwa makubwa sana. Kwa hiyo, kitu chochote chenye mshindo huwa kinashtua watu. Kwa hiyo, yeah (ndiyo) nadhani hicho tu. Kikubwa kiukweli hard working (kufanya kazi kwa bidii). Siwezikupoa, nataka niende na speed (kasi) hii hii". Katika mahojiano hayo ZUCHU alisema; " Sasa hivi ndiyo kwanza naanza. Kwa sababu miezi sita bado hujafanya chochote kwenye game musically (Kimziki). Huwezi ukafanya vitu vingi ndani ya miezi sita. Kwa hiyo, nina vitu vingi sana vya kurelease (toa/achia)" Tafsiri zilizofanyika katika mahojiano hayo ni za mchambuzi. Hii inadhihirisha kabisa kuwa ZUCHU anajitambua zaidi katika muziki wake. Hajalewa na jina lake, hajalewa na mama yake kuwa msanii wala hajalewa kuwepo katika lebo kubwa ya muziki barani Afrika ambayo ni Wasafi Classic Baby (WCB Wasafi). Jitihada zake ndizo zinazomfanya azidi kung'ara kupitia WCB. ZUCHU akazidi kupendwa na kupendeka na mashabiki zake kutokana na kazi anavyozifanya vizuri. Kupitia kipindi kiitwacho "Hivi Ni Kweli?" Kirushwacho kupitia Wasafi TV na muongozaji mkuu akiwa ni mwandishi Mo Town Sanya. Katika kipindi hichi mwandishi huyu hukifanyia mtaani kwa kumchukua msanii na kufanya mahojiano na mashabiki huku wakimuongelea msanii husika. Ikiwa ni 21/Oktoba/2020 Mo Town Sanya katika kipindi hiki kwa siku hiyo alikuwa na ZUCHU. Kipindi hiki kilichukuliwa katika maeneo ya Mbagala. Mapokezi yalikuwa ni makubwa sana kushinda ilivyo hata vipindi vingine vilivyopita vya "Hivi Ni Kweli?" Akina mama, baba na vijana walikifurahia sana kipindi hicho. Kwa siku hiyo watu walijaa sana katika mahojiano hayo na kila mtu akitaka kumuona ZUCHU. Watu walijaa sana barabarani mithili ya kusema kwamba kuna tamasha linatakiwa kufanyika. Watu wengi walikuwa na bashasha ya kutaka kuhojiwa juu ya ZUCHU na walipatiwa nafasi. Hadi wengine walikuja wenyewe bila kufuatwa na mwandishi kama ilivyo vipindi vingine. Hii ilionesha dhahiri namna ZUCHU anavyopendwa na mashabiki zake na yote hii ni kutokana na kazi nzuri anazozifanya katika muziki wake. Tarehe 02/Novemba/2020 ZUCHU aliachia audio iliyoenda kwa jina la SHANGILIA. Wimbo huu alikuwa akimpa hongera za ushindi kwa MH. Hussein Mwinyi kwa kushinda katika kinyang'anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM na kuzidi kukisifia zaidi chama hicho tawala. Tarehe 22/11/2020 ZUCHU aliachia wimbo ambao ulikuwa ni audio ulienda kwa jina la HASARA. Ni wimbo ambao kwa kweli ndani yake unaleta hisia fulani pindi uusikilizapo kwa umakini. Kimataifa ZUCHU akazidi kutanua mabawa yake, majukwaa mbalimbali ya kisanaa yakamtambua kwa kuangalia kazi zake anavyozifanya vizuri. Hii ilidhihirisha dhahiri baada ya ZUCHU kushinda tuzo ya AFRIMMA ikiwa ni tarehe 16/11/2020 katika kinyaang'anyiro cha Msanii chipukizi Bora (Best New comer Artist).
Hii ilidhihirisha kabisa kuwa ZUCHU kazi zake zimesambaa katika kukubalika. Ni tukio la furaha sana kwa msanii chipukizi kama huyu kushinda tuzo kubwa kama hizi ikiwa ndiyo ana miezi saba tu katika tasnia ya muziki. Jina la ZUCHU likazidi kung'aa katika mawazo ya wafanyabiashara. Hii ni baada ya ZUCHU kupatiwa nafasi ya kuwa balozi wa kampuni linalojishughulisha na uuzaji wa nywele (DARLING). Hii ni alama kubwa sana kwa msanii mdogo kama huyu kupata nafasi kubwa kama hii ya kuaminika na wafanyabiashara kuwa kwa kumuweka ZUCHU kuwa balozi wao atawasaidia katika biashara yao. Hii inaonesha dhahiri kuwa ZUCHU mizizi yake hadi sasa imeshazidi kukomaa.
Utambulisho huu ulifanyika tarehe 19/11/2020 katika ukumbi wa HYATT REGENCY jijini Dar- Es-Salaam ambapo katika tukio hili waandishi wa habari mbalimbali waliwasili kwa wingi sana. Hadi kufikia tarehe 24/11/2020 tayari ZUCHU alikuwa ameshafikisha miezi nane kuwa katika muziki. Lakini kwa miezi michache hii ni makubwa sana ameweza kuyafanya katika muziki. ZUCHU ameweza kuthibitisha kuwa kuna wanawake wakiwezeshwa wanaweza. Hakika anaweza kama nyendo hizi alizonazo akaziendeleza na kuzidi kuziimarisha. ZIFUATAZO NI NYIMBO ZA ZUCHU AUDIO NA PICHA JONGEO (VIDEO) HADI LEO AMBAZO ZIPO KATIKA AKAUNTI YAKE YA YouTube. Nyimbo hizo ni kama zifuatazo; 1. WANA-09/April/2020 2. KWARU- 14/April/2020 3. HAKUNA KULALA-20/April/2020 4. RAHA- 04/May/2020 5. NISAMEHE-17/May/2020 6. CHEHE- 15/09/2020 7. LITAWACHOMA- 28/09/2020 8. MAUZAUZA-14/July/2020 9. NoBody-16/0ktoba/2020 10. HASARA (AUDIO) 22/11/2020 11. SHANGILIA (AUDIO)- 02/Novemba/2020 NYIMBO AMBAZO ZUCHU AMEWASHIRIKISHA WASANII 1. CHECHE. Hapa alimshirikia Diamond Platinumz akiwa ni mkurugenzi wa WCB. 2. LITAWACHOMA. hapa alimshirikisha Diamond Platinumz 3. ASHUA- alimshirikisha Mboso kutoka lebo ya Wasafi 4. MAUZAUZA- alimshirikisha Khadija Kopa. 5. NoBody-alimshirikisha Joeboy kutoka Nigeria. 2.2 MUSTAKABALI WA ZUCHU BAADA YA MIAKA MITANO IJAYO Kabla ya kuzungumzia mustakabali wa ZUCHU katika muziki wake ni vyema zaidi kujua nini maana ya mustakabali. Mustakabali; ni matukio au hali ambayo itaweza kujitokeza kwa siku za badae au mbeleni. (http://bestdict.mobi/) Katika muziki panahitajika heshima na ustadi ili kuzidi kuwika katika masikio ya watu. Kutokana na ustadi na heshima kubwa aliyonayo ZUCHU katika kazi yake hakika ni moja ya vitu ambavyo vinamfanya azidi kung'ara sana. Kama ZUCHU akizidisha na kuendeleleza heshima na ustadi katika muziki wake baada ya miaka mitano ijayo atakuwa ni msanii nambari moja wa kike katika taifa la Tanzania na Afrika ambaye anafunika sana katika tasnia ya muziki wa bongo fleva na atakuwa ameandika historia kubwa sana katika maisha yake ya muziki kama wengine walivyo. Inawezekana ikawa ni zaidi. Nje ya kuwa msanii mkubwa sana wa kike nchini Afrika hata huko Ulaya na kwingineko atakuwa ameshika sana masikio ya watu juu ya muziki wake. Kutokana na lebo aliyeko, ufanisi wake na heshima yake katika muziki. 2.3 MAONI NA USHAURI (i). Heshima na uvumilivu katika muziki ni jambo la msingi sana ambalo unatakiwa kuwa nalo. Heshima katika muziki wako kuwa hii ni kazi yako, heshima kwa wafuasi wako ukijua hao ndio wateja wako. Wafuasi au mashabiki zako ndio wa kukufanya jina lako lizidi kung'ara au laa. Heshima kwa wanaokusimamia ukijua fika hao ndiyo wanaokusimamia katika kila hatua. Kumbuka unalofanya ni biashara tosha. Jambo hili hata boss wa WCB na msanii mkubwa barani Afrika na hata nje ya Afrika Diamond Platinumz aliliongelea wakati wa uzinduzi wa EP iliyofanyika 12/0April/2020. Mahojiano hayo yalikuwa mubashara kupitia channel ya Wasafi TV na YouTube yalioneshwa mubashara kupitia akaunti ya Wasafi media. Mwandishi alikuwa ni bibie Aaliyah. Diamond Platinumz alisema. Nanukuu. "Mbali ya kuwa na ukaribu na mama yake lakini ZUCHU ni kipaji chake, uvumilivu wake na nidhamu yake" Diamond Platinumz. Kwa hiyo ni jambo la msingi sana katika kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri hapo kesho. Chonde chonde usije ukalewa na sifa. (ii). Katika uimbaji au kazi yoyote ya kisanii suala zima la ufanisi wa lugha ni jambo la msingi sana. Ikumbukwe kuwa katika utungaji wa mashairi huhusisha sana ukiukwaji wa lugha. Ukiukwaji huo huhusisha utaalamu fulani ambao huhusisha matumizi mazuri ya lugha. Ni vizuri sana kuweza kutofautisha kati ya lugha ya kawaida na lugha ya kishairi. Utaalamu katika matumizi ya tafsida yanahitajika sana katika kazi zako. Ambayo yataweza kumsaidia msanii kama wewe kufanya watu watafakari juu ya unachokizungumzia na hata watu kusema ndiyo hapa tuna msanii anayefanya kazi kisanii na wafuasi wako kuzidi kukupigia makofi. Kuwa mpenzi wa kupitia kamusi za kiisimu na kamusi za kifasihi. (iii). Jiimarishe zaidi katika lugha na kuepuka kutumia sana misimu kulikoni lugha yenye ufasaha. Kwa sababu misimu ni maneno ambayo huzuka kwa kipindi fulani na kwa watu fulani na baadae hupotea. Misimu mingine huwa ya kanda tu au hata ya kitaifa ila kuwa nayo makini. Kupotea kwa misimu hiyo huweza hata kufanya wimbo husika ukiimbwa kwa wakati mwingine na msimu huo umeshapotea kukosa sana ile ladha ya kuitwa wimbo wenye lugha adhimu na unaoenda na wakati. (iv). Epuka matumizi ya ishara. Kumbuka mazungumzo ya ishara nayo yana ujumbe wa haraka sana kwa mtu anayeangalia. Ishara kama vile za uvutaji bangi, matusi na viashiria vingine vibaya. Katika watazamaji wako ukumbuke kuna watu wanaangalia picha jongeo zako lakini hawasikii. Lugha ya alama ikiwa ndiyo lugha yao ongozi. Hivyo, wanapoona hizo ishara na ndiyo lugha yao lazima wawe na namna fulani ya kuchukia nyimbo zako. (v). Jifunze sana matumizi ya mafumbo katika nyimbo. Msanii ni mtu pekee ambaye katika utunzi wa mashairi yake hupaswa kusema mambo kwa kuwafikirisha watu. Suala la mafumbo hili pia katika baadhi ya nyimbo zako ulizoziimba hakika umeyatumia tena vizuri sana na kufanya wimbo wako uwe wenye mvuto na utafakari katika vichwa vya wasikilizaji. Hivyo, endeleza vizuri mwenendo huu. (vi). Chunga sana suala zima la maadili. Ni sawa dunia kwa sasa imeandamwa na utandawazi. Suala la uvaaji limekuwa la uigaji sana kutoka tamaduni za nje. Katika picha jongeo zako jitahidi sana suala la uvaaji lisiwe katika ukiukaji wa maadili. Hii itaepusha wewe kuweka matabaka katika mashabiki. Nyimbo zako zinatakiwa ziwe ni za milele. Kila rika liangalie nyimbo zako, Kesho na keshokutwa hakika nyimbo zako zitapendwa na watu wa rika lolote. Pia, itasaidia kuondoa migogoro kati yako dhidi ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ndiyo mlezi wa wasanii. Jambo hili kwa asilimia fulani umelufanikisha vizuri. Kwa sababu tunahitaji nyimbo zako kwa kijana anayesikiliza leo akiwa na umri labda kuanzia miaka 15 na kuendelea ambaye tayari ameshajitambua hadi anakuja kufika miaka 50 na kuendelea akisikiliza nyimbo zako hakika atawahadithia wanawe kwamba wimbo huu unanikumbusha mbali sana nilipokuwa na umri wa miaka fulani hivi. (vii) Kwa sasa fanya siasa kama njia ya kukuingizia fedha na sio siasa kuifanya iwe katika maisha yako ya utendaji kazi. Hii ikimaanisha kuwa katika mashabiki ulionao wapo katika itikadi mbalimbali za vyama vya kisiasa. Hivyo, watahitaji uwaburudishe kisanii katika majukwaa ya kisiasa na sio kuwaongoza kisiasa. Kwa sababu si wote ambao ni wafuasi wako katika muziki watakuwa katika siasa. 2.4 HITIMISHO Tasnia ya muziki kwa nyakati za sasa imekuwa ni moja ya ajira kubwa sana kwa watu mbalimbali. Kupitia kipaji cha muziki msanii apatapo jina na nafasi yake ndipo inapozidi kuwa karibu kwa namna atakavyoyatengeneza mazingira vizuri na kufanya jina lake kuzidi kumuingizia kipato cha juu zaidi. Pia, muziki huenda na nyakati. Kwamba wakati fulani nyimbo za aina fulani huvuma sana kuliko hata nyingine. Japokuwa kuna wakati kabisa nyimbo hizo zilivuma na kuvuma kama mlio wa ngoma iliyotoka kupashwa kwa moto wa gogo na sio mabuwa au makaratasi. Hivyo, ukiwa ni msanii la msingi la kufanya ni kwamba ni vyema sana kujenga jina lako la kuwa ni endelevu, kesho na keshokutwa hatupajui namna palivyo. Uimbaji wako uzidi kuwa chachu si kwa miaka hii ya leo tu bali hata miaka ijayo. Upigwapo wimbo wake watu wote katika eneo husika lazima wasisimke na kuwa makini ili kusikiliza wimbo wako. MWANDISHI & MCHAMBUZI: SAID KAITA MAWASILIANO:+255783372139 Instagram: @Saidikaita7 BARUA PEPE: Saidikaita7@gmail.com Tweeter: @SaKaitahadithi Blog: Saidikaitastories.blogspot.com

Comments

  1. Habari! Ninapenda kukukaribisha katika makala hii inayozungumzia maisha ya ZUCHU hadi kuingia katika muziki katika lebo kubwa ya muziki Afrika ambayo ni WCB. Hii ni makala namba moja kutoka kwa mwandishi na mchambuzi Said kaita. Hivyo, makala namba mbili inakuja.
    KARIBU SANA.

    ReplyDelete
  2. KAZI nzuri saana inapendeza.

    ReplyDelete

Post a Comment