KIJIJI CHA UPEPO


 

KIJIJI CHA UPEPO

MWANDISHI: SAID KAITA

SIMU: +255 783 372 139      

BARUA PEPE: saidikaita7@gmail.com

 

ONESHO LA KWANZA

(Jua limewaka. Mriri anatembea hatua tatu kisha anasimama anatega masikio. Kuna kitu anakisikia kwa mbali, anatega masikio vyema. Inasikika kwa mbali sauti ya ngoma) Ngit Ngit Ngit (Sauti ya mwimbaji anayesikika inaonesha dhahiri mwimbaji huyo ana ujuzi wa uimbaji. Wanakaribia kutokea eneo alikokuwa amesimama Mriri. Anaongea pekee yake)

MRIRI:          Mbona hizi ngoma kama vile hivi si … nahisi kama kuna jambo hapa. Wanakuja… nahisi kama wanakuja na njia hii hii ninakoelekea mimi. Embu nifanye mpango nijifiche sababu huwa nasikia hizi ni kama ngoma za heshima japokuwa siujui uheshima wake. (Harakaharaka Mriri anajificha kwenye kichaka ili wasimuone. Muda si mchache wanafika karibu na alipojificha Mriri. Wanasimama huku wakiwa wanaimba na kucheza. Wanaonekana wasichana wawili wametangulizwa mbele huku wakiwa wamefungwa kaniki kifuani hadi magotini ndipo zilipoishia. Nyuso zao zikiwa zimerembwa kwa michoro fulani ya mistari ikiwa ni meupe na meusi. Shingoni wakiwa wamevaa shanga nyeupe pee. Miguuni wakiwa pekupeku mithili ya waganga wakienda kuwanga. Wanamama wamejifunga vibwebwe kuna mmoja anaimba, mwingine anapuliza filimbi na wengine wakiwa wanapiga ngoma hizo kwa furaha sana)

MUIMBAJI: (Kajifunga kilemba kikubwa kama vile malikia huku akiimba kwa madaha. Uso wake umerembwa kwa rangi tofautitofauti na rangi yake ilo nyeupe ndipo alizidi kupendeza zaidi).

                                                                                    Tafsiri

                        Vakurire vakurire,                   Wamekuwa wamekuwa,

Vakurire vana visu vakurire,   Wamekuwa wana wetu wamekuwa,

Heshima kwavo razima,          Heshima kwao lazima,

Ko reka usinga,                       Kwa kuacha utoto,

                       Hantu vodoma kwa boha,        Mahali wanapoenda pazuri,

Razima vaseke,                        Lazima wacheke,

                       Makulu kuyatanga,                   Makubwa kuyajua,

Sifa mojawavo ya iri itendo.    Sifa mojawapo ya hili tendo,

Makulu vayatangire,               Makubwa wameyajua,

                        Vikalo vikulu,                          Vikao vikubwa,

                        Vovo kufika,                            Wao kufika,

                        Mawazo kuseya,                      Mawazo kutoa,

HADHIRA:    (Wanapokelea kwa bashasha)

                         Vakurire eeee vakurire,                      Wamekuwa eee wamekuwa,

Vakurire vana visu vakurire,               Wamekuwa watoto wetu wamekuwa,

                        Vakurire eeee vakurire,                       Wamekuwa eee wamekuwa,

(Wanamama wanaendelea kuimba huku wakicheza vya uhakika kabisa bila kujali nini wala nini. Mabinti wamekaa kimya tu)

MRIRI:          (Bado kajificha. Anaanza kuongea kimoyomoyo). Mbona kama siamini ninachokiona? Yule si Chiku au…. yule ni Chiku kabisa… au kwa vile wamempaka marangi rangi ndiyo maana namfananisha? Lakini mbona wazazi wake siku za nyuma walinitaarifu kuwa Chiku anaumwa sana kwahiyo amepelekwa hospitali na hayuko hospitali za karibu ni huko mjini kabisa. Ndivyo alivyoniambia sasa hivi namuona Chiku pale. Nilikuwa nikimsubiria sana mpenzi wangu takribani kama miezi kadhaa imepita sasa nikiwa najua yuko hospitali alafu muda huu ninamuona hapa. Hapa kweli nina changu? Oooh … Chiku wangu mbona kama naona umenisaliti. Ahadi gani tulikuwa tumewekeana jamani. Heee… nataka nianze kulia hapa kumbe nimejificha hapa sinitaumbuka sasa. (Wanamama wanaendelea na msafara ndipo Mriri naye anaondoka)

 

 

ONESHO LA PILI

(Muda ni huo huo mazingira ni ya nyumbani kwa akina Mriri. Kuna vibanda vinne tu katika kaya yao. Upande wa mashariki kuna zizi la ng’ombe. Mbwa anasikika akimbwekea mbwa mwingine. Mriri amekaa na dada yake kwenye kirago wakiwa wamejiegemeza kwenye kibanda. Vibanda vyote vimeezekwa kwa nyasi. Kichiko amevaa gauni la bluu, kichwani kajifunga kitambaa cha rangi ya bluu bahari)

MRIRI:          Dada yangu… yaani huko nilikotoka… huko ni hatari… hadi nimejuta kupita njia hii ya kutoka kijiweni.

KICHIKO:     (Anaongea huku akiwa anamenya mbaazi zilizoko kwenye ungo na kuziweka kwenye safuria). Unamaanisha nini Mriri

MRIRI:          Hata sielewi nikuelezaje.

KICHIKO:   Sasa mdogo wangu ukishindwa kunieleza mimi nani tena mwingine?

MRIRI:          Kwa nini mnifiche?

KICHIKO:    Nini?

MRIRI:          Chiku…

KICHIKO:    Chiku?

MRIRI:          Ndiyo … Chiku…

KICHIKO:     Amefanayaje?

MRIRI:          Mlinidanganya Chiku anaumwa kumbe wamemkeketa. Nimekutana na msafara huko.

KICHIKO:     (Ananyamaza kwa sekunde tatu. Anaweka ungo chini na kuacha kazi ya kumenya Mbaazi).  Mdogo wangu ya zamani kuyafuta ni sawa na kuichubua rangi yako. Hata ujitahidi kuichubua rangi yako vipi uhalisia utabaki pale pale tu. Haya mambo yamekuwa yakifanywa tangu zamani. Kutoka enzi za mababu na mababu mbona ni kitu kijulikanacho tu katika kijiji cha Upepo.

MRIRI:          Unamaanisha mimi na Chiku ndiyo basi?

KICHIKO:     Mriri kumbuka mipango si matumizi. Pia Mriri hata kwa dawa mdogo wangu huwezi kumuoa Chiku.

MRIRI:          Unamaanisha nini?

KICHIKO:     Kuna siri kubwa sana mdogo wangu hapa… Istoshe kwanza sisi ni maskini hatuna uwezo wa kulipa mahari makubwa hivyo. Mwanamke kama yule katika kijiji hiki cha Upepo ana heshima na thamani kubwa.

MRIRI:          Tulipatana lakini…

KICHIKO:     Haya wewe ng’ang’ania kuwa mmeshapatana na huyo Chiku. Kweli Chiku ni msichana ambaye anajiheshimu tena kuliko hata wasichana wengine hapa kijijini. Lakini kuna vigezo mbalimbali vinaweza kukufanya kabisa usimuoe huyo Chiku.

MRIRI:          Vigezo gani?

KICHIKO:    Mama atakuja kukuelezea.

MRIRI:          Wewe ndiye unayetakiwa kunieleza vizuri kwa kuwa unaijua hii siri…

KICHIKO:    Mriri… mimi sina dhamana ya kukueleza lolote hapa… nimekugusia tu kwa kuwa umeileta hii mada hapa. Mwenye dhamana ya kukuambia yote ni mama.

MRIRI:          Unanikatisha tamaa Kichiko.

KICHIKO:     Wala… huo ndiyo ukweli.

MRIRI:          Natamani sana mama aje nilijue fumbo hili nililofumbiwa kwa mpenzi wangu.

KICHIKO:     Sawa… leo alisema atawahi kutoka kibaruani.

MRIRI:          Sijui kama atakubali kunihadithia lolote.

KICHIKO:   Atakubali tu… mimi nitatumia njia ya kumuambia.

MRIRI:          Nashukuru sana.

KICHIKO:     Sawa.

MRIRI:          (Anainuka na kuingia kwenye Kitara chake kilichoezekwa kwa nyasi. Anajilaza kwenye kitanda chake kilichotandikwa kwa ngozi ya ng’ombe)

KICHIKO:    (Anazungumza pekee yake kimyakimya). Babu… babu ndiye unajua mambo mengi kuhusu Mriri. Sasa leo uko mbali na macho yetu vipi siri hii atakuwa anaijua vizuri mama? Natamani ungekuwepo hapa mjukuu wako angeyajua mengi juu yake na hadi kuwepo hapa. Kama hukuwahi kumuambia mwanao sijui itakuwaje na wakati nimeshamuaminisha Mriri kuwa mama anajua. Uzidi kuwa mahali pema huko uliko (anaendelea kumenya Mbaazi).

(Mazingira ni ya pale pale nyumbani. Anaingia Huki ambaye ni mama Kichiko. Anaonekana amechoka sana. Kichwani amejitwisha ndoo kubwa ya maji, mgongoni amebeba furushi la mzigo. Gauni lake limejaa matope kila mahali. Kwenye mkono wa kulia amebeba galoni ya lita tano yenye maji. Anamuita Kichiko)

HUKI:            (Huku akiweka galoni chini) Kichiko…

KICHIKO:    Beee mama…

HUKI:            Embu njoo unitue mwanangu. Nakatire batuku (Nimechoka sana).

KICHIKO:     Sawa mama. Nakuja (Anainuka harakaharak). Shikamo mama.

HUKI:            Marhaba... Leo nimechoka sana.

KICHIKO:       Pole sana mama. (Anampokea galoni na kuiweka chini, anamtua ndoo na kuipeleka moja kwa moja hadi jikoni)

HUKI:            (Anaufungua mzigo aliokuwa ameubeba mgongoni na kuufungashia kwenye nguo vilevile bila kuonekana. Anaupeleka hadi jikoni. Anatoka nje na kuamua kukaa chini bila hata kujali kama kuna vumbi. Anatoa sauti ya kupumzika kutokana na uchovu alionao). Fuuuu.... mwanangu nimechoka...

KICHIKO:     (Amesimama mbele ya Mama). Inaonesha kabisa.

HUKI:            Choka ya leo imezidi.

KICHIKO:    Inaonesha kabisa.

HUKI:            Baba yenu yupo?

KICHIKO:     Baba… ametoka tangu asubuhi. Sijui kaelekea wapi…

HUKI:            Ameondoka kimyakimya tu?

KICHIKO:     Ndiyo…

HUKI:            Kwani wakati anatoka haukuwa nyumbani?

KICHIKO:    Ndiyo.

HUKI:            Ulikuwa wapi?

KICHIKO:   Nilienda kuchota maji… alikuwa amekaa pale kwenye mti (Ananyoosha mkono wake wa kulia kwenye mti wa mwembe). Alikuwa amekaa kwenye kirago. Nilivyorudi ndiyo sijamkuta hadi muda huu.

HUKI:            Chakula cha mchana amekula hapa?

KICHIKO:     Hajala…

HUKI:            Sasa kweli asubuhi yote ile tayari ameshatoka. Kwa ujumla hapo ameenda kilabuni tu… akirudi amelewa hadi hatamaniki. Ani amloha? (Nani kamloga?)

KICHIKO:     Yaani.

HUKI:            Yaani hapo itakuwa amechukua hela zote za jana nilizotoka nazo kibaruani.   

KICHIKO:     Yaani mama una kazi kubwa sana.

HUKI:            Mwanangu raha na uchungu wa ndoa siku zote ajuae ni aliyeolewa tu na wala si aliyekuwa katika uchumba… olewa au oa ndipo utajua vyote hivyo viwili vinakutokeaje.

KICHIKO:     (Anatulia kama sekunde tano na kuhema). Fuuuuuu.

HUKI:            Ndiyo hivyo mwanangu. Mwanangu Mriri yuko wapi?

KICHIKO:    Yuko ndani.

HUKI:            Anafanyaje?

KICHIKO:     Amelala.

HUKI:            Mbona mapema hivyo? Vipi kwani anaumwa?

KICHIKO:    Hapana… ila nahisi kama kuna jambo linamsumbua.

HUKI:            Jambo gani tena?

KICHIKO:     Nahisi akiamka atakuja kukueleza mwenyewe. Tumuache kwanza alale.

HUKI:            Sawa.

(Chumbani kwa Mriri, amelala usingizi mzito, ndoto inamuijia. Ndoto inaonesha kuwa yuko Mriri pamoja na Mzee wakiwa katika mazingira ya msituni. Giza la usiku wa manani kabisa. Mzee amejifunga kaniki tu. Mwili wake umeshiba na nywele zake nyeupe pee. Kwa mbali panasikika sauti ya Simba, bundi na sauti za wanyama wengine. Mzee ameshika mti mnene, kwenye mizizi ya mti ule inaonekana haina hata mchanga. Imening’inia ikiwa mikavu tu. Ila mizizi hiyo inaonekana kwa nguvu inayo. Mriri anashangaa mzee anachofanya. Ghafla hali ya hewa inabadilika kwa sekunde kama ishirini. Haraka upepo mkali unapita hadi miti inayumbayumba. Mriri anaogopa na anaamua kujishikisha kwenye mti uliokuwa pale pembeni. Mti unang’oka na hata mti wa jirani yake unang’oka, unachukuliwa na upepo na kwenda kuangukia mbali kabisa. Mriri anashangaa, anaamua kukaa karibu na mzee ili asije akapata madhara. Mzee yuko tu amesimama wala hana hata hofu na kinachoendelea kwa muda huo. Ameshikilia mti wake kwa makini.  Baada ya upepo kuisha tu sekunde chache joto linatokea na hali ya upepo mkali inapotea kabisa. Mzee anaanza kumuongelesha Mriri)

MZEE:           (Anaongea huku akimuangalia Mriri kwa umakini. Anatoa sauti nzito) Mjukuu wangu kuwa huru kwenye haya uyaonayo.

MRIRI:          Sawa babu. Ila tuko wapi hapa babu?

MZEE:          Tuko kwenye msitu wa manene. Huu msitu una maana kubwa sana kwako.

MRIRI:          Maana kubwa ukiwa unamaanisha nini babu?

MZEE:          Mengine utayajua tu nikishakuachia kazi.

MRIRI:          Sawa babu.

MZEE:          Unaona huu mti?

MRIRI:          Ndiyo nimeuona. Ndiyo nilikuwa nataka nikuulize kwamba huo mti unaenda kuupanda wapi angali hapa tayari kuna miti mikubwa hivyo?

MZEE:          Ahaa… sawa… ni swali zuri sana umeniuliza. Kwanza umejua huo upepo mkali uliopita hapa umetokea wapi?

MRIRI:          (Anafikiria kwa sekunde chache labda anaweza kupata majibu. Anaona hamna majibu. Anatingisha kichwa na kusema). Kwa kweli sijui umetokea wapi.

MZEE:           Sawa… unajua hii miti imeenda wapi?

MRIRI:         Siimeangukia huko mbali.

MZEE:          Sawa… sipendi kumtafunia mwanafunzi wangu majibu. Maswali niliyokuuliza ukashindwa kuyajibu. Kazi nitakuachia kwa ajili ya kwenda kufikiria.

MRIRI:          Nitaanzia wapi?

MZEE:           Utaanzia tutakapomalizia shughuli mimi na wewe.

MRIRI:         Kuna shughuli gani?

MZEE:          Ahaaa ahsante umejaaliwa maswali yenye mtiririko na yanaleta furaha na hamu ya mimi kukuachia kazi ya kwenda kufikiria nyumbani.

MRIRI:          Sawa babu.

MZEE:          Sasa unaona hiyo sehemu ambayo miti imeng’oka? (Ananyoosha kidole sehemu yenye shimo)

MRIRI:          Ndiyo… nimepaona.

MZEE:           Sawa… huu mti tunatakiwa tukaupandikize pale.

MRIRI:          Sasa mbona unaupanda huku katikakati ya msitu kabisa?

MZEE:          Ulitaka tuupande wapi?

MRIRI:          Kule pembeni kabisa.

MZEE:          Ondoa shaka. Huu mti hapa ni mdogo sana unavyouona… ila leoleo utakuwa na utazidi hata miti yote iliyopo katika huu msitu na miti yote itakuwa inauabudu huu mti na kuwa kama kiongozi wao mkuu na hatotokea kiongozi mwingine katika huu msitu kama huyu. Mti huu utakuwa umefungwa na ndugu na majirani kesho na keshokutwa tayari huu mti utakuwa ni mkubwa sana. Huu ndiyo muunganiko wa miti yote… kila kitu utajionea. Mti huo ndiyo utakuwa mshindi wa miti yote ambayo ilikuwa mibovu hapa na ndiyo utakaoleta Amani kubwa hapa. Harufu mbaya ambayo ipo katika hii miti lakini mti huu utaitoa harufu hiyo mbaya na kufanya kuwe na harufu nzuri.

MRIRI:          Sawa babu. Tukaupande huo mti.

MZEE:            Sawa. (Wanaelekea kwenye hilo shimo. Upepo uliopita pale uliacha alama kubwa kabisa katika sehemu hiyo). Sasa huu mti tunaupanda hapa. Tukishamaliza tu kufukia mizizi yake tutasimama kwa muda kidogo huku tukiwa tumerudi nyuma kama hatua tatu hivi na tufunge macho.

MRIRI:          Sawa.

MZEE:          Simama hapo tulia niupande huu mti. (Mriri anasimama hapo na kuzidi kuangalia nini kinaendelea pale. Mzee anaupanda ule mti na kuufukia). Tayari tumeshamaliza kazi.

MRIRI:          Sawa babu.

MZEE:           Haya tufumbe macho kama tulivyoahidiana.

MRIRI:         Sawa babu.

WOTE:           (Wanasimama wote kwa dakika tatu huku wakiwa wamefumba macho. Yanayoendelea pale kwa muda huo ni mazito sana. Kuna moto mkali unawaka katika eneo hilo na moto unasambaa msitu mzima. Ilipobaki dakika moja moto unazimika na hali ya mwanzoni inajirudia. Ule mti unaonekana unazidi kupanda juu na kuwa mnene zaidi na kwa shimo la pembeni mbegu ya mti ikaangukia pale na mbegu ile inaanza kuota na kukua. Dakika zinaisha wanaanza kufungua macho. Wanafungua macho Mriri anakutana na mti kwa mbele. Haamini anachokiona mbele yake. Mriri anamuuliza Mzee).

MRIRI:          Mbona hii miti imekuwa haraka hivyo?

MZEE:           Ndiyo imekuwa.

MRIRI:          Mbona hilo shimo lingine hatukuwa tumepanda mti?

MZEE:          Mbegu imeangukia hapo.

MRIRI:          Embu nielezee basi hata kwa uchache.

MZEE:           Mimi ninarudi kwetu.

MRIRI:          Wapi huko?

MZEE:          Mbali sana. Kayafikirie maswali ambayo sijakujibu na hili tukio lililotokea hapa. Kwaheri. (Mzee anapotoa pale pale na ghafla mwanga unatokea mkali na giza linafuatia)

MRIRI:          Babuuu. (Mriri anavurumbuka kutoka kwenye ndoto ile na kukaa kitandani huku akiwa anahema kwelikweli). Hii ndoto ina maana gani? Kila swali nililomuuliza hajanijibu na kuamua kuaniachia mimi nikahangaishe bongo langu. Mbona sielewi kabisa yaani… eeee Mungu wangu embu niletee basi hata ufumbuzi wa ndoto hii. (Ananyamaza kwa sekunde chache) … hapana simuelezi yeyote. Tuseme nimueleze mama? Nimueleze dada? au baba? Laaa embu kwanza niitafakari mwenyewe ndipo nitajaribu kwenda kumueleza mama au dada. Embu nirudie kulala labda ndoto ya kunifafanuliwa inaweza ikaja. (Anajirusha kitandani analala bila hata kujifunika shuka. Miguu kaining’iniza chini. Anahema kama ng’ombe). Fuuu…

(Mandhari ya nyumbani. Kuna sauti za ng’ombe zinasikika wakiwa wanaingizwa kwenye zizi lao.  Sauti ya Huki inasikika akiwa nje anamuita Mriri)

HUKI:            Mriri (Amesimama mlangoni amejishika kiuno)

MRIRI:          (Anaitika kwa kukurupuka). Nhaam mama…

HUKI:            Embu inuka.

MRIRI:          Sawa mama … haya nainuka mama.

HUKI:            Sawa… uinuke moja kwa moja. Naijua tabia yako.

MRIRI:          Naamka mama.

HUKI:            Nakusubiri hapa nje. (Anaamua kukaa kwenye kirago).

MRIRI:           (Anatoka huku akipikichapikicha macho na kuangalia mazingira ya nje. Anamsalimia mama). Mama shikamoo…

HUKI:            Marhaba Mriri. Vipi mbona umelala muda mrefu sana… ulikuwa unaumwa?

MRIRI:           (Anakaa kwenye kigoda). Hapana mama… sikuwa naumwa.

HUKI:            Shida nini kama huumwi?

MRIRI:           (Ananyamaza huku akiwa anaangalia chini na kujikuna kichwa).

HUKI:            Mbona unanyamaza mwanangu? Embu nieleze nini kimekusibu leo? Kwasababu leo hata haikuwa zamu yako ya kuchunga lakini umechoka kama mtu ambaye alienda machungajini kabisa. Kuwa huru mwanangu. Embu toa yaliyoko moyoni mwako. Sipendi usononeke kabisa.

MRIRI:          (Anajikaza na kuanza kutoa ya moyoni) Mama … natumai mimi nilishawahi kuongea na wewe kuhusu Chiku.

HUKI:            (Anashtuka kidogo) ndiyo… ulishawahi.

MRIRI:          Ahaaa … sawa… Mada niliyokuwa nikimuongelea unaikumbuka?

HUKI:            Ndiyo.

MRIRI:         Sawa. Nilikutaarifu kuwa mimi na Chiku ni wachumba. Lakini kwa siku ya leo kwa kweli nilichokutana nacho huko njiani nilipokuwa natoka matembezi yangu sikuamini nilichokiona. Niliamua kujificha kwanza ili hata watu hao wasinione kabisa. Nimemuona Chiku akiwa amefungwa kaniki walikuwa wawili huku watu wakiwa wanawacheza. Nilipoona vile nilikuja kumuelezea Kichiko lakini hakutaka kuongolea lolote zaidi ya kusema wewe ndiyo unajua yote juu ya suala hili. Unanificha nini mama?

HUKI:            (Anatafuta namna ya kumjibu). Mriri… sijui nianzie wapi na niishie wapi…

MRIRI:          Anzia hapo hapo mama. Ninatamani sana kuujua ukweli kuhusu mimi na Chiku. Ni vyema sana ukanieleza kabisa kwa undani. Yaani nakuomba sana tena sana nakuomba mama.

HUKI:            Unajua Mriri siku zote moyo hutamani sana kutimiza lengo ambalo moyo umelitamani bila hata kujali kama kutakuwa na vikwazo vyovyote. Niseme tu kwa kunyoosha maneno ni kwamba … Mriri ni kweli ulishawahi kunieleza kuhusu uhusiano wako na Chiku lakini Kichiko kakuambia huwezi kumuoa au siyo?

MRIRI:          Ndiyo.

HUKI:            Mriri jambo hili nitakalokueleza hapa natumai sikuwahi kukuelezea hata siku moja. Kwahiyo nitakapokuelezea usitishike sana bali ni ukweli wa kujua kuwa wewe utaweza kumuoa Chiku au laa.

MRIRI:          Sawa mama nakusikiliza … ndiyo maana nimeamua kukueleza suala hili nikijua kuwa wewe lazima unielezee kwa undani zaidi juu ya suala hili. (Sauti ya Nkorio inasikika)  

HUKI:            Nitakuelezea kesho juu ya suala hili. Baba yako huyo anaingia. Anaonekana amelewa chakari.

MRIRI:          Sawa mama.

WOTE:           (Wanainuka na kila mtu kuelekea kwake. Mama anaelekea chumbani kwake na Mriri anaelekea kwenye kitara chake.  Giza limeshaanza kuingia kabisa. Nkorio anaimba akiwa nyuma ya boma ya ng’ombe).

   Mengi nimejionea, Mengi nimejionea,

                                                  Ujanani sikuyafanya, mengi nilijionea,

         Leo niko uzeeeni, ya ujanani kuyafanya,

        Kweli nimechelewa, kweli nimechelewa,

 Kuvuka hatua, si jambo jema kabisa,

(Anaangalia kwenye zizi kama kuna usalama. Anaangalia na kuondoka kisha anaelekea hadi jikoni)

NKORIO:      Wewe Kichiko wewe?

KICHIKO:     Beee baba. (Anatoka jikoni kisha anasimama mlangoni na kumsalimia baba).  Shikamo baba.

NKORIO:      Marhaba binti yangu. Huko jikoni pana jambo au ndiyo tu?

KICHIKO:     Unamaanisha nini baba?

NKORIO:      (Anayumbayumba). Huko jikoni kuna chakula?

KICHIKO:    Ndiyo kipo.

NKORIO:      Mama yuko wapi? Hajarudi hadi muda huu?

KICHIKO:    Amesharudi…

NKORIO:     Yuko wapi?

KICHIKO:     Yuko ndani.

NKORIO:      Yaani wewe Huki ukae ndani wakati mimi nimekuja hapa. Ni adabu gani kabisa hiyo? Tangia asubuhi hatujaonana hapa hadi muda huu unasikia sauti yangu lakini bado unaamua kujifungia huko ndani kama mwari. Hivi huyu mama yako ana nini?

KICHIKO:    (Ananyamaza).

HUKI:            (Anatoka chumbani kwake. Anasimama na kusema hivi). Hivi Mume wangu kwa nini unapenda kila siku tugombane?

NKORIO:    Wewe ndiye unayesababisha hadi tugombane.

HUKI:            Kivipi?

NKORIO:      Alafu usijifanye hunielewi hapa. Maswala ya kuulizana maswali kama mahakama ya watu wa kuzimu. Mimi ni mume wako nikiongea kitu embu jaribu kunyamaza kimya tena kimya kweli. Nitakupiga kibao sasa hivi.

HUKI:            (Anakwepa). Hivi mume wangu huwezi hata kunionea huruma tu. Tangu asubuhi nilikuwa huko vibaruani na nimechoka kwelikweli na hata kama nimechoka hivi hela zenyewe wewe ndiye unayechukua na kwenda kulewea tu huko na kuwalewesha marafiki zako tu huku hata hujui hizi pesa zimepatikanaje. (Ananyoosha kidole).

NKORIO:      Weee… yaani unathubutu kuniita mimi mwizi kabisa? Yaani mimi mume wako kabisa alafu unanivisha jina lingine kabisa? Hivi wewe mwanamke mimi nahisi hata aliyekulaani ameshakufa. Yaani huna adabu kabisa…Yaani mimi niache kwenda kunywa pombe sababu kuwa hela ni zako. Wewe ndiyo mke wangu una wajibu wa kunihudumia.

HUKI:            Mwanaume wewe…

NKORIO:      Nini?

HUKI:            Yaani mwanaume unachukua hela na kwenda kulewea na marafiki zako ambao ni marafiki wa unafiki tu.

NKORIO:      Embu niache mimi nikalale kwanza.  (Anaamua kuelekea kulala)

HUKI:            Sawa… ila ukweli unauma. 

(Mriri anaonekana yuko anaota moto huku akiwa katika wimbi la mawazo sana) 

 

 

ONESHO LA TATU

(Mazingira ni ya pale pale nyumbani. Sauti za ndege zinasikika kwa mbali. Mama na Mriri wamekaa kwenye vigoda wakinywa uji. Kila mtu ana bakuli la uji)

HUKI:            (Anaweka bakuli chini) Mriri...

MRIRI:          Nhaam mama.

HUKI:            Najua jana tuliishia njiani … nilitamani sana nikuhadithie jambo lililokuwa likikusokota moyoni mwako.

MRIRI:           Ni kweli mama … leo nimelala nikiwa nimejawa na mawazo sana.

HUKI:            Haina shida. Afadhali hata huyu baba yako kaondoka nitaweza kukueleza yote. Kwa sababu huwa hapendi kabisa mimi na wewe tukae hivi. Huwa anajua kabisa kuna jambo tunalipanga.

MRIRI:          Nakusikiliza mama.

HUKI:            (Anakohoa kikohozi cha kuweka sauti vizuri) Mriri…. siku zote huwa nakuambia kwamba sisi ni mang’ombe wa kuanguka muda wowote. Kwa hiyo, naweza nisikuambie hii siri alafu mwisho wa siku nikianguka leo najikuta nimeacha kovu kwako ambalo ni kubwa sana. Ila nakuomba kuna hadithi nitakuhadithia juu ya wewe kuwa hapa.

MRIRI:           Sawa… (Anakaa vizuri katika namna ya kutaka kumsikiliza kwa makini)

HUKI:            (Anaongea kwa hisia) Kipindi ukiwa na umri wa miaka miwili katika hiki kijiji cha Upepo paliwezakutokea vita kubwa sana kati ya wakulima na wafugaji. Wakulima walipenda sana mazao yao yasiliwe na mifugo ya wafugaji. Lakini wafugaji walikuwa wabishi sana… kwa hiyo walitumia mbinu zote ilimradi mifugo yao ipate majani. Ilifikia wakati kabisa wafugaji walianza kuwafunguliwa mifugo yao usiku wa manani.

MRIRI:           Eee… usiku wa manani kabisa? Mbona ni wakati mbaya kabisa huo.

HUKI:            Kwa hiyo kulikuwa na kiongozi wa wakulima na kiongozi wa wafugaji. Sasa aliyekuwa kiongozi wa wakulima alikuwa na nafasi mbili. Yaani alikuwa ni mwenyekiti wa kijiji cha Upepo na hapo hapo akiwa ni kiongozi wa wakulima. Huyu jamaa alikuwa ni mtu mwenye ushawishi sana na pia alikuwa akijitolea mhanga sana katika kuwasaidia wakulima. Kijiji cha Upepo kilineemeka sana wakati wa uongozi wa mwenyekiti huyo aliyekuwa akiitwa Majuva. Majuva alifanya kazi kote kote usiku na mchana. Basi kwa mwaka huo palivyotokea vita hivyo ilikuwa ni kipindi ambacho tayari mazao kama vile mahindi ndiyo yalikuwa yameanza kuiva. Unajua nini kilitoekea?

MRIRI:          Sijui mama.

HUKI:            Sasa mwanangu naona hapa jua limeshaanza kupanda kabisa. Tulia kwanza niende kibaruani alafu baadae nitakuja kumalizia hadithi yako. Sababu nikichelewa huko nitakuta watu wameshapata sehemu nyingi na watapata hela.

MRIRI:          Daaa kweli mama utakuja kumalizia?

HUKI:            Ndiyo Mriri (Anainuka na kuchukua zile bakuli na kuelekea jikoni. Anaweka vyombo vile na kutoka huku akiwa amechukua jembe lake la kibaruani ndoo ya kwenda kuchotea maji) Mwanangu mimi naenda.

MRIRI:          Sawa mama.

(Mandhari ya kilabuni. Kilabu kimeezekwa kwa majani tu. Kimechoka sana. Kwa nje panaonekana kuna Malambo makubwa ya kupikia pombe yamebandikwa hapo yanafuka moshi kama msitu uliowaka moto. Mlangoni kuna watu kumi wamelala. Walipolala kuna vumbi. Nyuso zao zimepauka na kuwa kama soli za viatu. Miguu ndiyo hatari kabisa. Wengine wamevaa viatu na wengine hawana hata nguo kabisa wamebaki na vinguo vyao vya ndani vilivyojaa kunguni. Nkorio anaonekana yuko na marafiki zake watatu. Hapo walipokaa kuna chubuku zina pombe. Kila mtu anapuliza pombe kwa furaha tu)

NKORIO:      (Amevaa sarawili. Kichwani amevaa boshori jeusi tii) Yaani leo kunyweni mtakavyotaka hadi mkate moto.

WOTE:           (Sauti zao za pombe). Hamna wa kukata moto hapa.

NKORIO:      Nyiye kunyweni bana… Jana shemeji yenu alienda kibaruani… amepiga kazi kwelikweli. Unajua ananipenda sana… akaamua kunipatia zote. Ndiyo maana nimeamua kabla hata kuku hawajaamka nikaja kuwaamsha ili tuje kumwaga radhi hapa.

CHOGO:        (Amevaa koti refu hadi chini ya magoti. Koti hilo ni muda halijala povu. Ndevu zimezunguka mdomo mzima na weusi wake aliokuwa nao ni macho tu ndiyo yanaonekana. Anacheka) Hahahaha… yaani mke wako anakupenda sana. Hadi kakupa zote hizo… wewe ni hatari sana… unajua kufinya sana…

TUNDU:        Yaani wewe Nkorio kweli mke wako ana akili sana.

NKORIO:      Kwa nini?

TUNDU:        Anaamua kukuhudumia hivi ili usijeingia kwenye himaya nyingine alafu ukaharibu familia ya pale.

CHOGO:        (Anacheka kisha anasema). Mke wako ana akili sana.

MAPANGA:   (Anaongeaa huku akilalalala. Amenyoa kipara, ameacha ndevu) Ila mnajua… hapa tunafurahi kwa hela za mtu… jasho la mtu hili limevuja.

WOTE:           (Wanaangaliana)

MAPANGA:  Yaani wewe Nkorio unaamua kuchukua kabisa pesa za mke wako. Mchana mzima jana ameshinda kibaruani… na jua lote lile. Unajua kuna muda inabidi tuwe na roho ya huruma. Naona wote… wote tunafurahia tu hili jambo. Huu ni ujinga kabisa tunaufanya. Tunawatesa sana wanawake. Wanateseka mchana tena usiku tunawawajibisha… huruma mbona hatuna?

NKORIO:      Embu niache bana… Kama mke wako hakupendi nenda kajinyonge na   kamasi huko.

MAPANGA:  Yaani mke wangu ananipenda tena sana…. Lakini siwezi nikamnyanyasa kwa vile ananipenda ndiyo nitumie hiyo nafasi na kumfanyia hivyo. Huoni ni uonevu kabisa? Yaani mimi hata nilewe vipi lakini si kumvunjia heshima mke wangu wala kumtesa. Hivi mbona Nkorio wewe ni mkubwa tu lakini huna hata ule utu kabisa.

NKORIO:   Wewe niache bana. Embu kunyweni pombe. Huyu anajifanya ananitolea povu la kijinga hapa. Embu nenda zako kama hutaki kunywa hii pombe.

MAPANGA: Yaani nyiye ni marafiki zangu lakini katika hili kwa kweli nawapinga kabisa. Kwa sababu huo ni uonevu kabisa. Mfano wewe Nkorio ndiyo ungekuwa mwanamke.

NKORIO:      Mimi siwezi kuwa mwanamke.

MAPANGA:  Ndiyo maana nimesema mfano tu.

NKORIO:      Hata kwenye mfano siwezi kuwepo.

MAPANGA: Haya kuwa mgumu kama mkate wa waisraeli. Muda mwingine huwa tunakaza bongo bure tu. Ila tukikaa na kufikiria ndipo tutajua kuwa tuna makosa au laa.

NKORIO:      Embu nenda zako bana wewe. Yaani kwanzia leo mimi siyo rafiki yako kabisa. Marafiki zangu ni hawa hapa tu. Acha tulewe.

MAPANGA: Hivi nyinyi mnaoambiwa ni marafiki yaani hata hamna wivu. Huyo rafiki yenu ana mke na watoto nyiye ndiyo hivyo tu mnazidi kufuga madevu tu hapa. Ukubwa siyo ndevu… ndevu hata mbuzi anazo… 

WOTE:           (Wanainuka na ugomvi unaanza. Wanashikana mashati. Wote wanamchangia Mapanga. Mapanga anaamua kuondoka na kuanza kuongea akiwa amewageukia huku akiendelea na mwendo). Hata kama mkinipiga ila ujumbe umefika. Mijitu mikubwa kumbe mnamiliki ndevu tu. (Anatembea huku anayumbayumba. Anaanza kuimba na barabara nzima akiifanya ni yake).

Mwanaume mjinga, Mwanaume mjinga,

Hula hela za mke wake, asubuhi na mapema,

Kilabuni aamkia, hela siyo zake,

Afanyia kufuru, kwa marafiki zake,

Wampigia makofi, furaha ya pombe.

Huo ni ujinga, huruma kuweni nayo

(Wanaonekana Mriri na Chiku wakiwa wamekaa pembezoni mwa mfereji kwenye gogo la mti)

MRIRI:          (Amevaa suruali nyeusi na shati jekundu chini amevaa masendeu). Chiku… tulianza mapenzi tangu tukiwa tumekuwa. Yaani tayari tukiwa na hisia za mapenzi kila mtu kujua hisia kuhusu mtu fulani. Tukaahidiana kweli lazima tutaoana. Japokuwa siku zote mipango si matumizi si lazima iwe hivyo ila inaweza ikawa hivyo kwa namna mipango tu ilivyo. Siku zote nilikuwa nikijua kabisa kuwa Chiku ndiyo mke wangu mtarajiwa. Lakini kwa namna nilivyojionea kwa kweli sijui kama safari yetu itaweza kukamilika. Najua mapenzi ni upofu ndiyo maana hakuna ajuae kwenye mapenzi zaidi ya yaliyopita tu.

CHIKU:       (Amevaa gauni refu jekundu, kichwani amejifunga kilemba cheusi. Kwa pembeni kuna ndoa yake ikiwa na maji). Mriri kweli najua ni zamani tumeanza safari yetu ya mapenzi. Hadi tumefikisha umri huu hatujawahi kuonesha dalili za kuachana… japokuwa kukwaruzana kwa hapa na pale hapakuwa panaepukika. Najua hadi nyumbani kwetu walikuwa wanajua kabisa uhusiano wetu wa kimapenzi na kweli ulishawahi kuwaeleza kabisa. Lakini nyuma ya pazia kuna jambo fulani litakalofanya mimi na wewe tusioane.

MRIRI:         (Anashituka kisha anasema). Embu tulia kwanza Chiku. Unasema kuna jambo litafanya tusionane?

CHIKU:         Ndiyo. Kuna siku mama yangu alinihadithia hadithi fulani hivi.

MRIRI:          Hadithi gani hiyo na ilikuwa inahusu nini?

CHIKU:          Hadithi hiyo ilikuwa na lengo la kunikanya mimi kutenda jambo fulani.

MRIRI:          Usifanye nini?

CHIKU:           Natamani nikuelezee sema ni hadithi ndefu sana. Kwa muda huu itakuwa ni vigumu sana kwa sababu nitachelewa alafu mama ataenda kugomba sana.

MRIRI:          Nakuomba unidokezee hata kidogo tu. Kwa sababu utakuwa umeniweka mahali pabaya sana kimawazo.

CHIKU:         (Anainuka na kuchukua kata yake kisha anajitwisha ndoo). Nitakuambia siku myingine. Kwa sasa hivi muda umeshaenda sana. Si vizuri mwanamke kuchelewa nyumbani.

MRIRI:          (Mriri anabaki anashangaa tu namna Chiku anavyoondoka. Mikono ameweka kichwani kama mwana aliyeachwa na mama).

(Mandhari ya nyumbani, Huki na Mriri wanaota moto)

HUKI:            (Anaongea huku akiwa anachochea moto. Moshi mkali unafuka… anakohohoa) Kohokoho… Mriri acha niendelee nilipoishia muda ule.

MRIRI:        Embu niambie mama. Sababu moyo wangu unapata maumivu juu ya jambo hili. Naomba unisimulie.

HUKI:            Sawa. Ni kwamba … Majuva alizidi kupapambania hapa katika kijiji cha Upepo. Lakini vita hiyo ilipozidi basi naye aliamua kujiunga na wakulima wenzako akiwa kama kiongozi wao. Kwa kipindi hicho tayari alikuwa na watoto wawili. Mmoja wa kiume na mwingine wa kike. Mwana wake wa kike ndiyo alikuwa wa kwanza. Kwa hiyo hata mambo yote yanatokea hayo naye alikuwa akiyaona kabisa. Vita vile vilipiganiwa kwenye mashamba ya Majuva ambapo mashamba hayo yalikuwa karibu na kaya yake iliko.

MRIRI:          Hatari!

HUKI:            Wewe sikia kilichotokea.

MRIRI:           Sawa.

HUKI:            Basi vita vile vilipamba moto na kupamba kweli. Mwenye upanga, upinde na kila aina ya silaha alichukua na kwenda kupigana. Hapakuwa na mwamuzi kabisa. Majuva naye alijitahidi sana kuwapiga wafugaji kwakuwa naye alikuwa na nguvu sana lakini wapi walimchangia na kumpiga kipigo cha mbwa aliyeingia msikitini.

MRIRI:          (Alishtuka na kuuliza). Alipona sasa?

HUKI:            (Alikuwa akiongea kwa sauti ya huzuni). Ya Mungu mengi… kwa kweli walimpiga sana na kumkatakata viungo vyake vyote kama nyama inayoandaliwa kupelekwa jikoni ndipo ikawa mwisho wa maisha yake.

MRIRI:          Sasa mke wake na watoto wake ikawaje?

HUKI:            Mke wake baada ya kuona vile alishikwa na hasira sana akaamua kuchukua panga akitaka kuingia vitani. Alipofika hapo hakumgusa mtu hata mmoja bali ni wafugaji wote walimshambulia na silaha zote hata alipokata umauti hapo hapo.

MRIRI:           Hawakuwa na huruma kabisa… sasa wanaye vipi?

HUKI:            Kwa wanaye kwa kweli yule wa kike alifariki. Kwasababu nyumba yao ilibomolewa na kuchomwa moto. Kwahiyo alifia huko huko ndani alikokimbilia.

MRIRI:          Kwa yule wa kiume ikawaje?

HUKI:            Yule alipona. Kwa sababu mama yake alimuacha jikoni. Kwahiyo kule jikoni wafugaji hawakupagusa wakiwa wanajua kuwa hapakuwa na mtu. Ndipo baada ya watu wale kuondoka ndipo wanakijiji tukaenda pale…. Mimi na Nkorio ndipo tukaingia hadi pale jikoni na kumkuta huyo mtoto pale.

MRIRI:           Kumbe alipona?

HUKI:            Ndio… alipona… yule mtoto tuliishi naye hadi leo hii.

MRIRI:           (Alishtuka na kusema).  Mbona kama sijakuelewa mama?

HUKI:            Mwanangu hii hadithi kwa ujumla ilikuwa ikikuhusu wewe. Sijawahi kukuhadithia hata siku moja. Wewe ndiye mtoto pekee wa Majuva. Mriri wewe si mwanetu tulipenda tu kukulea hapa baada ya majanga yale kutokea. Hatukuwahi kukwambia. Tumeishi na wewe kwa muda mrefu…

MRIRI:           (Hakuwa na la kuongea kabisa juu ya mada hiyo. Alikaa kimya kama dakika moja hivi. Hakuna aliyethubutu kutoa neno lolote kwa muda huo. Kichwa alikiinamisha chini kama kondoo wakiwa wamepumzika).  

     

ONESHO LA NNE

(Mandhari ya mbugani, Mriri anachunga ng’ombe. Yupo katika dimbwi la mawazo, anatokea Anatokea Salala ambaye ni mdogo wa Chiku)

SALALA:       (Akiwa ameshikilia karatasi iliyokunjwa. Anamuita). Kaka Mriri.

MRIRI:         (Anashtuka… sababu hakuwa anataraji kama Salala angetokea pale) Nhaam…

SALALA:       Shikamo kaka Mriri.

MRIRI:          Marhaba… hujambo?

SALALA:       Mimi sijambo. Mbona unaonekana una mawazo sana?

MRIRI:           (Anatabasamu) Hapana mdogo wangu. Sina mawazo ya kivile ni ya kawaida tu.

SALALA:      Hapana… hiyo siyo kawaida…

MRIRI:          Ndiyo ukweli…

SALALA:      Kwamba una mawazo sana.

MRIRI:          Hapana… yaani kawaida tu ya mwanadamu kuwa na mawazo.

SALALA:      Hapana… kwa wewe imezidi.

MRIRI:          Umejuaje?

SALALA:      Namna nilivyokukuta tu hapa.

MRIRI:          Ni mambo ya kawaida tu.

SALALA:      Sitokaa… kuna mzigo tu dada kanipa nikuletee. (Anampa ile karatasi) Haya kwaheri.

MRIRI:          (Anaipokea karatasi na kuifunua, anaanza kuisoma)

 

 

 

Kwako mpenzi (Mriri),

Natumai u bukheri wa afya. Mpenzi kwangu kuwa bukheri ni hadi nitakapojua wewe hali yako ikoje. Bado ninakukumbuka na kukuheshimu uliyeniingiza ukubwani.

Tumekuwa muda mrefu mimi na wewe katika ulimwengu wa mahaba, ulimwengu ambao ulikuwa na milima na mabonde japokuwa tulipendana kwa dhati, vizuri na vitamu tulipeana. Tulipanga mengi sana ni vipi tutaishi na mengi zaidi. Lakini wahenga walinena hakuna marefu yasiyokuwa na ncha na mbio za sakafuni huishia ukutani ndipo nilipofikia kuamini kuwa mipango siyo matumizi.

Mpenzi, ninapenda kukutaarifu jambo hili kwa sikitiko la hali ya juu kuwa, penzi letu tulilokuwa nalo muda mrefu halipo tena, jambo hili liko nje ya uwezo wangu. Ni muda umeisha naamini utakuwa umeambiwa mimi siyo kabila lenu. Kwa maana hiyo itakuwa ni vigumu wewe kunioa mimi. Mpenzi wangu ulonihudumia kihisia kwa muda mrefu nakuomba usihuzunike sana kwa hili, japokuwa naamini ni vigumu sana kuvumilia. Vitamu ulivyonipa bado ninavikumbuka, utashangaa sana kwa nini hata kwenye arusi hukutaarifiwa ni kwa sababu arusi ilifanyika kisirisiri tu na mtu ambaye alitokea huko mbali kwa kuwa ni tajiri baba alimkubali. Arusi ilifanyika usiku wa manani mithili ya watu wakiwanga. Mriri nitakukumbuka, milele sitokusahau. Ili kupata siku lazima pakuche na pakuchwe, basi mikono yetu itakutana Mungu akipenda kutukutanisha. Mriri… mimi naamini wewe ndiyo msuluhishi wa haya madhila yanayojitokeza katika jamii hii. Ukishinda yawezekana mikono yetu ikawa rahisi kushikana.

Usitoe machozi ungali u hai natumai udongo utajashikana na pengo litafutika.

Wasalamu,

Chiku aliyekupenda milele.

25.05.2001

 

 

(Anamaliza kuisoma barua ile na kuanza kumuangalia Salala. Anasahau kama Salala alimuaga alipompatia barua. Anawafuata ng’ombe wake. Kidogo wamesogea kutoka pale alipokuwa nao kisha wanazidi kusogea kwenye eneo lingine. Anaongea pekee yake)

MRIRI:          Kijiji cha Upepo haya ni mambo gani kabisa inashikilia? Kwa sababu ni tamaduni ambazo zimepitwa na wakati kabisa. Yaani watu tunapendana hivyo alafu kwa sababu ya ukabila tu inatutenganisha kabisa. Hiki Kijiji kinahitajika kufundishwa kabisa juu ya haya mambo. Ila Chiku lazima nimuoe tu hata kama huyo jamaa ameshamchukua. Nitahama hii sehemu…

(Mandhari ya nyumbani, Huki na Kichiko wamekaa kwenye kirago alafu Mriri amekaa kwenye kigoda)

MRIRI:          Mama… dada… nimewaiteni hapa nina jambo nataka kuwaambieni…

HUKI:            Jambo gani?

KICHIKO:     Kuna nini tena Mriri?

MRIRI:          Jamani mama baada ya kunihadithia ile hadhithi yote… kwa sasa mimi najiona mamluki kabisa katika kijiji hiki.

HUKI:            Siyo hivyo mwanangu…

MRIRI:          Mama wala usiubishe ukweli… acha mimi nirudi kwenye kijiji cha Mwanga… kijijini kwetu nikaanze kujenga huko. Siku zote mkataa kwao ni mtumwa… acha mimi nikajenge kule… ipo siku jambo hili litakuja kuisha tu.

KICHIKO:     Kwa hiyo Mriri ndiyo unataka kutukimbia hapa?

MRIRI:          Si kwamba nawakimbia…

KICHIKO:     Kwamba…

MRIRI:          Huu ndiyo uhalisia tu… sina namna… mimi naanza kujiandaa… baadae baba akirudi nitamwambia… kesho naanzisha safari ya kwenda mwanga.

HUKI:            Mwanangu nashindwa hata kusema maneno mengi… napenda kusema tu kwamba ufikapo huko nenda kaishi na watu vizuri… yawezekana wewe ukawa ni mshindi mkubwa sana wa kuyaondoa matatizo yote ya jamii hizi mbili.

MRIRI:          Yataisha tu.

KICHIKO:     Tunakuamini Mriri…

MRIRI:          Haya… mimi nilikuwa nawajulisha tu hilo. Tulia mimi nikapangepange vitu.

KICHIKO:     Sawa.

(Sasa Mriri amehama kutoka katika Kijiji cha Upepo na kwenda katika kijiji cha Mwanga. Nyumba yake ya miti. Kwa juu imeezekwa kwa nyasi huku ikiwa imepakwa matopematope kwa namna yake na kuficha vitu vya ndani kutoonekana. Mriri yupo na jirani yake aitwaye Tuja. Tuja amekaa kwenye kigoda amejifunika shuka ambayo inaficha hata nguo alizokuwa amevaa)

MRIRI:          Unajua Tuja hiki Kijiji cha Mwanga kinasadifu jina lake. Natamani sana tangu zamani ningekuwa naishi huku huku.

TUJA:             (Anamuangalia Mriri kwa sekunde kama mbili hivi kisha akasema). Kwa nini unaongea hivyo? Mbona mimi nimeishi hapa muda mrefu sana lakini ninaona ni mahali pa kawaida tu… au wewe unaonaje?

MRIRI:           Aaa… unajua Tuja siku zote penye miti hapana wajenzi.

TUJA:             Unamaanisha nini?

MRIRI:        Maana yake wala haihitaji mwalimu wa elimu kubwa sana. Maana yake kwanza msemo huu ulianzishwa na wahenga na hata hao wahenga wenyewe hawakuwa na elimu yoyote juu ya misemo kama hii waliyokuwa wakiijadili.

TUJA:            Naomba unipatie maana yake.

MRIRI:          Namaanisha kuwa… katika sehemu fulani panaweza kuwa na watu wenye kitu fulani na watu hao unakuta wapo tu hapo lakini wanashidwa kufanyia kazi kitu kilichopo katika sehemu hiyo. Mfano vitu tulivyojaaliwa katika bara letu ni vingi sana lakini walio nje ndiyo wanaoviona thamani yake.

TUJA:             Kivipi?

MRIRI:          Yaani tuna mali nyingi au vitu vingi lakini hatuna uwezo wa kuvifanyia kazi mwisho wa siku tunaanza kuagizia hata majirani ili kuleta mafanikio. Sasa ndiyo ukikuta watu mliowaomba hawana utu basi nao wanaamua kujifaidisha kwanza wao ndipo wawafaidishe nanyi. Hii ni shida kubwa sana iliyoko katika Bara la Dunia ya zamani. Sasa nikiunganisha na hapa kwenu ni kwamba kwa sasa watu wapo katika hiki kijiji lakini kuna wachache ndiyo wanaoelewa faida kubwa iliyopo katika kijiji chao. Ndiyo maana hata maendeleo ya kiuchumi yanakuwa namna hivyo.

TUJA:           Ahaaa… sawa nimekuelewa.

MRIRI:         Hapa Mwanga kuna neema sana. Kwa baadhi ya wananchi wanaojua kabisa ndiyo maana kwamba kuna wachache wanafaidika kupitia vitu vilivyopo katika kijiji hiki.

TUJA:           Kwa nini tangu mwanzo hukuishi hapa Mwanga?

MRIRI:          Aaa… Tuja ni historia ndefu sana. Nimeishi katika Kijiji cha Upepo kwa muda mrefu sana lakini baadae nilikuja kuonekana ni mamuluki. Baada ya mimi kujua hivyo ndiyo nikaamua kuja kwenye kijiji changu. Embu tuachane na hayo mazungumzo na tuangalie mengine. Sababu kuna baadhi ya mambo yanaumiza sana.

TUJA:           Sawa ndugu yangu. Haya nambie vipi kule shambani umeshapaandaa vizuri?

MRIRI:         Ndiyo nimeshapaandaa vizuri. Hapa yenyewe ndiyo nilikuwa na mpango wa kuanza safari ya kuelekea huko shambani. Kwa sababu kuna baadhi ya visehemu vinatakiwa kumaliziwa polepole tu si unajua harakaharaka haina Baraka.

TUJA:            Ndiyo ndiyo… natumai hadi kesho kutwa hivi tunaweza kuingia shambani na kuanza kulima.

MRIRI:         Ndiyo.

TUJA:            Basi sawa. Acha na mimi nikajiandae na yangu. Kwa sababu nilimuaga mama watoto nikamuahidi nikisharudi ndiyo tutoke wote kwenda hospitali. Kwa sababu ni mbali sana na nikiangalia hali ya mama watoto si nzuri sana. Kwa hiyo inabidi nikaandae ile baiskeli vizuri ili tuende na usafiri wa baiskeli.

MRIRI:          Sawa jirani. Msalimie shemeji.

TUJA:           Sawa. Jitahidi na wewe upate mwenza bana. Sababu kukaakaa hivi hivi tu wala si vyema. Wewe mwanaume bana…

MRIRI:          Haya bana… sawa… utani mwingine wa ukweli (Anaitikia kwa sauti ya chini)

(Tuja anainuka na kulirusha shuka lake vizuri mabegani)

 

 

ONESHO LA TANO

(Ni miaka minne imepita tangu Mriri kuhamia katika Kijiji cha Mwanga, Sasa Mriri ni Mbunge wa Wilaya ya Muungano, wanaonekana Mriri, Majuto ambaye ni diwani, Isuja ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Upepo, Kidima ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mwanga, Kidudu ni kiongozi wa wafugaji na Chapa ni kiongozi wa wakulima na viongozi watatu kutoka ngazi ya juu ya serikali. Mriri amekaa kwenye meza moja na viongozi hao wa ngazi ya juu ambao ni Bwanari, Kinara na Jafari)

MRIRI:          Habarini za muda huu ndugu wajumbe?

WOTE:           Salama kabisa…

MRIRI:          Jambo jema… aaa kabla ya yote ninapenda kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana katika kikao hiki maalumu chenye malengo chanya katika jamii hizi mbili na Muungano kwa ujumla. Lengo kuu la kikao hiki ni kujadili namna nzuri ya kuleta Amani katika vijiji viwili ambavyo ni Upepo na Mwanga. Hapa mezani kwangu niko na wasuluhishi katika ngazi za juu za serikali ambao wamekuja kwa malengo mazuri ya kuleta Amani katika jamii hizi mbili. Nimewasumbua usiku na mchana hadi waje na kuweza kulimaliza jambo hili. Labda niweze kumkaribisha kila mmoja ajitambulishe na kuongea lake kidogo juu ya mada hii. Karibu…

BWANARI:   Habarini za muda huu?

WOTE:           Salama…

BWANARI:   Aaa… kwa jina naitwa ndugu Bwanari Tafao Nkija ni afisa msuluhishi kutoka katika ngazi ya wilaya. Lengo la sisi kuwepo katika kikao hiki ni kutaka kuweka alama ya Amani katika jamii zetu… madhara ya kutoweka kwa Amani tumejionea… hatuna haja ya kuendelea na vita kila siku ambayo haina maana yoyote. Mimi yangu ni machache bali mheshimiwa mbunge hapa ndiyo mkaziaji zaidi. Ahsanteni.

MRIRI:          Ahsante sana… anayefuatia.

KINARA:      Habarini za muda huu?

WOTE:           Salama…

KINARA:      Kwa jina naitwa Kinara Rasul Butuka, nami ni afisa msuluhishi kutoka wilayani. Tumekuja hapa kwa lengo la usimamizi wa saini hizi. Sina mengi… nashukuru.

JAFARI:        Ninaitwa Jafari Mukulu, kama walivyojitambulisha maafisa wengine ndiyo wadhifa wangu. Sote tumekuja hapa tukiwa tumelenga kuleta Amani.

MRIRI:          Tunashukuru kwa utambulisho wenu. Aaa… ndugu wajumbe kikao hiki ni chachu kwa maendeleo ya wilaya ya Muungano… hapa kuna viongozi wa jamii zote mbili. Kila mmoja natumai amejionea hali halisi iliyopo kutokana utengano tuliooneshana kwa miaka mingi.  Sisi tukiwa kama viongozi… basi sisi ndiyo tunatakiwa kuwa mbele katika kutafuta namna ya kuondokana na balaa hili. Hapa tumeitana kwa ajili ya kuja kuweka jina moja la vijiji hivi ambalo litakuwa ni muungano na ishara ya Amani na upendo katika vijiji vyote. Kabla hatujafikia hatua ya kwenda kuitisha mkutano wa kuwakutanisha wananchi wa vijiji vyote hivyo lazima kwanza sisi viongozi tuwe na kauli moja yenye malengo chanya. Tuondokapo hapa kila mmoja awe amejua siku fulani litafanyika jambo fulani na litakuwa hivi na vile. Kwa ujumla hiki si kwamba ndiyo kikao cha kwanza mimi kukaa, bali ni cha kwanza kukaa na viongozi hawa kwa pamoja. Vile vile kwa ngazi za juu tumekaa sana vikao na kuweza kutengenez jina moja ambalo litaonesha umoja na mshikamano wa vijiji hivyo. Hivyo, nikiwa kama mwenyekiti wa kikao hiki ninapenda kusema kuwa jamii hizi zitaungana na kupatikana kwa jina moja liitwalo UNGA ikimaanisha Upepo na Mwanga. Haya ni mambo ambayo tulikubaliana kutoka katika ngazi ya juu. Basi kwa muda huu nipende kusikia lolote kutoka kwa wajumbe wa pande zote. Karibuni.

KIDIMA:       Mheshimiwa mbunge na mwenyekiti wa kikao hiki nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika kikao hiki. Kwanza niseme natoa pongezi kubwa sana kwa jitihada zako. Hakika ni kazi kubwa sana uliyoweza kufanya… kweli wewe ndiyo mshindi wa hili. Unastahiki kupewa sifa zote… hakika naweza kusema wewe ndiyo msuluhishi mkubwa katika hili. Kwa ujumla, mimi nipo tayari kulipokea jina hilo. Sijajua kwa wenzangu.

WOTE:           Sote tumekubaliana… umoja na mshikamano udumu.

MRIRI:          Jambo jema… bila kupoteza muda… maafisa embu toweni zile karatasi za maridhiano kila mmoja wetu aweke saini (Maafisa wanatoa karatasi na kuanza kupitisha kwa kila mjumbe)

(Ni saa kumi alaasiri. Mriri anahutubia watu katika uwanja wa Makutanoni. Amevaa tisheti ya rangi nyekundu na suruali nyeusi ya jinsi. Wananchi wanaonekana wana furaha sana kwa kiongozi wao kuwakutanisha katika uwanja wa makutanoni. Walinzi wanaonekana wamevimba kama mbuyu. Wako makini wakiwa wanamlinda kiongozi wao. Jukwaa limependezeshwa kwa kanga za rangi mbalimbali zilizofungwa kwa ustadi wa hali ya juu)

MRIRI:           (Anaongea kwa sauti ya kikakamavu ambayo inafanya wananchi wote wakae kimya na kusikiliza kwa makini. Anaanza kwa kuwasalimia wananchi). Habarini ndugu wanakijiji?

WANAKIJIJI: (Wanapokelea kwa sauti ya juu) Salamaaa...

MRIRI:         Ndugu wanakijiji wa Upepo na wanakijiji wa Mwanga leo hii nimeamua kukuiteni katika uwanja huu wa Makutanoni ukiwa ni kama uwanja wenye historia kubwa sana kati ya makabila haya mawili. Nina madhumuni machache ya kuwakutanisha wanakijiji wa pande zote mbili nikiwa kama mbunge wa mkoa wa Muungano hili ni jukumu langu. Ni miaka mingi sana tangu mapigano makubwa ambayo yalishawahi kutokea katika kijiji cha Upepo. Ni historia kubwa sana ambayo imebaki kwa makabila haya mawili… kwa historia ilivyo… imenifanya sana mimi kufanya mazungumzo ya karibu sana ili kuweza kupata mkutano wa pamoja ili kuweza kuyasuluhisha mambo haya. Kwa sababu utengano huu unaleta madhara makubwa sana katika jamii hizi mbili. Tulikaa vikao mbalimbali vya mwanzo na viongozi wa ngazi zote ili kulimaliza suala hili. Suala la ukabila kwa kweli ni suala baya sana ndiyo na huwa silipendi sana suala hili na ndiyo maana hata nikiwa bungeni suala hili huwa nalizungumza kwa hasira sana. (Analichangamsha jukwaa). Wanakijiji mpooo?

WANAKIJIJI: (Wanapokelea kwa sauti ya juu sana). Tupooo...

MRIRI:          Nafurahi kusikia hivyo. Hivyo, nikiwa kama mbuge wa mkoa wa Muungano ninapenda kutangaza kuwa kuanzia leo kijiji cha Upepo na kijiji cha Mwanga vinaungana na kuwa kijiji kimoja kiitwacho UNGA.

WANAKIJIJI: (Wananchi wanafurahi kwa shangwe kubwa baada ya kusikia maneno yale ya mbunge wao.

MRIRI:          Sasa ni muda wa wanakijiji wa vijiji vyote kukaa kwa pamoja… tupeane mikono kwa furaha na tubadilishana zana zetu za kazi.

WANAKIJIJI: (Wanapeana mikono, mwenye jembe anabadilishana jembe na mwenye fimbo kama ishara ya Amani na upendo katika muungano. Kwanzia muda huo wananchi wote wanaanza kujichanganya na kukaa kwa pamoja huku wakiwa na furaha)

MRIRI:          (Mriri anaendelea na hotuba yake). Leo ni siku ya furaha sana. Hivyo, kwanzia sasa tutakuwa na kijiji kikubwa kiitwacho UNGA ikiwa inamaanisha kuwa Upepo na Mwanga. Nimeamua kutangaza muungano huu ni baada ya kufanya majadiliano na viongozi wangu wa juu na chini na kuwapa hoja zenye nguvu juu ya muungano huu. Muungano huu utafaidisha sana kwa pande mbili zote. Mojawapo ni kuzidi kuleta Umoja na mshikamano kati yetu. Sote tunategemeana mkulima anamtegemea mfugaji na mfugaji anamtegemea mkulima. Kilimo kitazidi kunawiri sana. Viongozi watakuwa wanabadilishana sana mawazo yakiwa ni ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Suala la ukabila litakuwa limeisha na kila mtu kuanza kumthamini mwenzake kwa kuwa kila kabila lina heshima yake. Pia ni matarijio yangu kuwa UNGA kwa miaka michache ijayo mbeleni kwakweli kutakuwa na maendeleo ya kila aina. Miundombinu itazidi kukuwa, viwanda mbalimbali vitaanzishwa kwa kuwa hapa UNGA kuna malighafi za kutosha sana kama vile mifugo na mazao tofautitofauti. Kuna vivutio mbalimbali vya kiutalii. Vivutio hivi vitakuwa vya wananchi wote yaani wananchi wa UNGA si kusema tena kwamba wananchi wa Upepo wala wananchi wa Mwanga bali ni wananchi wa UNGA. Nikiwa kama Mbunge wenu kwa muda wote nitakaokuwa madarakani natumai kutakuwa na mabadiliko mengi sana yenye kuleta maendeleo. Nilikuwa nachukizwa sana na hali ya kiuchumi iliyokuwako katika kijiji cha Upepo pamoja na kijiji cha Mwanga. Nitaimarisha elimu kwa hali na mali ili tuweze kupata viongozi katika sekta mbalimbali wenye ujuzi mzuri katika sekta zao. Katika kijiji cha UNGA kuna utajiri mkubwa sana wa misitu. Katika misitu iliyopo kuna miti ambayo inawezakutufaidisha sana kama tukiitumia vilivyo. Ninawaahidi nikiwa kama kiongozi wenu na ninyi ndiyo mmpenipatia nafasi ya mimi kuwa bungeni lazima niwaletee mafanikio ya mimi kuwako pale. Ndugu wana UNGA nisiwe na mengi ya kunena sana bali nipende kumaliza kwa kusema kuwa nikushukuruni nyote kwa kuweza kunisikiliza kwa makini na kuweza kuonesha nderemo palipohitajika nderemo. Pia nazidi kuwaahidi kuwa matunda mengi yatakuja kwaajili ya muungano huu. Kwa sasa tusherehekee kwa amani muungano wetu huu. Ahsanteni sana. (Anashuka kutoka kwenye jukwaa huku akiwapungia mikono, wananchi wanampigia vigelegele)

 (Mandhari ya nyumbani kwa Mriri, Mandhari ya sasa si kama mwanzoni alipohamia. Nyumba tatu zikiwa zimezungushiwa ukuta mrefu. Kuna askari mmoja. Pembezoni mwa ukuta ule kuna miti mbalimbali ya matunda kama vile miti ya matopetope, mastafeli, maparachichi, miembe ya mbegu fupi na machungwa. Getini anaingia Kitori. Askari anamsimamisha na kuanza kumuuliza maswali juu ya ujio wake)

ASKARI:       (Amevaa mavazi ya kiaskari ya rangi ya kaki, amening’iniza bunduki begani). Mama habari yako?

KITORI:        (Anaongea kwa woga). Sa… salama...

ASKARI:       Una shida gani asubuhi hii unakuja kwa Mbunge?

KITORI:        Nina mazungumzo naye ya kifamilia. Ninatumai mtakuwa mna taarifa kuwa mbunge anataka kuoa. Kwa hiyo anataka kumuoa mwanangu.

ASKARI:       (Anamfungulia geti anaingia, askari anafunga geti kisha anampeleka) Sawa… twende huku.

(Askari anatangulia huku Kitori akiwa anamfuata nyuma. Anampeleka hadi kwenye hicho chumba cha mazungumzo. Askari anatoka pale na kwenda kumjulisha Mriri kuwa kuna mgeni wake.  Mriri anatoka akiwa anajua ana mazungumzo ya kiofisi kwa namna alivyovaa tu.  Amevaa suti nyeusi na shati likiwa jeupe huku akiwa amening’iniza tai vizuri. Anafika kwenye chumba hicho anakutana na sura ya Kitori anasimama kwanza hapo kama sekunde mbili hivi. Kitori anasimama na kumsalimia)

KITORI:        Shikamo kiongozi. Natumai unanikumbuka. (Anaongea huku anatetemeka).

MRIRI:            (Anaongea huku anaeleka kukaa kwenye kiti chake). Sidhani kama mimi ni mkubwa hivyo hadi kufikia kunisalimia mama. Wewe si Kitori… Mama yake Chiku?

KITORI:        Ndiyo ni mimi.

MRIRI:          Sawa. Heshima yako mama…

KITORI:       Sawa.

MRIRI:          Natumai kuna usalama huko ulikotoka.

KITORI:        Ndiyo kuna usalama wa kutosha kabisa. Kuna taarifa nilikuwa nakuletea.

MRIRI:          Nitaarifu.

KITORI:        Nakumbuka tangu zamani wewe ndiyo mchumba wa Chiku. Pia wewe ndiye kijana wa kwanza kwa kipindi kile kuja kunijulisha kuwa unataka kumuoa Chiku. Ila kwa hali ya kipindi kile ilivyokuwa ikashindikana wewe kufanikisha malengo yako.

MRIRI:          Nhaam nakumbuka. Vipi kwa sasa ana watoto wangapi na wote hawajambo?

KITORI:        (Anajibu huku akiwa anaangalia chini kwa aibu). Hawakuweza kupata mtoto. Kwa sababu hawakuishi hata kwa mwaka mmoja. Yule mume wake kumbe kipindi hicho tayari alikuwa ana wake wanne na Chiku akawa wa tano.

MRIRI:          Kwa hiyo ikawaje?

KITORI:        Wameshaachana. Chiku aliamua kurudi nyumbani. Kwahiyo ndiyo maana nikaamua kuja kwako kuleta taarifa hii. Kwakuwa tumeshaungana na hamna ukabila kwa sasa basi nikasema Mriri ndiyo mwanaume wa kwanza kwa Chiku basi nije nikutaarifu hili kuwa Chiku bado anakupenda na anahitaji umuoe.

MRIRI:          (Ananyamaza kama sekunde tano hivi kisha anamjibu). Aaaa Kitori unajua wengi hatujui kwanza ndani ya sekunde fulani nini kitatokea kwa mtu fulani… hatujui leo wala kesho patakuwaje kwa mtu fulani. Ila nashukuru nimejua tabia yako ilivyo japo kwa tabia hiyo sina haja nayo bali mimi nina haja na Chiku. Nasema bado nampenda Chiku na maandalizi yanaanza… kwanza Chiku niliwahi kuzungumza naye kwa haraka tu kabla hatujaungana. Nataka kweli nioneshe mimi nimeungana na watu wa Upepo.

KITORI:        (Anaipokea taarifa ile kwa furaha zaidi). Ahsante Mriri. Wewe ndiyo mwanaume pekee kwa Chiku.

MRIRI:           Sawa.

KITORI:        Sawa Mriri.

MRIRI:           (Anamuita askari) Askari aliyepo hapo nje amuite dereva wangu sasa hivi.

ASKARI:       Sawa mkuu. (Mlinzi anaenda haraka kumuita dereva)

MRIRI:           Sasa kuna dereva atakuja hapa ndiye atakayekupeleka hadi nyumbani. (Anaingiza mkono mfukoni, anatoa noti kazaa na kumpatia Kitori). Sasa hizi fedha chukua umpelekee Chiku ili akafanye manunuzi ya nguo nguo na baadhi ya vitu na itakayobaki hapo utachukua nawe yako.

KITORI:        Nashukuru sana.

MRIRI:           Sawa.

(Dereva anaingia, amevaa suti nyeusi. Mriri anampa maelekezo pale kisha Kitori anamuaga Mriri. Anatoka nje. Mriri anabaki pale pale akiwa anafurahi)

(Ni siku ya arusi, arusi ya Mriri na Chiku, kwenye ukumbi watu wamekusanyika kutoka katika sehemu mbalimbli. Ukumbi umepambwa kwa mapambo ya aina mbalimbali. Viongozi wa serikali wenye nyadhifa tofautitofauti wamehudhuria katika arusi hiyo. Watu wamekaa kwenye viti kwa mpangilio maalumu. Magari ya viongozi yapo sehemu hayo husika na magari ya watu wa kawaida yapo katika sehemu maalumu iliyotengwa. Mshindi anaonekana kwa mbalimbali akisalimiana na viongozi wenzake. Amevaa suti nyeusi. Naye mama Kichiko anaonekana kwa mbali akiwa amekaa na akina mama wengine. Mshereheshaji anasikika akisema)

MSHEREHESHAJI: Sasa ni ule wakati wa kupata chakula… Dj wapatie watu wimbo waasili watu waburudike wakati wanapata chakula.          

                                                                                                Tafsiri

                                    Viyendire viyendire,                Wamependana wamependana,

                                    Vareki haha vakaboye yavo,   Waacheni sasa wakafanye yao,

                                    Ni muda wavo haha,               Ni muda wao sasa,

                                    Kusina wovadalavya,              Hakuna wa kuwagombeza,

                                    Familia vakajenga,                 Familia wakajenge,

                                    Lukolo vyakakuryee,               Ukoo wakaukuze.

MWISHO

Comments

  1. Karibuni sana ndugu katika tamthiliya hii. Ni tamthiliya inayoelimisha sana. Maoni yako ni ya msingi sana...

    ReplyDelete
  2. Kijiji cha Upepo ni tamthiliya inayozungumzia zaidi matatizo ya kijamii yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali. Mwandishi anajaribu kuikumbusha jamii ya sasa kuonesha uhalisia wa suala la ukabila kwa miaka ya nyuma watu walivyokuwa wameubeba bila kujali madhara yake. Mwandishi anaona kuwa ni vyema jambo hili viongozi wa ngazi zote wakajitoa mhanga katika kuweza kusimamia suala hili. Ni vigumu jamii moja na jamii nyingine kusuluhishana hadi aweze kutokea kiongozi mwenye kuona thamani ya kutokuwa na migogoro katika jamii hizo. Vilevile, mwandishi anawakumbusha viongozi wa mataifa ya kusini mwa dunia kuwa huu ni wakati wa kusimama kwa pamoja ili kuvifaidi tulivyonavyo. Tusipofanya hivyo lazima tutazidi kuwaabudu wageni kuja kutupatia msaada angali mali tuliyonayo ni zaidi ya msaada tunaopewa.

    ReplyDelete

Popular posts from this blog

WIMBO WA AFRIKA MASHARIKI (EAC)

SIRI

PESA ILIVYO