KIJIJI CHA UPEPO
KIJIJI CHA UPEPO
MWANDISHI: SAID KAITA
SIMU: +255 783 372 139
BARUA PEPE:
saidikaita7@gmail.com
ONESHO LA KWANZA
(Jua limewaka. Mriri anatembea hatua tatu
kisha anasimama anatega masikio. Kuna kitu anakisikia kwa mbali, anatega
masikio vyema. Inasikika kwa mbali sauti ya ngoma) Ngit Ngit Ngit (Sauti ya mwimbaji anayesikika inaonesha dhahiri
mwimbaji huyo ana ujuzi wa uimbaji. Wanakaribia kutokea eneo alikokuwa
amesimama Mriri. Anaongea pekee yake)
MRIRI: Mbona
hizi ngoma kama vile hivi si … nahisi kama kuna jambo hapa. Wanakuja… nahisi kama wanakuja na njia hii hii ninakoelekea mimi.
Embu nifanye mpango nijifiche sababu huwa nasikia hizi ni kama ngoma za heshima
japokuwa siujui uheshima wake. (Harakaharaka
Mriri anajificha kwenye kichaka ili wasimuone. Muda si mchache wanafika karibu
na alipojificha Mriri. Wanasimama huku wakiwa wanaimba na kucheza. Wanaonekana
wasichana wawili wametangulizwa mbele huku wakiwa wamefungwa kaniki kifuani
hadi magotini ndipo zilipoishia. Nyuso zao zikiwa zimerembwa kwa michoro fulani
ya mistari ikiwa ni meupe na meusi. Shingoni wakiwa wamevaa shanga nyeupe pee. Miguuni
wakiwa pekupeku mithili ya waganga wakienda kuwanga. Wanamama wamejifunga
vibwebwe kuna mmoja anaimba, mwingine anapuliza filimbi na wengine wakiwa
wanapiga ngoma hizo kwa furaha sana)
MUIMBAJI:
(Kajifunga
kilemba kikubwa kama vile malikia huku akiimba kwa madaha. Uso wake umerembwa
kwa rangi tofautitofauti na rangi yake ilo nyeupe ndipo alizidi kupendeza zaidi).
Tafsiri
Vakurire vakurire, Wamekuwa
wamekuwa,
Vakurire vana visu
vakurire, Wamekuwa wana wetu wamekuwa,
Heshima kwavo razima,
Heshima kwao lazima,
Ko reka usinga, Kwa kuacha utoto,
Hantu vodoma kwa boha, Mahali wanapoenda pazuri,
Razima vaseke, Lazima wacheke,
Makulu kuyatanga, Makubwa kuyajua,
Sifa mojawavo ya
iri itendo. Sifa mojawapo ya hili tendo,
Makulu
vayatangire, Makubwa
wameyajua,
Vikalo vikulu, Vikao vikubwa,
Vovo kufika, Wao
kufika,
Mawazo kuseya, Mawazo kutoa,
HADHIRA: (Wanapokelea
kwa bashasha)
Vakurire
eeee vakurire, Wamekuwa
eee wamekuwa,
Vakurire
vana visu vakurire, Wamekuwa
watoto wetu wamekuwa,
Vakurire
eeee vakurire, Wamekuwa
eee wamekuwa,
(Wanamama wanaendelea kuimba huku wakicheza
vya uhakika kabisa bila kujali nini wala nini. Mabinti wamekaa kimya tu)
MRIRI: (Bado
kajificha. Anaanza kuongea kimoyomoyo). Mbona kama siamini ninachokiona?
Yule si Chiku au…. yule ni Chiku kabisa… au kwa vile wamempaka marangi rangi
ndiyo maana namfananisha? Lakini mbona wazazi wake siku za nyuma walinitaarifu kuwa
Chiku anaumwa sana kwahiyo amepelekwa hospitali na hayuko hospitali za karibu
ni huko mjini kabisa. Ndivyo alivyoniambia sasa hivi namuona Chiku pale.
Nilikuwa nikimsubiria sana mpenzi wangu takribani kama miezi kadhaa imepita
sasa nikiwa najua yuko hospitali alafu muda huu ninamuona hapa. Hapa kweli nina
changu? Oooh … Chiku wangu mbona kama naona umenisaliti. Ahadi gani tulikuwa
tumewekeana jamani. Heee… nataka nianze kulia hapa kumbe nimejificha hapa sinitaumbuka
sasa. (Wanamama wanaendelea na msafara
ndipo Mriri naye anaondoka)
ONESHO
LA PILI
(Muda ni huo huo mazingira ni ya nyumbani kwa
akina Mriri. Kuna vibanda vinne tu katika kaya yao. Upande wa mashariki kuna
zizi la ng’ombe. Mbwa anasikika akimbwekea mbwa mwingine. Mriri amekaa na dada
yake kwenye kirago wakiwa wamejiegemeza kwenye kibanda. Vibanda vyote
vimeezekwa kwa nyasi. Kichiko amevaa gauni la bluu, kichwani kajifunga kitambaa
cha rangi ya bluu bahari)
MRIRI: Dada
yangu… yaani huko nilikotoka… huko ni hatari… hadi nimejuta kupita njia hii ya
kutoka kijiweni.
KICHIKO:
(Anaongea
huku akiwa anamenya mbaazi zilizoko kwenye ungo na kuziweka kwenye safuria).
Unamaanisha nini Mriri
MRIRI: Hata sielewi nikuelezaje.
KICHIKO: Sasa mdogo wangu ukishindwa kunieleza mimi
nani tena mwingine?
MRIRI: Kwa
nini mnifiche?
KICHIKO: Nini?
MRIRI: Chiku…
KICHIKO: Chiku?
MRIRI: Ndiyo
… Chiku…
KICHIKO: Amefanayaje?
MRIRI: Mlinidanganya Chiku anaumwa kumbe
wamemkeketa. Nimekutana na msafara huko.
KICHIKO:
(Ananyamaza
kwa sekunde tatu. Anaweka ungo chini na kuacha kazi ya kumenya Mbaazi). Mdogo wangu ya zamani kuyafuta ni sawa na
kuichubua rangi yako. Hata ujitahidi kuichubua rangi yako vipi uhalisia utabaki
pale pale tu. Haya mambo yamekuwa yakifanywa tangu zamani. Kutoka enzi za
mababu na mababu mbona ni kitu kijulikanacho tu katika kijiji cha Upepo.
MRIRI:
Unamaanisha mimi na Chiku ndiyo
basi?
KICHIKO: Mriri
kumbuka mipango si matumizi. Pia Mriri hata kwa dawa mdogo wangu huwezi kumuoa
Chiku.
MRIRI: Unamaanisha
nini?
KICHIKO: Kuna
siri kubwa sana mdogo wangu hapa… Istoshe kwanza sisi ni maskini hatuna uwezo
wa kulipa mahari makubwa hivyo. Mwanamke kama yule katika kijiji hiki cha Upepo
ana heshima na thamani kubwa.
MRIRI: Tulipatana
lakini…
KICHIKO: Haya
wewe ng’ang’ania kuwa mmeshapatana na huyo Chiku. Kweli Chiku ni msichana
ambaye anajiheshimu tena kuliko hata wasichana wengine hapa kijijini. Lakini kuna vigezo mbalimbali vinaweza
kukufanya kabisa usimuoe huyo Chiku.
MRIRI: Vigezo
gani?
KICHIKO: Mama atakuja kukuelezea.
MRIRI: Wewe
ndiye unayetakiwa kunieleza vizuri kwa kuwa unaijua hii siri…
KICHIKO: Mriri…
mimi sina dhamana ya kukueleza lolote hapa… nimekugusia tu kwa kuwa umeileta
hii mada hapa. Mwenye dhamana ya kukuambia yote ni mama.
MRIRI:
Unanikatisha tamaa Kichiko.
KICHIKO: Wala…
huo ndiyo ukweli.
MRIRI: Natamani
sana mama aje nilijue fumbo hili nililofumbiwa kwa mpenzi wangu.
KICHIKO: Sawa…
leo alisema atawahi kutoka kibaruani.
MRIRI: Sijui
kama atakubali kunihadithia lolote.
KICHIKO: Atakubali tu… mimi nitatumia njia ya
kumuambia.
MRIRI: Nashukuru
sana.
KICHIKO: Sawa.
MRIRI: (Anainuka na kuingia kwenye Kitara chake
kilichoezekwa kwa nyasi. Anajilaza kwenye kitanda chake kilichotandikwa kwa
ngozi ya ng’ombe)
KICHIKO: (Anazungumza
pekee yake kimyakimya). Babu… babu ndiye unajua mambo mengi kuhusu Mriri.
Sasa leo uko mbali na macho yetu vipi siri hii atakuwa anaijua vizuri mama? Natamani
ungekuwepo hapa mjukuu wako angeyajua mengi juu yake na hadi kuwepo hapa. Kama
hukuwahi kumuambia mwanao sijui itakuwaje na wakati nimeshamuaminisha Mriri
kuwa mama anajua. Uzidi kuwa mahali pema huko uliko (anaendelea kumenya Mbaazi).
(Mazingira ni ya pale
pale nyumbani. Anaingia Huki ambaye ni mama Kichiko. Anaonekana amechoka sana.
Kichwani amejitwisha ndoo kubwa ya maji, mgongoni amebeba furushi la mzigo. Gauni
lake limejaa matope kila mahali. Kwenye mkono wa kulia amebeba galoni ya lita
tano yenye maji. Anamuita Kichiko)
HUKI:
(Huku akiweka galoni chini) Kichiko…
KICHIKO: Beee mama…
HUKI: Embu
njoo unitue mwanangu. Nakatire batuku (Nimechoka
sana).
KICHIKO: Sawa mama. Nakuja (Anainuka harakaharak). Shikamo mama.
HUKI:
Marhaba... Leo nimechoka sana.
KICHIKO: Pole
sana mama. (Anampokea galoni na kuiweka
chini, anamtua ndoo na kuipeleka moja kwa moja hadi jikoni)
HUKI:
(Anaufungua mzigo aliokuwa ameubeba mgongoni na kuufungashia kwenye nguo
vilevile bila kuonekana. Anaupeleka hadi jikoni. Anatoka nje na kuamua kukaa
chini bila hata kujali kama kuna vumbi. Anatoa sauti ya kupumzika kutokana na uchovu
alionao). Fuuuu.... mwanangu nimechoka...
KICHIKO: (Amesimama
mbele ya Mama). Inaonesha kabisa.
HUKI:
Choka ya leo imezidi.
KICHIKO: Inaonesha kabisa.
HUKI: Baba
yenu yupo?
KICHIKO: Baba…
ametoka tangu asubuhi. Sijui kaelekea wapi…
HUKI:
Ameondoka kimyakimya tu?
KICHIKO: Ndiyo…
HUKI: Kwani
wakati anatoka haukuwa nyumbani?
KICHIKO: Ndiyo.
HUKI: Ulikuwa wapi?
KICHIKO: Nilienda kuchota maji… alikuwa amekaa pale
kwenye mti (Ananyoosha mkono wake wa
kulia kwenye mti wa mwembe). Alikuwa amekaa kwenye kirago. Nilivyorudi
ndiyo sijamkuta hadi muda huu.
HUKI: Chakula
cha mchana amekula hapa?
KICHIKO: Hajala…
HUKI:
Sasa kweli asubuhi yote ile
tayari ameshatoka. Kwa ujumla hapo ameenda kilabuni tu… akirudi amelewa hadi
hatamaniki. Ani amloha? (Nani kamloga?)
KICHIKO:
Yaani.
HUKI: Yaani
hapo itakuwa amechukua hela zote za jana nilizotoka nazo kibaruani.
KICHIKO: Yaani
mama una kazi kubwa sana.
HUKI:
Mwanangu raha na uchungu wa
ndoa siku zote ajuae ni aliyeolewa tu na wala si aliyekuwa katika uchumba…
olewa au oa ndipo utajua vyote hivyo viwili vinakutokeaje.
KICHIKO:
(Anatulia
kama sekunde tano na kuhema). Fuuuuuu.
HUKI:
Ndiyo hivyo mwanangu. Mwanangu Mriri
yuko wapi?
KICHIKO: Yuko ndani.
HUKI:
Anafanyaje?
KICHIKO: Amelala.
HUKI:
Mbona mapema hivyo? Vipi kwani
anaumwa?
KICHIKO: Hapana…
ila nahisi kama kuna jambo linamsumbua.
HUKI:
Jambo gani tena?
KICHIKO:
Nahisi akiamka atakuja kukueleza
mwenyewe. Tumuache kwanza alale.
HUKI:
Sawa.
(Chumbani kwa Mriri, amelala usingizi mzito, ndoto
inamuijia. Ndoto inaonesha kuwa yuko Mriri pamoja na Mzee wakiwa katika
mazingira ya msituni. Giza la usiku wa manani kabisa. Mzee amejifunga kaniki
tu. Mwili wake umeshiba na nywele zake nyeupe pee. Kwa mbali panasikika sauti
ya Simba, bundi na sauti za wanyama wengine. Mzee ameshika mti mnene, kwenye
mizizi ya mti ule inaonekana haina hata mchanga. Imening’inia ikiwa mikavu tu. Ila
mizizi hiyo inaonekana kwa nguvu inayo. Mriri anashangaa mzee anachofanya.
Ghafla hali ya hewa inabadilika kwa sekunde kama ishirini. Haraka upepo mkali
unapita hadi miti inayumbayumba. Mriri anaogopa na anaamua kujishikisha kwenye
mti uliokuwa pale pembeni. Mti unang’oka na hata mti wa jirani yake unang’oka,
unachukuliwa na upepo na kwenda kuangukia mbali kabisa. Mriri anashangaa, anaamua
kukaa karibu na mzee ili asije akapata madhara. Mzee yuko tu amesimama wala
hana hata hofu na kinachoendelea kwa muda huo. Ameshikilia mti wake kwa
makini. Baada ya upepo kuisha tu sekunde
chache joto linatokea na hali ya upepo mkali inapotea kabisa. Mzee anaanza
kumuongelesha Mriri)
MZEE: (Anaongea
huku akimuangalia Mriri kwa umakini. Anatoa sauti nzito) Mjukuu wangu kuwa
huru kwenye haya uyaonayo.
MRIRI: Sawa
babu. Ila tuko wapi hapa babu?
MZEE: Tuko
kwenye msitu wa manene. Huu msitu una maana kubwa sana kwako.
MRIRI: Maana
kubwa ukiwa unamaanisha nini babu?
MZEE: Mengine
utayajua tu nikishakuachia kazi.
MRIRI: Sawa
babu.
MZEE: Unaona
huu mti?
MRIRI: Ndiyo nimeuona. Ndiyo nilikuwa nataka
nikuulize kwamba huo mti unaenda kuupanda wapi angali hapa tayari kuna miti
mikubwa hivyo?
MZEE: Ahaa…
sawa… ni swali zuri sana umeniuliza. Kwanza umejua huo upepo mkali uliopita
hapa umetokea wapi?
MRIRI: (Anafikiria kwa sekunde chache labda anaweza kupata
majibu. Anaona hamna majibu. Anatingisha kichwa na kusema). Kwa kweli sijui
umetokea wapi.
MZEE: Sawa…
unajua hii miti imeenda wapi?
MRIRI: Siimeangukia
huko mbali.
MZEE: Sawa…
sipendi kumtafunia mwanafunzi wangu majibu. Maswali niliyokuuliza ukashindwa
kuyajibu. Kazi nitakuachia kwa ajili ya kwenda kufikiria.
MRIRI: Nitaanzia
wapi?
MZEE: Utaanzia
tutakapomalizia shughuli mimi na wewe.
MRIRI: Kuna
shughuli gani?
MZEE: Ahaaa
ahsante umejaaliwa maswali yenye mtiririko na yanaleta furaha na hamu ya mimi
kukuachia kazi ya kwenda kufikiria nyumbani.
MRIRI: Sawa
babu.
MZEE: Sasa
unaona hiyo sehemu ambayo miti imeng’oka? (Ananyoosha
kidole sehemu yenye shimo)
MRIRI: Ndiyo…
nimepaona.
MZEE: Sawa…
huu mti tunatakiwa tukaupandikize pale.
MRIRI: Sasa
mbona unaupanda huku katikakati ya msitu kabisa?
MZEE: Ulitaka
tuupande wapi?
MRIRI: Kule
pembeni kabisa.
MZEE: Ondoa
shaka. Huu mti hapa ni mdogo sana unavyouona… ila leoleo utakuwa na utazidi hata
miti yote iliyopo katika huu msitu na miti yote itakuwa inauabudu huu mti na kuwa
kama kiongozi wao mkuu na hatotokea kiongozi mwingine katika huu msitu kama
huyu. Mti huu utakuwa umefungwa na ndugu na majirani kesho na keshokutwa tayari
huu mti utakuwa ni mkubwa sana. Huu ndiyo muunganiko wa miti yote… kila kitu
utajionea. Mti huo ndiyo utakuwa mshindi wa miti yote ambayo ilikuwa mibovu
hapa na ndiyo utakaoleta Amani kubwa hapa. Harufu mbaya ambayo ipo katika hii
miti lakini mti huu utaitoa harufu hiyo mbaya na kufanya kuwe na harufu nzuri.
MRIRI: Sawa
babu. Tukaupande huo mti.
MZEE: Sawa. (Wanaelekea kwenye hilo shimo. Upepo uliopita
pale uliacha alama kubwa kabisa katika sehemu hiyo). Sasa huu mti
tunaupanda hapa. Tukishamaliza tu kufukia mizizi yake tutasimama kwa muda
kidogo huku tukiwa tumerudi nyuma kama hatua tatu hivi na tufunge macho.
MRIRI: Sawa.
MZEE: Simama
hapo tulia niupande huu mti. (Mriri
anasimama hapo na kuzidi kuangalia nini kinaendelea pale. Mzee anaupanda ule
mti na kuufukia). Tayari tumeshamaliza kazi.
MRIRI: Sawa
babu.
MZEE: Haya
tufumbe macho kama tulivyoahidiana.
MRIRI: Sawa
babu.
WOTE: (Wanasimama wote kwa dakika tatu huku wakiwa
wamefumba macho. Yanayoendelea pale kwa muda huo ni mazito sana. Kuna moto
mkali unawaka katika eneo hilo na moto unasambaa msitu mzima. Ilipobaki dakika
moja moto unazimika na hali ya mwanzoni inajirudia. Ule mti unaonekana unazidi
kupanda juu na kuwa mnene zaidi na kwa shimo la pembeni mbegu ya mti ikaangukia
pale na mbegu ile inaanza kuota na kukua. Dakika zinaisha wanaanza kufungua
macho. Wanafungua macho Mriri anakutana na mti kwa mbele. Haamini anachokiona
mbele yake. Mriri anamuuliza Mzee).
MRIRI:
Mbona
hii miti imekuwa haraka hivyo?
MZEE: Ndiyo
imekuwa.
MRIRI: Mbona hilo shimo lingine hatukuwa tumepanda
mti?
MZEE: Mbegu
imeangukia hapo.
MRIRI: Embu
nielezee basi hata kwa uchache.
MZEE: Mimi
ninarudi kwetu.
MRIRI: Wapi
huko?
MZEE: Mbali
sana. Kayafikirie maswali ambayo sijakujibu na hili tukio lililotokea hapa. Kwaheri.
(Mzee anapotoa pale pale na ghafla mwanga
unatokea mkali na giza linafuatia)
MRIRI: Babuuu.
(Mriri anavurumbuka kutoka kwenye ndoto ile
na kukaa kitandani huku akiwa anahema kwelikweli). Hii ndoto ina maana
gani? Kila swali nililomuuliza hajanijibu na kuamua kuaniachia mimi
nikahangaishe bongo langu. Mbona sielewi kabisa yaani… eeee Mungu wangu embu
niletee basi hata ufumbuzi wa ndoto hii. (Ananyamaza
kwa sekunde chache) … hapana simuelezi yeyote. Tuseme nimueleze mama? Nimueleze
dada? au baba? Laaa embu kwanza niitafakari mwenyewe ndipo nitajaribu kwenda
kumueleza mama au dada. Embu nirudie kulala labda ndoto ya kunifafanuliwa
inaweza ikaja. (Anajirusha kitandani analala
bila hata kujifunika shuka. Miguu kaining’iniza chini. Anahema kama ng’ombe).
Fuuu…
(Mandhari ya nyumbani.
Kuna sauti za ng’ombe zinasikika wakiwa wanaingizwa kwenye zizi lao. Sauti ya Huki inasikika akiwa nje anamuita Mriri)
HUKI: Mriri
(Amesimama mlangoni amejishika kiuno)
MRIRI: (Anaitika
kwa kukurupuka). Nhaam mama…
HUKI: Embu
inuka.
MRIRI: Sawa mama … haya nainuka mama.
HUKI: Sawa…
uinuke moja kwa moja. Naijua tabia yako.
MRIRI: Naamka mama.
HUKI: Nakusubiri
hapa nje. (Anaamua kukaa kwenye kirago).
MRIRI: (Anatoka
huku akipikichapikicha macho na kuangalia mazingira ya nje. Anamsalimia mama).
Mama shikamoo…
HUKI:
Marhaba Mriri. Vipi mbona
umelala muda mrefu sana… ulikuwa unaumwa?
MRIRI:
(Anakaa
kwenye kigoda). Hapana mama… sikuwa naumwa.
HUKI: Shida
nini kama huumwi?
MRIRI: (Ananyamaza
huku akiwa anaangalia chini na kujikuna kichwa).
HUKI:
Mbona unanyamaza mwanangu? Embu
nieleze nini kimekusibu leo? Kwasababu leo hata haikuwa zamu yako ya kuchunga
lakini umechoka kama mtu ambaye alienda machungajini kabisa. Kuwa huru
mwanangu. Embu toa yaliyoko moyoni mwako. Sipendi usononeke kabisa.
MRIRI: (Anajikaza
na kuanza kutoa ya moyoni) Mama … natumai mimi nilishawahi kuongea na wewe
kuhusu Chiku.
HUKI: (Anashtuka kidogo) ndiyo… ulishawahi.
MRIRI: Ahaaa … sawa… Mada niliyokuwa
nikimuongelea unaikumbuka?
HUKI: Ndiyo.
MRIRI: Sawa.
Nilikutaarifu kuwa mimi na Chiku ni wachumba. Lakini kwa siku ya leo kwa kweli
nilichokutana nacho huko njiani nilipokuwa natoka matembezi yangu sikuamini
nilichokiona. Niliamua kujificha kwanza ili hata watu hao wasinione kabisa. Nimemuona
Chiku akiwa amefungwa kaniki walikuwa wawili huku watu wakiwa wanawacheza. Nilipoona
vile nilikuja kumuelezea Kichiko lakini hakutaka kuongolea lolote zaidi ya
kusema wewe ndiyo unajua yote juu ya suala hili. Unanificha nini mama?
HUKI: (Anatafuta namna ya kumjibu). Mriri… sijui
nianzie wapi na niishie wapi…
MRIRI: Anzia hapo hapo mama. Ninatamani sana kuujua
ukweli kuhusu mimi na Chiku. Ni vyema sana ukanieleza kabisa kwa undani. Yaani
nakuomba sana tena sana nakuomba mama.
HUKI:
Unajua Mriri siku zote moyo
hutamani sana kutimiza lengo ambalo moyo umelitamani bila hata kujali kama
kutakuwa na vikwazo vyovyote. Niseme tu kwa kunyoosha maneno ni kwamba … Mriri
ni kweli ulishawahi kunieleza kuhusu uhusiano wako na Chiku lakini Kichiko
kakuambia huwezi kumuoa au siyo?
MRIRI: Ndiyo.
HUKI: Mriri
jambo hili nitakalokueleza hapa natumai sikuwahi kukuelezea hata siku moja.
Kwahiyo nitakapokuelezea usitishike sana bali ni ukweli wa kujua kuwa wewe
utaweza kumuoa Chiku au laa.
MRIRI: Sawa
mama nakusikiliza … ndiyo maana nimeamua kukueleza suala hili nikijua kuwa wewe
lazima unielezee kwa undani zaidi juu ya suala hili. (Sauti ya Nkorio inasikika)
HUKI: Nitakuelezea
kesho juu ya suala hili. Baba yako huyo anaingia. Anaonekana amelewa chakari.
MRIRI: Sawa mama.
WOTE: (Wanainuka na kila mtu kuelekea kwake. Mama
anaelekea chumbani kwake na Mriri anaelekea kwenye kitara chake. Giza limeshaanza kuingia kabisa. Nkorio
anaimba akiwa nyuma ya boma ya ng’ombe).
Mengi nimejionea, Mengi nimejionea,
Ujanani
sikuyafanya, mengi nilijionea,
Leo niko uzeeeni, ya ujanani kuyafanya,
Kweli nimechelewa, kweli nimechelewa,
Kuvuka hatua, si jambo jema kabisa,
(Anaangalia kwenye zizi kama kuna usalama.
Anaangalia na kuondoka kisha anaelekea hadi jikoni)
NKORIO: Wewe Kichiko wewe?
KICHIKO: Beee baba. (Anatoka jikoni kisha anasimama mlangoni na kumsalimia baba). Shikamo baba.
NKORIO: Marhaba
binti yangu. Huko jikoni pana jambo au ndiyo tu?
KICHIKO: Unamaanisha
nini baba?
NKORIO: (Anayumbayumba). Huko jikoni kuna
chakula?
KICHIKO: Ndiyo kipo.
NKORIO: Mama
yuko wapi? Hajarudi hadi muda huu?
KICHIKO: Amesharudi…
NKORIO: Yuko
wapi?
KICHIKO: Yuko ndani.
NKORIO: Yaani wewe Huki ukae ndani wakati mimi
nimekuja hapa. Ni adabu gani kabisa hiyo? Tangia asubuhi hatujaonana hapa hadi
muda huu unasikia sauti yangu lakini bado unaamua kujifungia huko ndani kama mwari.
Hivi huyu mama yako ana nini?
KICHIKO: (Ananyamaza).
HUKI:
(Anatoka chumbani kwake. Anasimama na kusema hivi). Hivi Mume wangu
kwa nini unapenda kila siku tugombane?
NKORIO: Wewe ndiye unayesababisha hadi tugombane.
HUKI: Kivipi?
NKORIO: Alafu
usijifanye hunielewi hapa. Maswala ya kuulizana maswali kama mahakama ya watu
wa kuzimu. Mimi ni mume wako nikiongea kitu embu jaribu kunyamaza kimya tena
kimya kweli. Nitakupiga kibao sasa hivi.
HUKI: (Anakwepa). Hivi mume wangu huwezi hata
kunionea huruma tu. Tangu asubuhi nilikuwa huko vibaruani na nimechoka
kwelikweli na hata kama nimechoka hivi hela zenyewe wewe ndiye unayechukua na
kwenda kulewea tu huko na kuwalewesha marafiki zako tu huku hata hujui hizi
pesa zimepatikanaje. (Ananyoosha kidole).
NKORIO: Weee…
yaani unathubutu kuniita mimi mwizi kabisa? Yaani mimi mume wako kabisa alafu
unanivisha jina lingine kabisa? Hivi wewe mwanamke mimi nahisi hata
aliyekulaani ameshakufa. Yaani huna adabu kabisa…Yaani mimi niache kwenda
kunywa pombe sababu kuwa hela ni zako. Wewe ndiyo mke wangu una wajibu wa
kunihudumia.
HUKI: Mwanaume
wewe…
NKORIO: Nini?
HUKI: Yaani
mwanaume unachukua hela na kwenda kulewea na marafiki zako ambao ni marafiki wa
unafiki tu.
NKORIO: Embu
niache mimi nikalale kwanza. (Anaamua kuelekea kulala)
HUKI: Sawa…
ila ukweli unauma.
(Mriri anaonekana yuko anaota moto huku akiwa
katika wimbi la mawazo sana)
ONESHO LA TATU
(Mazingira ni ya pale pale nyumbani. Sauti za
ndege zinasikika kwa mbali. Mama na Mriri wamekaa kwenye vigoda wakinywa uji. Kila
mtu ana bakuli la uji)
HUKI: (Anaweka bakuli chini) Mriri...
MRIRI: Nhaam mama.
HUKI:
Najua jana tuliishia njiani …
nilitamani sana nikuhadithie jambo lililokuwa likikusokota moyoni mwako.
MRIRI: Ni kweli mama … leo nimelala nikiwa
nimejawa na mawazo sana.
HUKI:
Haina shida. Afadhali hata huyu
baba yako kaondoka nitaweza kukueleza yote. Kwa sababu huwa hapendi kabisa mimi
na wewe tukae hivi. Huwa anajua kabisa kuna jambo tunalipanga.
MRIRI: Nakusikiliza mama.
HUKI: (Anakohoa kikohozi cha kuweka sauti vizuri)
Mriri…. siku zote huwa nakuambia kwamba sisi ni mang’ombe wa kuanguka muda wowote.
Kwa hiyo, naweza nisikuambie hii siri alafu mwisho wa siku nikianguka leo
najikuta nimeacha kovu kwako ambalo ni kubwa sana. Ila nakuomba kuna hadithi
nitakuhadithia juu ya wewe kuwa hapa.
MRIRI: Sawa… (Anakaa vizuri katika namna ya kutaka kumsikiliza kwa makini)
HUKI: (Anaongea kwa hisia) Kipindi ukiwa na
umri wa miaka miwili katika hiki kijiji cha Upepo paliwezakutokea vita kubwa
sana kati ya wakulima na wafugaji. Wakulima walipenda sana mazao yao yasiliwe
na mifugo ya wafugaji. Lakini wafugaji walikuwa wabishi sana… kwa hiyo
walitumia mbinu zote ilimradi mifugo yao ipate majani. Ilifikia wakati kabisa
wafugaji walianza kuwafunguliwa mifugo yao usiku wa manani.
MRIRI: Eee… usiku wa manani kabisa? Mbona ni
wakati mbaya kabisa huo.
HUKI:
Kwa
hiyo kulikuwa na kiongozi wa wakulima na kiongozi wa wafugaji. Sasa aliyekuwa
kiongozi wa wakulima alikuwa na nafasi mbili. Yaani alikuwa ni mwenyekiti wa
kijiji cha Upepo na hapo hapo akiwa ni kiongozi wa wakulima. Huyu jamaa alikuwa
ni mtu mwenye ushawishi sana na pia alikuwa akijitolea mhanga sana katika
kuwasaidia wakulima. Kijiji cha Upepo kilineemeka sana wakati wa uongozi wa
mwenyekiti huyo aliyekuwa akiitwa Majuva. Majuva alifanya kazi kote kote usiku
na mchana. Basi kwa mwaka huo palivyotokea vita hivyo ilikuwa ni kipindi
ambacho tayari mazao kama vile mahindi ndiyo yalikuwa yameanza kuiva. Unajua
nini kilitoekea?
MRIRI: Sijui mama.
HUKI: Sasa
mwanangu naona hapa jua limeshaanza kupanda kabisa. Tulia kwanza niende
kibaruani alafu baadae nitakuja kumalizia hadithi yako. Sababu nikichelewa huko
nitakuta watu wameshapata sehemu nyingi na watapata hela.
MRIRI: Daaa kweli mama utakuja kumalizia?
HUKI: Ndiyo
Mriri (Anainuka na kuchukua zile bakuli
na kuelekea jikoni. Anaweka vyombo vile na kutoka huku akiwa amechukua jembe
lake la kibaruani ndoo ya kwenda kuchotea maji) Mwanangu mimi naenda.
MRIRI: Sawa mama.
(Mandhari ya kilabuni. Kilabu kimeezekwa kwa
majani tu. Kimechoka sana. Kwa nje panaonekana kuna Malambo makubwa ya kupikia
pombe yamebandikwa hapo yanafuka moshi kama msitu uliowaka moto. Mlangoni kuna
watu kumi wamelala. Walipolala kuna vumbi. Nyuso zao zimepauka na kuwa kama soli
za viatu. Miguu ndiyo hatari kabisa. Wengine wamevaa viatu na wengine hawana
hata nguo kabisa wamebaki na vinguo vyao vya ndani vilivyojaa kunguni. Nkorio
anaonekana yuko na marafiki zake watatu. Hapo walipokaa kuna chubuku zina
pombe. Kila mtu anapuliza pombe kwa furaha tu)
NKORIO: (Amevaa sarawili. Kichwani amevaa boshori
jeusi tii) Yaani leo kunyweni mtakavyotaka hadi mkate moto.
WOTE: (Sauti
zao za pombe). Hamna wa kukata moto hapa.
NKORIO: Nyiye
kunyweni bana… Jana shemeji yenu alienda kibaruani… amepiga kazi kwelikweli. Unajua
ananipenda sana… akaamua kunipatia zote. Ndiyo maana nimeamua kabla hata kuku
hawajaamka nikaja kuwaamsha ili tuje kumwaga radhi hapa.
CHOGO: (Amevaa koti refu hadi chini ya magoti. Koti
hilo ni muda halijala povu. Ndevu zimezunguka mdomo mzima na weusi wake
aliokuwa nao ni macho tu ndiyo yanaonekana. Anacheka) Hahahaha… yaani mke
wako anakupenda sana. Hadi kakupa zote hizo… wewe ni hatari sana… unajua
kufinya sana…
TUNDU: Yaani
wewe Nkorio kweli mke wako ana akili sana.
NKORIO: Kwa nini?
TUNDU: Anaamua kukuhudumia hivi ili usijeingia
kwenye himaya nyingine alafu ukaharibu familia ya pale.
CHOGO: (Anacheka
kisha anasema). Mke wako ana akili sana.
MAPANGA: (Anaongeaa
huku akilalalala. Amenyoa kipara, ameacha ndevu) Ila mnajua… hapa
tunafurahi kwa hela za mtu… jasho la mtu hili limevuja.
WOTE: (Wanaangaliana)
MAPANGA: Yaani wewe Nkorio unaamua kuchukua kabisa
pesa za mke wako. Mchana mzima jana ameshinda kibaruani… na jua lote lile. Unajua
kuna muda inabidi tuwe na roho ya huruma. Naona wote… wote tunafurahia tu hili
jambo. Huu ni ujinga kabisa tunaufanya. Tunawatesa sana wanawake. Wanateseka
mchana tena usiku tunawawajibisha… huruma mbona hatuna?
NKORIO: Embu
niache bana… Kama mke wako hakupendi nenda kajinyonge na kamasi huko.
MAPANGA: Yaani mke wangu ananipenda tena sana…. Lakini
siwezi nikamnyanyasa kwa vile ananipenda ndiyo nitumie hiyo nafasi na kumfanyia
hivyo. Huoni ni uonevu kabisa? Yaani mimi hata nilewe vipi lakini si kumvunjia
heshima mke wangu wala kumtesa. Hivi mbona Nkorio wewe ni mkubwa tu lakini huna
hata ule utu kabisa.
NKORIO: Wewe niache bana. Embu kunyweni pombe. Huyu
anajifanya ananitolea povu la kijinga hapa. Embu nenda zako kama hutaki kunywa
hii pombe.
MAPANGA:
Yaani nyiye ni marafiki zangu lakini katika hili kwa kweli nawapinga kabisa.
Kwa sababu huo ni uonevu kabisa. Mfano wewe Nkorio ndiyo ungekuwa mwanamke.
NKORIO: Mimi siwezi kuwa mwanamke.
MAPANGA: Ndiyo maana nimesema mfano tu.
NKORIO: Hata
kwenye mfano siwezi kuwepo.
MAPANGA:
Haya kuwa mgumu kama mkate wa waisraeli. Muda mwingine huwa tunakaza bongo bure
tu. Ila tukikaa na kufikiria ndipo tutajua kuwa tuna makosa au laa.
NKORIO: Embu
nenda zako bana wewe. Yaani kwanzia leo mimi siyo rafiki yako kabisa. Marafiki
zangu ni hawa hapa tu. Acha tulewe.
MAPANGA:
Hivi nyinyi mnaoambiwa ni marafiki yaani
hata hamna wivu. Huyo rafiki yenu ana mke na watoto nyiye ndiyo hivyo tu mnazidi
kufuga madevu tu hapa. Ukubwa siyo ndevu… ndevu hata mbuzi anazo…
WOTE: (Wanainuka na ugomvi unaanza. Wanashikana
mashati. Wote wanamchangia Mapanga. Mapanga anaamua kuondoka na kuanza kuongea
akiwa amewageukia huku akiendelea na mwendo). Hata kama mkinipiga ila ujumbe
umefika. Mijitu mikubwa kumbe mnamiliki ndevu tu. (Anatembea huku anayumbayumba. Anaanza kuimba na barabara nzima
akiifanya ni yake).
Mwanaume mjinga,
Mwanaume mjinga,
Hula hela za mke
wake, asubuhi na mapema,
Kilabuni aamkia,
hela siyo zake,
Afanyia kufuru, kwa
marafiki zake,
Wampigia makofi,
furaha ya pombe.
Huo ni ujinga, huruma
kuweni nayo…
(Wanaonekana Mriri na Chiku wakiwa wamekaa
pembezoni mwa mfereji kwenye gogo la mti)
MRIRI: (Amevaa suruali nyeusi na shati jekundu chini
amevaa masendeu). Chiku… tulianza mapenzi tangu tukiwa tumekuwa. Yaani
tayari tukiwa na hisia za mapenzi kila mtu kujua hisia kuhusu mtu fulani. Tukaahidiana kweli lazima tutaoana.
Japokuwa siku zote mipango si matumizi si lazima iwe hivyo ila inaweza ikawa
hivyo kwa namna mipango tu ilivyo. Siku zote nilikuwa nikijua kabisa kuwa Chiku
ndiyo mke wangu mtarajiwa. Lakini kwa namna nilivyojionea kwa kweli sijui kama
safari yetu itaweza kukamilika. Najua mapenzi ni upofu ndiyo maana hakuna ajuae
kwenye mapenzi zaidi ya yaliyopita tu.
CHIKU: (Amevaa
gauni refu jekundu, kichwani amejifunga kilemba cheusi. Kwa pembeni kuna ndoa
yake ikiwa na maji). Mriri kweli najua ni zamani tumeanza safari yetu ya
mapenzi. Hadi tumefikisha umri huu hatujawahi kuonesha dalili za kuachana…
japokuwa kukwaruzana kwa hapa na pale hapakuwa panaepukika. Najua hadi nyumbani
kwetu walikuwa wanajua kabisa uhusiano wetu wa kimapenzi na kweli ulishawahi
kuwaeleza kabisa. Lakini nyuma ya pazia kuna jambo fulani litakalofanya mimi na
wewe tusioane.
MRIRI: (Anashituka kisha anasema). Embu tulia
kwanza Chiku. Unasema kuna jambo litafanya tusionane?
CHIKU: Ndiyo. Kuna siku mama yangu alinihadithia
hadithi fulani hivi.
MRIRI: Hadithi
gani hiyo na ilikuwa inahusu nini?
CHIKU: Hadithi hiyo ilikuwa na lengo la
kunikanya mimi kutenda jambo fulani.
MRIRI: Usifanye
nini?
CHIKU: Natamani nikuelezee sema ni hadithi
ndefu sana. Kwa muda huu itakuwa ni vigumu sana kwa sababu nitachelewa alafu
mama ataenda kugomba sana.
MRIRI:
Nakuomba
unidokezee hata kidogo tu. Kwa sababu utakuwa umeniweka mahali pabaya sana
kimawazo.
CHIKU: (Anainuka na kuchukua kata yake kisha
anajitwisha ndoo). Nitakuambia siku myingine. Kwa sasa hivi muda umeshaenda
sana. Si vizuri mwanamke kuchelewa nyumbani.
MRIRI: (Mriri anabaki anashangaa tu namna Chiku
anavyoondoka. Mikono ameweka kichwani kama mwana aliyeachwa na mama).
(Mandhari ya nyumbani, Huki na Mriri wanaota
moto)
HUKI:
(Anaongea huku akiwa anachochea moto. Moshi mkali unafuka… anakohohoa)
Kohokoho… Mriri acha niendelee nilipoishia muda ule.
MRIRI: Embu niambie mama. Sababu moyo wangu unapata
maumivu juu ya jambo hili. Naomba unisimulie.
HUKI:
Sawa. Ni kwamba … Majuva
alizidi kupapambania hapa katika kijiji cha Upepo. Lakini vita hiyo ilipozidi
basi naye aliamua kujiunga na wakulima wenzako akiwa kama kiongozi wao. Kwa
kipindi hicho tayari alikuwa na watoto wawili. Mmoja wa kiume na mwingine wa
kike. Mwana wake wa kike ndiyo alikuwa wa kwanza. Kwa hiyo hata mambo yote
yanatokea hayo naye alikuwa akiyaona kabisa. Vita vile vilipiganiwa kwenye
mashamba ya Majuva ambapo mashamba hayo yalikuwa karibu na kaya yake iliko.
MRIRI: Hatari!
HUKI:
Wewe sikia kilichotokea.
MRIRI: Sawa.
HUKI: Basi
vita vile vilipamba moto na kupamba kweli. Mwenye upanga, upinde na kila aina
ya silaha alichukua na kwenda kupigana. Hapakuwa na mwamuzi kabisa. Majuva naye
alijitahidi sana kuwapiga wafugaji kwakuwa naye alikuwa na nguvu sana lakini
wapi walimchangia na kumpiga kipigo cha mbwa aliyeingia msikitini.
MRIRI: (Alishtuka
na kuuliza). Alipona sasa?
HUKI:
(Alikuwa akiongea kwa sauti ya huzuni). Ya Mungu mengi… kwa kweli walimpiga
sana na kumkatakata viungo vyake vyote kama nyama inayoandaliwa kupelekwa
jikoni ndipo ikawa mwisho wa maisha yake.
MRIRI: Sasa mke wake na watoto wake ikawaje?
HUKI: Mke
wake baada ya kuona vile alishikwa na hasira sana akaamua kuchukua panga
akitaka kuingia vitani. Alipofika hapo hakumgusa mtu hata mmoja bali ni
wafugaji wote walimshambulia na silaha zote hata alipokata umauti hapo hapo.
MRIRI: Hawakuwa na huruma kabisa… sasa wanaye
vipi?
HUKI:
Kwa wanaye kwa kweli yule wa
kike alifariki. Kwasababu nyumba yao ilibomolewa na kuchomwa moto. Kwahiyo
alifia huko huko ndani alikokimbilia.
MRIRI: Kwa yule wa kiume ikawaje?
HUKI: Yule alipona. Kwa sababu mama yake
alimuacha jikoni. Kwahiyo kule jikoni wafugaji hawakupagusa wakiwa wanajua kuwa
hapakuwa na mtu. Ndipo baada ya watu wale kuondoka ndipo wanakijiji tukaenda
pale…. Mimi na Nkorio ndipo tukaingia hadi pale jikoni na kumkuta huyo mtoto
pale.
MRIRI: Kumbe alipona?
HUKI: Ndio…
alipona… yule mtoto tuliishi naye hadi leo hii.
MRIRI: (Alishtuka
na kusema). Mbona kama sijakuelewa
mama?
HUKI: Mwanangu hii hadithi kwa ujumla
ilikuwa ikikuhusu wewe. Sijawahi kukuhadithia hata siku moja. Wewe ndiye mtoto
pekee wa Majuva. Mriri wewe si mwanetu tulipenda tu kukulea hapa baada ya
majanga yale kutokea. Hatukuwahi kukwambia. Tumeishi na wewe kwa muda mrefu…
MRIRI: (Hakuwa
na la kuongea kabisa juu ya mada hiyo. Alikaa kimya kama dakika moja hivi.
Hakuna aliyethubutu kutoa neno lolote kwa muda huo. Kichwa alikiinamisha chini
kama kondoo wakiwa wamepumzika).
ONESHO LA NNE
(Mandhari ya mbugani, Mriri anachunga
ng’ombe. Yupo katika dimbwi la mawazo, anatokea Anatokea Salala ambaye ni mdogo
wa Chiku)
SALALA: (Akiwa ameshikilia karatasi iliyokunjwa.
Anamuita). Kaka Mriri.
MRIRI: (Anashtuka… sababu hakuwa anataraji kama Salala
angetokea pale) Nhaam…
SALALA: Shikamo kaka Mriri.
MRIRI: Marhaba…
hujambo?
SALALA: Mimi sijambo. Mbona unaonekana una
mawazo sana?
MRIRI: (Anatabasamu)
Hapana mdogo wangu. Sina mawazo ya kivile ni ya kawaida tu.
SALALA:
Hapana… hiyo siyo kawaida…
MRIRI:
Ndiyo ukweli…
SALALA:
Kwamba una mawazo sana.
MRIRI:
Hapana… yaani kawaida tu ya
mwanadamu kuwa na mawazo.
SALALA:
Hapana… kwa wewe imezidi.
MRIRI:
Umejuaje?
SALALA:
Namna nilivyokukuta tu hapa.
MRIRI:
Ni mambo ya kawaida tu.
SALALA: Sitokaa…
kuna mzigo tu dada kanipa nikuletee. (Anampa
ile karatasi) Haya kwaheri.
MRIRI: (Anaipokea karatasi na kuifunua, anaanza
kuisoma)
Kwako mpenzi (Mriri),
Natumai u bukheri wa
afya. Mpenzi kwangu kuwa bukheri ni hadi nitakapojua wewe hali yako ikoje. Bado
ninakukumbuka na kukuheshimu uliyeniingiza ukubwani.
Tumekuwa muda mrefu
mimi na wewe katika ulimwengu wa mahaba, ulimwengu ambao ulikuwa na milima na
mabonde japokuwa tulipendana kwa dhati, vizuri na vitamu tulipeana. Tulipanga
mengi sana ni vipi tutaishi na mengi zaidi. Lakini wahenga walinena hakuna
marefu yasiyokuwa na ncha na mbio za sakafuni huishia ukutani ndipo nilipofikia
kuamini kuwa mipango siyo matumizi.
Mpenzi, ninapenda
kukutaarifu jambo hili kwa sikitiko la hali ya juu kuwa, penzi letu tulilokuwa
nalo muda mrefu halipo tena, jambo hili liko nje ya uwezo wangu. Ni muda
umeisha naamini utakuwa umeambiwa mimi siyo kabila lenu. Kwa maana hiyo itakuwa
ni vigumu wewe kunioa mimi. Mpenzi wangu ulonihudumia kihisia kwa muda mrefu
nakuomba usihuzunike sana kwa hili, japokuwa naamini ni vigumu sana kuvumilia. Vitamu
ulivyonipa bado ninavikumbuka, utashangaa sana kwa nini hata kwenye arusi
hukutaarifiwa ni kwa sababu arusi ilifanyika kisirisiri tu na mtu ambaye
alitokea huko mbali kwa kuwa ni tajiri baba alimkubali. Arusi ilifanyika usiku
wa manani mithili ya watu wakiwanga. Mriri nitakukumbuka, milele sitokusahau. Ili
kupata siku lazima pakuche na pakuchwe, basi mikono yetu itakutana Mungu
akipenda kutukutanisha. Mriri… mimi naamini wewe ndiyo msuluhishi wa haya
madhila yanayojitokeza katika jamii hii. Ukishinda yawezekana mikono yetu ikawa
rahisi kushikana.
Usitoe machozi ungali u
hai natumai udongo utajashikana na pengo litafutika.
Wasalamu,
Chiku aliyekupenda
milele.
25.05.2001
(Anamaliza kuisoma
barua ile na kuanza kumuangalia Salala. Anasahau kama Salala alimuaga
alipompatia barua. Anawafuata ng’ombe wake. Kidogo wamesogea kutoka pale
alipokuwa nao kisha wanazidi kusogea kwenye eneo lingine. Anaongea pekee yake)
MRIRI:
Kijiji
cha Upepo haya ni mambo gani kabisa inashikilia? Kwa sababu ni tamaduni ambazo
zimepitwa na wakati kabisa. Yaani watu tunapendana hivyo alafu kwa sababu ya
ukabila tu inatutenganisha kabisa. Hiki Kijiji kinahitajika kufundishwa kabisa
juu ya haya mambo. Ila Chiku lazima nimuoe tu hata kama huyo jamaa ameshamchukua.
Nitahama hii sehemu…
(Mandhari ya nyumbani, Huki na Kichiko
wamekaa kwenye kirago alafu Mriri amekaa kwenye kigoda)
MRIRI:
Mama… dada… nimewaiteni hapa nina
jambo nataka kuwaambieni…
HUKI:
Jambo gani?
KICHIKO:
Kuna nini tena Mriri?
MRIRI:
Jamani mama baada ya kunihadithia
ile hadhithi yote… kwa sasa mimi najiona mamluki kabisa katika kijiji hiki.
HUKI:
Siyo hivyo mwanangu…
MRIRI:
Mama wala usiubishe ukweli… acha
mimi nirudi kwenye kijiji cha Mwanga… kijijini kwetu nikaanze kujenga huko.
Siku zote mkataa kwao ni mtumwa… acha mimi nikajenge kule… ipo siku jambo hili
litakuja kuisha tu.
KICHIKO:
Kwa hiyo Mriri ndiyo unataka
kutukimbia hapa?
MRIRI:
Si kwamba nawakimbia…
KICHIKO:
Kwamba…
MRIRI:
Huu ndiyo uhalisia tu… sina
namna… mimi naanza kujiandaa… baadae baba akirudi nitamwambia… kesho naanzisha
safari ya kwenda mwanga.
HUKI:
Mwanangu nashindwa hata kusema
maneno mengi… napenda kusema tu kwamba ufikapo huko nenda kaishi na watu
vizuri… yawezekana wewe ukawa ni mshindi mkubwa sana wa kuyaondoa matatizo yote
ya jamii hizi mbili.
MRIRI:
Yataisha tu.
KICHIKO:
Tunakuamini Mriri…
MRIRI:
Haya… mimi nilikuwa nawajulisha
tu hilo. Tulia mimi nikapangepange vitu.
KICHIKO:
Sawa.
(Sasa Mriri amehama kutoka katika Kijiji cha
Upepo na kwenda katika kijiji cha Mwanga. Nyumba yake ya miti. Kwa juu
imeezekwa kwa nyasi huku ikiwa imepakwa matopematope kwa namna yake na kuficha
vitu vya ndani kutoonekana. Mriri yupo na jirani yake aitwaye Tuja. Tuja amekaa
kwenye kigoda amejifunika shuka ambayo inaficha hata nguo alizokuwa amevaa)
MRIRI: Unajua Tuja hiki Kijiji cha Mwanga kinasadifu
jina lake. Natamani sana tangu zamani ningekuwa naishi huku huku.
TUJA: (Anamuangalia
Mriri kwa sekunde kama mbili hivi kisha akasema). Kwa nini unaongea hivyo?
Mbona mimi nimeishi hapa muda mrefu sana lakini ninaona ni mahali pa kawaida
tu… au wewe unaonaje?
MRIRI: Aaa… unajua Tuja siku zote penye miti hapana
wajenzi.
TUJA: Unamaanisha nini?
MRIRI: Maana yake wala haihitaji mwalimu wa
elimu kubwa sana. Maana yake kwanza msemo huu ulianzishwa na wahenga na hata
hao wahenga wenyewe hawakuwa na elimu yoyote juu ya misemo kama hii waliyokuwa
wakiijadili.
TUJA: Naomba unipatie maana yake.
MRIRI: Namaanisha
kuwa… katika sehemu fulani panaweza kuwa na watu wenye kitu fulani na watu hao
unakuta wapo tu hapo lakini wanashidwa kufanyia kazi kitu kilichopo katika
sehemu hiyo. Mfano vitu tulivyojaaliwa katika bara letu ni vingi sana lakini
walio nje ndiyo wanaoviona thamani yake.
TUJA: Kivipi?
MRIRI: Yaani tuna mali nyingi au vitu vingi lakini
hatuna uwezo wa kuvifanyia kazi mwisho wa siku tunaanza kuagizia hata majirani
ili kuleta mafanikio. Sasa ndiyo ukikuta watu mliowaomba hawana utu basi nao
wanaamua kujifaidisha kwanza wao ndipo wawafaidishe nanyi. Hii ni shida kubwa
sana iliyoko katika Bara la Dunia ya zamani. Sasa nikiunganisha na hapa kwenu
ni kwamba kwa sasa watu wapo katika hiki kijiji lakini kuna wachache ndiyo wanaoelewa
faida kubwa iliyopo katika kijiji chao. Ndiyo maana hata maendeleo ya kiuchumi yanakuwa
namna hivyo.
TUJA: Ahaaa…
sawa nimekuelewa.
MRIRI: Hapa
Mwanga kuna neema sana. Kwa baadhi ya wananchi wanaojua kabisa ndiyo maana
kwamba kuna wachache wanafaidika kupitia vitu vilivyopo katika kijiji hiki.
TUJA: Kwa
nini tangu mwanzo hukuishi hapa Mwanga?
MRIRI: Aaa…
Tuja ni historia ndefu sana. Nimeishi katika Kijiji cha Upepo kwa muda mrefu
sana lakini baadae nilikuja kuonekana ni mamuluki. Baada ya mimi kujua hivyo
ndiyo nikaamua kuja kwenye kijiji changu. Embu tuachane na hayo mazungumzo na
tuangalie mengine. Sababu kuna baadhi ya mambo yanaumiza sana.
TUJA: Sawa
ndugu yangu. Haya nambie vipi kule shambani umeshapaandaa vizuri?
MRIRI: Ndiyo
nimeshapaandaa vizuri. Hapa yenyewe ndiyo nilikuwa na mpango wa kuanza safari
ya kuelekea huko shambani. Kwa sababu kuna baadhi ya visehemu vinatakiwa
kumaliziwa polepole tu si unajua harakaharaka haina Baraka.
TUJA: Ndiyo
ndiyo… natumai hadi kesho kutwa hivi tunaweza kuingia shambani na kuanza
kulima.
MRIRI: Ndiyo.
TUJA: Basi
sawa. Acha na mimi nikajiandae na yangu. Kwa sababu nilimuaga mama watoto
nikamuahidi nikisharudi ndiyo tutoke wote kwenda hospitali. Kwa sababu ni mbali
sana na nikiangalia hali ya mama watoto si nzuri sana. Kwa hiyo inabidi nikaandae
ile baiskeli vizuri ili tuende na usafiri wa baiskeli.
MRIRI: Sawa
jirani. Msalimie shemeji.
TUJA: Sawa.
Jitahidi na wewe upate mwenza bana. Sababu kukaakaa hivi hivi tu wala si vyema.
Wewe mwanaume bana…
MRIRI: Haya
bana… sawa… utani mwingine wa ukweli (Anaitikia
kwa sauti ya chini)
(Tuja anainuka na kulirusha shuka lake vizuri
mabegani)
ONESHO LA TANO
(Ni miaka minne imepita tangu Mriri kuhamia
katika Kijiji cha Mwanga, Sasa Mriri ni Mbunge wa Wilaya ya Muungano,
wanaonekana Mriri, Majuto ambaye ni diwani, Isuja ambaye ni mwenyekiti wa
kijiji cha Upepo, Kidima ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Mwanga, Kidudu ni
kiongozi wa wafugaji na Chapa ni kiongozi wa wakulima na viongozi watatu kutoka
ngazi ya juu ya serikali. Mriri amekaa kwenye meza moja na viongozi hao wa
ngazi ya juu ambao ni Bwanari, Kinara na Jafari)
MRIRI:
Habarini za muda huu ndugu
wajumbe?
WOTE:
Salama kabisa…
MRIRI:
Jambo jema… aaa kabla ya yote
ninapenda kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana katika kikao hiki
maalumu chenye malengo chanya katika jamii hizi mbili na Muungano kwa ujumla.
Lengo kuu la kikao hiki ni kujadili namna nzuri ya kuleta Amani katika vijiji
viwili ambavyo ni Upepo na Mwanga. Hapa mezani kwangu niko na wasuluhishi
katika ngazi za juu za serikali ambao wamekuja kwa malengo mazuri ya kuleta
Amani katika jamii hizi mbili. Nimewasumbua usiku na mchana hadi waje na kuweza
kulimaliza jambo hili. Labda niweze kumkaribisha kila mmoja ajitambulishe na
kuongea lake kidogo juu ya mada hii. Karibu…
BWANARI:
Habarini za muda huu?
WOTE:
Salama…
BWANARI:
Aaa… kwa jina naitwa ndugu Bwanari Tafao
Nkija ni afisa msuluhishi kutoka katika ngazi ya wilaya. Lengo la sisi kuwepo
katika kikao hiki ni kutaka kuweka alama ya Amani katika jamii zetu… madhara ya
kutoweka kwa Amani tumejionea… hatuna haja ya kuendelea na vita kila siku
ambayo haina maana yoyote. Mimi yangu ni machache bali mheshimiwa mbunge hapa
ndiyo mkaziaji zaidi. Ahsanteni.
MRIRI:
Ahsante sana… anayefuatia.
KINARA:
Habarini za muda huu?
WOTE:
Salama…
KINARA:
Kwa jina naitwa Kinara Rasul Butuka,
nami ni afisa msuluhishi kutoka wilayani. Tumekuja hapa kwa lengo la usimamizi
wa saini hizi. Sina mengi… nashukuru.
JAFARI:
Ninaitwa Jafari Mukulu, kama
walivyojitambulisha maafisa wengine ndiyo wadhifa wangu. Sote tumekuja hapa
tukiwa tumelenga kuleta Amani.
MRIRI:
Tunashukuru kwa utambulisho wenu.
Aaa… ndugu wajumbe kikao hiki ni chachu kwa maendeleo ya wilaya ya Muungano… hapa
kuna viongozi wa jamii zote mbili. Kila mmoja natumai amejionea hali halisi
iliyopo kutokana utengano tuliooneshana kwa miaka mingi. Sisi tukiwa kama viongozi… basi sisi ndiyo
tunatakiwa kuwa mbele katika kutafuta namna ya kuondokana na balaa hili. Hapa
tumeitana kwa ajili ya kuja kuweka jina moja la vijiji hivi ambalo litakuwa ni
muungano na ishara ya Amani na upendo katika vijiji vyote. Kabla hatujafikia
hatua ya kwenda kuitisha mkutano wa kuwakutanisha wananchi wa vijiji vyote
hivyo lazima kwanza sisi viongozi tuwe na kauli moja yenye malengo chanya. Tuondokapo
hapa kila mmoja awe amejua siku fulani litafanyika jambo fulani na litakuwa
hivi na vile. Kwa ujumla hiki si kwamba ndiyo kikao cha kwanza mimi kukaa, bali
ni cha kwanza kukaa na viongozi hawa kwa pamoja. Vile vile kwa ngazi za juu
tumekaa sana vikao na kuweza kutengenez jina moja ambalo litaonesha umoja na
mshikamano wa vijiji hivyo. Hivyo, nikiwa kama mwenyekiti wa kikao hiki
ninapenda kusema kuwa jamii hizi zitaungana na kupatikana kwa jina moja
liitwalo UNGA ikimaanisha Upepo na Mwanga. Haya ni mambo ambayo tulikubaliana
kutoka katika ngazi ya juu. Basi kwa muda huu nipende kusikia lolote kutoka kwa
wajumbe wa pande zote. Karibuni.
KIDIMA:
Mheshimiwa mbunge na mwenyekiti wa
kikao hiki nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika kikao hiki. Kwanza
niseme natoa pongezi kubwa sana kwa jitihada zako. Hakika ni kazi kubwa sana
uliyoweza kufanya… kweli wewe ndiyo mshindi wa hili. Unastahiki kupewa sifa
zote… hakika naweza kusema wewe ndiyo msuluhishi mkubwa katika hili. Kwa
ujumla, mimi nipo tayari kulipokea jina hilo. Sijajua kwa wenzangu.
WOTE:
Sote tumekubaliana… umoja na
mshikamano udumu.
MRIRI:
Jambo jema… bila kupoteza muda… maafisa
embu toweni zile karatasi za maridhiano kila mmoja wetu aweke saini (Maafisa wanatoa karatasi na kuanza kupitisha
kwa kila mjumbe)
(Ni saa kumi alaasiri. Mriri anahutubia watu
katika uwanja wa Makutanoni. Amevaa tisheti ya rangi nyekundu na suruali nyeusi
ya jinsi. Wananchi wanaonekana wana furaha sana kwa kiongozi wao kuwakutanisha
katika uwanja wa makutanoni. Walinzi wanaonekana wamevimba kama mbuyu. Wako
makini wakiwa wanamlinda kiongozi wao. Jukwaa limependezeshwa kwa kanga za
rangi mbalimbali zilizofungwa kwa ustadi wa hali ya juu)
MRIRI: (Anaongea
kwa sauti ya kikakamavu ambayo inafanya wananchi wote wakae kimya na kusikiliza
kwa makini. Anaanza kwa kuwasalimia wananchi). Habarini ndugu wanakijiji?
WANAKIJIJI:
(Wanapokelea kwa sauti ya juu)
Salamaaa...
MRIRI: Ndugu
wanakijiji wa Upepo na wanakijiji wa Mwanga leo hii nimeamua kukuiteni katika
uwanja huu wa Makutanoni ukiwa ni kama uwanja wenye historia kubwa sana kati ya
makabila haya mawili. Nina madhumuni machache ya kuwakutanisha wanakijiji wa
pande zote mbili nikiwa kama mbunge wa mkoa wa Muungano hili ni jukumu langu.
Ni miaka mingi sana tangu mapigano makubwa ambayo yalishawahi kutokea katika
kijiji cha Upepo. Ni historia kubwa sana ambayo imebaki kwa makabila haya
mawili… kwa historia ilivyo… imenifanya sana mimi kufanya mazungumzo ya karibu
sana ili kuweza kupata mkutano wa pamoja ili kuweza kuyasuluhisha mambo haya.
Kwa sababu utengano huu unaleta madhara makubwa sana katika jamii hizi mbili.
Tulikaa vikao mbalimbali vya mwanzo na viongozi wa ngazi zote ili kulimaliza
suala hili. Suala la ukabila kwa kweli ni suala baya sana ndiyo na huwa
silipendi sana suala hili na ndiyo maana hata nikiwa bungeni suala hili huwa
nalizungumza kwa hasira sana. (Analichangamsha
jukwaa). Wanakijiji mpooo?
WANAKIJIJI:
(Wanapokelea kwa sauti ya juu sana).
Tupooo...
MRIRI: Nafurahi
kusikia hivyo. Hivyo, nikiwa kama mbuge wa mkoa wa Muungano ninapenda kutangaza
kuwa kuanzia leo kijiji cha Upepo na kijiji cha Mwanga vinaungana na kuwa
kijiji kimoja kiitwacho UNGA.
WANAKIJIJI:
(Wananchi wanafurahi kwa shangwe kubwa
baada ya kusikia maneno yale ya mbunge wao.
MRIRI:
Sasa ni muda wa wanakijiji wa
vijiji vyote kukaa kwa pamoja… tupeane mikono kwa furaha na tubadilishana zana
zetu za kazi.
WANAKIJIJI:
(Wanapeana mikono, mwenye jembe
anabadilishana jembe na mwenye fimbo kama ishara ya Amani na upendo katika
muungano. Kwanzia muda huo wananchi wote wanaanza kujichanganya na kukaa kwa
pamoja huku wakiwa na furaha)
MRIRI: (Mriri
anaendelea na hotuba yake). Leo ni siku ya furaha sana. Hivyo, kwanzia sasa
tutakuwa na kijiji kikubwa kiitwacho UNGA ikiwa inamaanisha kuwa Upepo na
Mwanga. Nimeamua kutangaza muungano huu ni baada ya kufanya majadiliano na viongozi
wangu wa juu na chini na kuwapa hoja zenye nguvu juu ya muungano huu. Muungano
huu utafaidisha sana kwa pande mbili zote. Mojawapo ni kuzidi kuleta Umoja na
mshikamano kati yetu. Sote tunategemeana mkulima anamtegemea mfugaji na mfugaji
anamtegemea mkulima. Kilimo kitazidi kunawiri sana. Viongozi watakuwa
wanabadilishana sana mawazo yakiwa ni ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Suala la ukabila litakuwa limeisha na kila mtu kuanza kumthamini mwenzake kwa
kuwa kila kabila lina heshima yake. Pia ni matarijio yangu kuwa UNGA kwa miaka
michache ijayo mbeleni kwakweli kutakuwa na maendeleo ya kila aina. Miundombinu
itazidi kukuwa, viwanda mbalimbali vitaanzishwa kwa kuwa hapa UNGA kuna
malighafi za kutosha sana kama vile mifugo na mazao tofautitofauti. Kuna
vivutio mbalimbali vya kiutalii. Vivutio hivi vitakuwa vya wananchi wote yaani
wananchi wa UNGA si kusema tena kwamba wananchi wa Upepo wala wananchi wa Mwanga
bali ni wananchi wa UNGA. Nikiwa kama Mbunge wenu kwa muda wote nitakaokuwa
madarakani natumai kutakuwa na mabadiliko mengi sana yenye kuleta maendeleo.
Nilikuwa nachukizwa sana na hali ya kiuchumi iliyokuwako katika kijiji cha
Upepo pamoja na kijiji cha Mwanga. Nitaimarisha elimu kwa hali na mali ili tuweze
kupata viongozi katika sekta mbalimbali wenye ujuzi mzuri katika sekta zao. Katika
kijiji cha UNGA kuna utajiri mkubwa sana wa misitu. Katika misitu iliyopo kuna
miti ambayo inawezakutufaidisha sana kama tukiitumia vilivyo. Ninawaahidi
nikiwa kama kiongozi wenu na ninyi ndiyo mmpenipatia nafasi ya mimi kuwa
bungeni lazima niwaletee mafanikio ya mimi kuwako pale. Ndugu wana UNGA nisiwe
na mengi ya kunena sana bali nipende kumaliza kwa kusema kuwa nikushukuruni
nyote kwa kuweza kunisikiliza kwa makini na kuweza kuonesha nderemo
palipohitajika nderemo. Pia nazidi kuwaahidi kuwa matunda mengi yatakuja kwaajili
ya muungano huu. Kwa sasa tusherehekee kwa amani muungano wetu huu. Ahsanteni
sana. (Anashuka kutoka kwenye jukwaa huku
akiwapungia mikono, wananchi wanampigia vigelegele)
(Mandhari
ya nyumbani kwa Mriri, Mandhari ya sasa si kama mwanzoni alipohamia. Nyumba
tatu zikiwa zimezungushiwa ukuta mrefu. Kuna askari mmoja. Pembezoni mwa ukuta
ule kuna miti mbalimbali ya matunda kama vile miti ya matopetope, mastafeli,
maparachichi, miembe ya mbegu fupi na machungwa. Getini anaingia Kitori. Askari
anamsimamisha na kuanza kumuuliza maswali juu ya ujio wake)
ASKARI:
(Amevaa
mavazi ya kiaskari ya rangi ya kaki, amening’iniza bunduki begani). Mama
habari yako?
KITORI:
(Anaongea kwa woga). Sa… salama...
ASKARI: Una
shida gani asubuhi hii unakuja kwa Mbunge?
KITORI:
Nina mazungumzo naye ya kifamilia.
Ninatumai mtakuwa mna taarifa kuwa mbunge anataka kuoa. Kwa hiyo anataka kumuoa
mwanangu.
ASKARI:
(Anamfungulia
geti anaingia, askari anafunga geti kisha anampeleka) Sawa… twende huku.
(Askari anatangulia huku Kitori akiwa
anamfuata nyuma. Anampeleka hadi kwenye hicho chumba cha mazungumzo. Askari
anatoka pale na kwenda kumjulisha Mriri kuwa kuna mgeni wake. Mriri anatoka akiwa anajua ana mazungumzo ya
kiofisi kwa namna alivyovaa tu. Amevaa
suti nyeusi na shati likiwa jeupe huku akiwa amening’iniza tai vizuri. Anafika
kwenye chumba hicho anakutana na sura ya Kitori anasimama kwanza hapo kama
sekunde mbili hivi. Kitori anasimama na kumsalimia)
KITORI:
Shikamo kiongozi. Natumai
unanikumbuka. (Anaongea huku anatetemeka).
MRIRI: (Anaongea huku anaeleka kukaa kwenye kiti chake). Sidhani kama mimi
ni mkubwa hivyo hadi kufikia kunisalimia mama. Wewe si Kitori… Mama yake Chiku?
KITORI:
Ndiyo ni mimi.
MRIRI: Sawa. Heshima yako mama…
KITORI: Sawa.
MRIRI: Natumai kuna usalama huko ulikotoka.
KITORI: Ndiyo
kuna usalama wa kutosha kabisa. Kuna taarifa nilikuwa nakuletea.
MRIRI: Nitaarifu.
KITORI: Nakumbuka
tangu zamani wewe ndiyo mchumba wa Chiku. Pia wewe ndiye kijana wa kwanza kwa
kipindi kile kuja kunijulisha kuwa unataka kumuoa Chiku. Ila kwa hali ya
kipindi kile ilivyokuwa ikashindikana wewe kufanikisha malengo yako.
MRIRI: Nhaam nakumbuka. Vipi kwa sasa ana watoto
wangapi na wote hawajambo?
KITORI: (Anajibu huku akiwa anaangalia chini kwa aibu).
Hawakuweza kupata mtoto. Kwa sababu hawakuishi hata kwa mwaka mmoja. Yule mume
wake kumbe kipindi hicho tayari alikuwa ana wake wanne na Chiku akawa wa tano.
MRIRI: Kwa hiyo ikawaje?
KITORI: Wameshaachana.
Chiku aliamua kurudi nyumbani. Kwahiyo ndiyo maana nikaamua kuja kwako kuleta
taarifa hii. Kwakuwa tumeshaungana na hamna ukabila kwa sasa basi nikasema Mriri
ndiyo mwanaume wa kwanza kwa Chiku basi nije nikutaarifu hili kuwa Chiku bado
anakupenda na anahitaji umuoe.
MRIRI: (Ananyamaza kama sekunde tano hivi kisha
anamjibu). Aaaa Kitori unajua wengi hatujui kwanza ndani ya sekunde fulani
nini kitatokea kwa mtu fulani… hatujui leo wala kesho patakuwaje kwa mtu fulani.
Ila nashukuru nimejua tabia yako ilivyo japo kwa tabia hiyo sina haja nayo bali
mimi nina haja na Chiku. Nasema bado nampenda Chiku na maandalizi yanaanza…
kwanza Chiku niliwahi kuzungumza naye kwa haraka tu kabla hatujaungana. Nataka
kweli nioneshe mimi nimeungana na watu wa Upepo.
KITORI: (Anaipokea taarifa ile kwa furaha zaidi).
Ahsante Mriri. Wewe ndiyo mwanaume pekee kwa Chiku.
MRIRI: Sawa.
KITORI: Sawa Mriri.
MRIRI: (Anamuita
askari) Askari aliyepo hapo nje amuite dereva wangu sasa hivi.
ASKARI:
Sawa mkuu. (Mlinzi anaenda haraka kumuita dereva)
MRIRI: Sasa
kuna dereva atakuja hapa ndiye atakayekupeleka hadi nyumbani. (Anaingiza mkono mfukoni, anatoa noti kazaa
na kumpatia Kitori). Sasa hizi fedha chukua umpelekee Chiku ili akafanye
manunuzi ya nguo nguo na baadhi ya vitu na itakayobaki hapo utachukua nawe
yako.
KITORI: Nashukuru
sana.
MRIRI: Sawa.
(Dereva anaingia, amevaa suti nyeusi. Mriri anampa
maelekezo pale kisha Kitori anamuaga Mriri. Anatoka nje. Mriri anabaki pale
pale akiwa anafurahi)
(Ni siku ya arusi, arusi ya Mriri na Chiku,
kwenye ukumbi watu wamekusanyika kutoka katika sehemu mbalimbli. Ukumbi
umepambwa kwa mapambo ya aina mbalimbali. Viongozi wa serikali wenye nyadhifa
tofautitofauti wamehudhuria katika arusi hiyo. Watu wamekaa kwenye viti kwa
mpangilio maalumu. Magari ya viongozi yapo sehemu hayo husika na magari ya watu
wa kawaida yapo katika sehemu maalumu iliyotengwa. Mshindi anaonekana kwa
mbalimbali akisalimiana na viongozi wenzake. Amevaa suti nyeusi. Naye mama
Kichiko anaonekana kwa mbali akiwa amekaa na akina mama wengine. Mshereheshaji
anasikika akisema)
MSHEREHESHAJI:
Sasa ni ule wakati wa kupata chakula… Dj wapatie watu wimbo waasili watu
waburudike wakati wanapata chakula.
Tafsiri
Viyendire viyendire, Wamependana wamependana,
Vareki haha vakaboye yavo, Waacheni sasa wakafanye yao,
Ni muda wavo haha, Ni muda wao sasa,
Kusina wovadalavya, Hakuna wa kuwagombeza,
Familia vakajenga, Familia wakajenge,
Lukolo vyakakuryee, Ukoo wakaukuze.
MWISHO
Karibuni sana ndugu katika tamthiliya hii. Ni tamthiliya inayoelimisha sana. Maoni yako ni ya msingi sana...
ReplyDeleteKijiji cha Upepo ni tamthiliya inayozungumzia zaidi matatizo ya kijamii yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali. Mwandishi anajaribu kuikumbusha jamii ya sasa kuonesha uhalisia wa suala la ukabila kwa miaka ya nyuma watu walivyokuwa wameubeba bila kujali madhara yake. Mwandishi anaona kuwa ni vyema jambo hili viongozi wa ngazi zote wakajitoa mhanga katika kuweza kusimamia suala hili. Ni vigumu jamii moja na jamii nyingine kusuluhishana hadi aweze kutokea kiongozi mwenye kuona thamani ya kutokuwa na migogoro katika jamii hizo. Vilevile, mwandishi anawakumbusha viongozi wa mataifa ya kusini mwa dunia kuwa huu ni wakati wa kusimama kwa pamoja ili kuvifaidi tulivyonavyo. Tusipofanya hivyo lazima tutazidi kuwaabudu wageni kuja kutupatia msaada angali mali tuliyonayo ni zaidi ya msaada tunaopewa.
ReplyDeleteKaribuni sana
ReplyDelete